Na; Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema Biashara ya Kaboni ni moja ya fursa za kiuchumi zinazoweza kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuwanufaisha wakulima.
Amesema kupitia kilimo himilivu na kilimo mseto ambapo wakulima wanaweza kushiriki katika miradi ya Biashara ya Kaboni na kupata mapato ya ziada sambamba na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Masauni ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuhusu Ufadhili wa Kijani kwa sekta ya kilimo 2025–2027, iliyofanyika Mei 12, 2026 jijini Dar es Salaam.
“Kupitia upanuzi wa huduma za kifedha, matumizi ya mifumo ya kidijitali na ushirikiano na taasisi nyingine za kifedha, wakulima wengi zaidi watanufaika na mikopo, elimu ya kifedha na fursa za uwekezaji katika kilimo cha kisasa.”
Taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo wanapaswa kuendelea kusaidia uwekezaji katika miradi hiyo na kujenga uwezo wa wananchi kushiriki kikamilifu katika soko la kaboni.
“Ushirikiano madhubuti kati ya taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi za kifedha, taasisi za utafiti, asasi za kiraia pamoja na sekta binafsi utakuwa muhimu katika kuhamasisha rasilimali, kuongeza ubunifu na kuwawezesha wakulima kuhamia katika kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.” Amesema Mhe. Masauni.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alisema mkakati huo umekuja muda mwafaka kutokana na Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa kwenye mipango ya uzinduzi wa Mkakat wa Kukijanisha Tanzania.
“Mkakati huu utahitaji fedha na utagusa maeneo yote ambayo yataendana na Dira ya 2050, lakini hautaweza kufanikiwa na kufika mbali kama hakuna taasisi ambazo zitasaidia fedha ili kuwafikia wananchi kwenye mambo ya msingi kama kilimo,” amesema Dkt. Muyungi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Frank Nyabundege amesema kutokana na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kumeendelea kushuhudiwa madhara makubwa katika sekta ya kilimo nchini.
“Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya kilimo imekuwa ikikumbwa na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. Kuanzia mvua nyingi zaidi zinazosababisha mafuriko makubwa hadi ukame wa muda mrefu unaotokana na ongezeko la joto kali.
“Mabadiliko haya ya hali ya hewa yanaendelea kuhatarisha uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula, na kipato cha wananchi wa vijijini kote nchini.”
“Tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaisababishia sekta ya kilimo nchini hasara ya wastani wa dola za Marekani milioni 28 kila mwaka kutokana na kupungua kwa uzalishaji, sambamba na hasara ya wastani wa dola milioni 140 kila mwaka inayotokana na mafuriko na ukame.” Amesema Bw. Nyabundege.













No comments:
Post a Comment