Pemba, Zanzibar | 30.04.2026. Kampuni ya
huduma za fedha kidigitali, Mixx, imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya
kuimarisha uchumi wa wakulima wa karafuu Zanzibar kwa kukabidhi hundi mbili
zenye jumla ya shilingi milioni 175 kwa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar
(ZSTC).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya
ya Mkoani-Pemba, Mhe. Mizza Hassan Faki alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi
endelevu za kampuni katika kuboresha maisha ya wakulima na kuleta mapinduzi
katika sekta ya kilimo kupitia suluhisho za kifedha za kidigitali.
Katika makabidhiano hayo, Mixx ilikabidhi
hundi ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa wakulima
wa zao la karafuu, hatua inayokamilisha ahadi ya jumla ya shilingi milioni 350
kutoka Mixx kwenda ZSTC.
Aidha, hundi nyingine ya shilingi milioni 25
ilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa miche 25,000 ya karafuu, ikiwa ni mkakati wa
kuendeleza zao hilo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Vilevile, hafla hiyo ilishuhudia zoezi la
upandaji wa miche ya karafuu, ikiwa ni ishara na dhamira ya pamoja katika
kukuza na kulinda zao hilo.
Akielezea umuhimu wa ushirikiano huo, Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mixx, Bi. Angelica Pesha alisisitiza kuwa ushirikiano wa
kimkakati kati ya Mixx na ZSTC umejengwa katika msingi wa kuhakikisha wakulima
wanapata huduma bora za kifedha zinazowawezesha kuongeza tija na kipato chao.
Alibainisha kuwa kupitia mfumo wa malipo
kidigitali wa Mixx, kumekuwa na uwazi, upungufu wa upotevu wa fedha, na
kuimarika kwa imani ya wakulima kwa taasisi zinazosimamia sekta hiyo.
“Tunaamini kuwa teknolojia ya kifedha ina
nafasi kubwa katika kubadilisha maisha ya wakulima. Kupitia Mixx, tumefanikisha
malipo ya haraka, salama na yenye uwazi, na kuondoa changamoto za ucheleweshaji
wa malipo zilizokuwepo hapo awali,” alisema.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, katika
msimu wa karafuu wa 2025/2026, Mixx kwa kushirikiana na ZSTC imefanikiwa
kufanya malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 48 kwa wakulima wa Zanzibar.
Hatua hiyo pia imechangia kuongezeka kwa ajira,
ambapo zaidi ya mawakala 11,000 wamepata ajira na kushiriki katika mnyororo wa
utoaji huduma za kifedha.
Aidha, Mixx ilitangaza mipango ya kuanzisha
huduma ya mikopo nafuu kwa wakulima wa karafuu, inayotarajiwa kuanza kabla ya
msimu wa 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wakulima kuwekeza
zaidi katika uzalishaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZSTC, Ndugu Soud
Said Ali, alieleza kuwa ushirikiano na Mixx umeleta mageuzi makubwa katika
mfumo wa malipo kwa wakulima, na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa zao la
karafuu.
Mixx imeendelea kuahidi kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ZSTC pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha sekta ya karafuu inakuwa ya kisasa, yenye tija na endelevu kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.









No comments:
Post a Comment