Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Hydrocarbons wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mhe. Acacia Bandubola Mongo, kwa lengo la kujadili masuala yatakayoimarisha ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
Ushirikiano huo ni katika utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na utekelezaji wa miradi ya usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za petroli ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo nchini DRC.
Kikao hicho kimefanyika Mei 7, 2026 katika Ofisi za Wizara ya Nishati, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Ndejembi amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali kubwa ya gesi asilia na inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu ya mafuta na gesi, ikiwemo mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania pamoja na mradi wa bomba jipya la TAZAMA.
Amesema miradi hiyo inaweza kufungua fursa zaidi za ushirikiano kati ya Tanzania na DRC, hususan katika usambazaji wa bidhaa za petroli na maendeleo ya sekta ndogo ya mafuta, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi wa biashara ya nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Mataifa yetu yana nafasi kubwa ya kushirikiana katika kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya wananchi wetu na kukuza uwekezaji pamoja na biashara ya nishati katika ukanda huu,” amesema Mhe. Ndejembi
Kwa upande wake, Mhe. Acacia Bandubola Mongo amepongeza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuendeleza sekta ya nishati na kueleza utayari wa DRC kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya mafuta na gesi asilia.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw. Mussa Makame, Kamishna wa Petroli, Bw. Goodluck Shirima, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, pamoja na wataalam kutoka Wizara ya Nishati nchinj na Wizara ya Mafuta ya DRC.










No comments:
Post a Comment