LICHA YA MAAGIZO YA SERIKALI, MTOTO MWENYE USONJI AENDELEA KUSOTA NYUMBANI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, May 6, 2026

LICHA YA MAAGIZO YA SERIKALI, MTOTO MWENYE USONJI AENDELEA KUSOTA NYUMBANI


 Mtoto Swaum Shabani Machela (14), akiwa amepakatwa na Mama yake Sauda Selemani nyumbani kwao..

.................................

Na Mwandishi Wetu

MTOTO Swaum Shabani Machela (14), mkazi wa Mtaa wa Kibong’wa, Pugu kwa Mustafa wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, anaendelea kusota nyumbani licha ya kuwepo kwa maagizo ya serikali ya kuhakikisha anapatiwa matibabu.

Swaum, ambaye anasumbuliwa na maradhi ya usonji, aligusa hisia za wengi baada ya taarifa yake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Mei 2, 2026, ambapo mama yake, Sauda Selemani (42), aliomba msaada wa matibabu pamoja na mahitaji ya msingi kutokana na hali ngumu ya maisha anayopitia.

Kufuatia taarifa hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alichukua hatua kwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Tiba na kuagiza suala hilo lifanyiwe kazi mara moja ili mtoto huyo apate huduma stahiki.

Akizungumza na mwandishi wetu, Sauda alisema baada ya maagizo hayo, alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Pugu, kwa jina la Prisca Kaminsa. 

Kwa mujibu wa Sauda, afisa huyo alimueleza kuwa amepokea maelekezo kutoka kwa waziri na kupanga kufika nyumbani kwake Mei 4, 2026 ili kumuangalia mtoto huyo.

Hata hivyo, Sauda alisema kuwa licha ya ahadi hiyo, afisa huyo hakufika kama ilivyopangwa. Badala yake, alimjulisha kuwa angefika siku iliyofuata majira ya saa 12 jioni, lakini pia hakutokea.

Aliongeza kuwa mawasiliano yaliendelea, ambapo aliahidiwa tena kufika asubuhi ya Mei 6, 2026, lakini hadi leo hii Mei 7, 2026 hakuna aliyefika nyumbani kwake na kuwa simu yake wakati wote ipo hewani.

“Kutofika kwake kunanifanya nishindwe hata kufanya shughuli nyingine za kutafuta riziki, huku nikiendelea kuteseka na mwanangu. Licha ya Mheshimiwa Waziri kuonesha dhamira ya dhati ya kutusaidia, bado hatujapata msaada huo,” alisema Sauda kwa masikitiko.

Afisa Ustawi wa Jamii Prisca Kaminsa alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alidai kuwa mama wa  mtoto huyo alikuwa hapatikani kwenye simu baada ya kuahidiana kuwa angekwenda ambapo ameahidi kwenda leo hii.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umebaini kuwa kutoka Hospitali ya Pugu kwenda Pugu kwa Mustafa anapoishi mama huyo kwa mwendo wa gari haizidi hata dakika 10 jambo ambalo linasikitisha.

Hali ya kutotekeleza maagizo ya viongozi wa serikali kwa wakati, hasa katika masuala nyeti yanayohusu afya na ustawi wa jamii yanazua maswali mengi kwa jamii na kuonesha baadhi ya watendaji wanavyoshindwa kwenda na kasi ya utendaji kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad