Kiongozi wa Ujumbe wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kimataifa, Dkt. Doris Macharia (kushoto) na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi wakikabidhiana nyaraka kwenye mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kuboresha huduma za afya nchini Mei 4, 2026 Jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalihusisha timu nzima ya EGPAF Tanzania iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkazi, Dkt. Sajida Kimambo, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa.
..................................
Na Shaban Juma, Dodoma
Serikali imeongeza kasi ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Taasisi ya EGPAF, hatua inayolenga kutokomeza kabisa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.
Hayo yamesemwa na Dkt. Florencw Samizi, leo Mei 04, 2026 jijini Dodoma, alipokutana na ujumbe wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) ukiongozwa na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa kimataifa, Dkt. Doris Macharia, pamoja na timu ya EGPAF Tanzania inayoongozwa na Mkurugenzi Mkazi, Dkt. Sajida Kimambo, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kuboresha huduma za afya nchini.
Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea kujenga mfumo imara, endelevu na jumuishi wa afya, unaolenga kuimarisha huduma za mama na mtoto na kutokomeza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Amesema ziara ya ujumbe huo imelenga kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo tangu mwaka 2003, pamoja na kumtambulisha Dkt. Macharia kwa viongozi wa Wizara na kujadili vipaumbele vya nchi vinavyoendana na maeneo ya utaalamu wa taasisi hiyo ili kuimarisha ushirikiano zaidi.
Dkt. Samizi amebainisha maeneo ya kipaumbele ambayo Serikali itaendelea kushirikiana na EGPAF, ikiwemo kuimarisha ubora wa huduma za afya ya mama na mtoto ili kutokomeza maambukizi ya VVU, homa ya ini na kaswende kwa watoto wachanga, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika upatikanaji wa rasilimali fedha na msaada wa kiufundi ili kuhakikisha uendelevu wa huduma hizo, hasa katika kipindi hiki cha kupungua kwa ufadhili kutoka kwa wahisani.
Kwa upande wake, Rais wa EGPAF, Dkt. Doris Macharia, amesema taasisi hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele, ikiwemo kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji (sentinel surveillance) kwa ajili ya kubaini na kushughulikia maambukizi mapya kwa watoto.
Ameongeza kuwa EGPAF iko katika hatua za kujumuisha Tanzania katika mpango wake wa kimataifa wa Generation Zero Campaign, unaolenga kusaidia nchi kufanya uchambuzi wa vipaumbele na rasilimali zitakazohitajika ili kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU, homa ya ini na kaswende kwa watoto wachanga.
Pia amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa msaada wa kiufundi katika kufanya tathmini ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (Vertical Transmission Audit) pamoja na kusaidia kuandaa mfumo utakaowezesha maambukizi mapya kutambuliwa, kuripotiwa na kujadiliwa kwa lengo la kupata suluhisho, kama ilivyo kwa vifo vitokanavyo na uzazi.
Dkt. Samizi amesisitiza umuhimu wa kukamilika kwa wakati kwa taarifa ya uchambuzi wa vipaumbele na gharama zinazohitajika ili kutokomeza maambukizi kwa watoto wachanga, ili iweze kuingizwa katika mipango mikakati ya Wizara na maandiko ya miradi ya kutafuta rasilimali za utekelezaji.
Kiongozi wa Ujumbe wa Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF), Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Kimataifa, Dkt. Doris Macharia (kushoto) na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi wakionesha furaha zao baada ya mazungumzo.Mazungumzo yakiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye kikao cha mazungumzo
Kikao kikiendelea.















No comments:
Post a Comment