Wauguzi Mkoa wa Iringa wakijadiliana wakati wakitoa huduma bure kwa Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Garden Manispaa ya Iringa kupata huduma za afya bure kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yatakayofanyika Mei 12 mwaka huu.
............................
Na Godwin Myovela, Iringa
Mamia ya wananchi wamejitokeza katika viwanja vya Garden Manispaa ya Iringa kupata huduma za afya bure kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yatakayofanyika Mei 12 mwaka huu.
Huduma hizo zimeanza rasmi kwa lengo la kusogeza matibabu karibu na wananchi pamoja na kujenga uelewa na imani kwa jamii kuhusu sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk. Alfred Mwakalebela, amesema huduma hizo zinalenga kuwafikia wananchi wengi na kuondoa hofu ya baadhi yao kufika hospitalini.
Amesema wahudumu wa afya wanapaswa kutoa huduma kwa upendo, utu na lugha nzuri ili kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za afya.
Dk. Mwakalebela amesema maadhimisho hayo yanaakisi kaulimbiu ya mwaka huu isemayo, “Muuguzi wetu, mustakabali wetu, nguvu ya kiuchumi ya huduma za afya,” huku wauguzi wakitoa huduma kwa kujituma na ukaribu zaidi kwa jamii.
Katika Idara ya Afya ya Mama na Mtoto, wananchi wamepata huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, uzazi wa mpango, ushauri wa afya pamoja na elimu kwa vijana kuhusu ukatili wa kijinsia.
Aidha, vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza kama sukari, presha na uzito vinaendelea kutolewa sambamba na elimu ya afya ya akili, lishe na upimaji wa virusi vya UKIMWI bila malipo.
Wananchi wamepongeza huduma hizo wakisema zimeongeza matumaini na kuonyesha sura mpya ya sekta ya afya yenye ukaribu, utu na kujali mahitaji ya jamii.
Huduma zikiendelea kutolewa.Wanaanchi wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa afya
Wauguzi wakiwa katika uwajibikaji.
















No comments:
Post a Comment