...................................................
Na Dotto Mwaibale,Ikungi
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo,akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa ameendelea kuhimiza vijana
kujiunga na vyuo vya ufundi ili kupata mafunzo ya ufundi yatakayo wasaidia kupata
ajira pamoja na kujiajiri.
Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya
maendeleo alipokitembelea Chuo cha Ufundi Stadi cha Veta wilayani Ikungi mkoani Singida Februari 28, 2023 aliitaka Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanza kutoa elimu ya ufundi kuanzia
ngazi ya chini na kueleza umuhimu wake jambo litakalosaidia kuwavutia vijana
wengi.
Chongolo alisema mbali ya vijana kupata elimu hiyo aliiomba mamlaka hiyo
somo la kompyuta liwe la kawaida na la muhimu ili kila mwanafunzi alifahamu
kwani hivi sasa mambo mengi ya teknolia ya ufundi yanahusisha matumizi ya
kompyuta.
“Matumizi ya kompyuta yawe ya lazima katika mafunzo ya ufundi kuanzia ngazi
ya chini kutokana na umuhimu wake na kukua kwa teknolojia” alisema Chongolo.
Chongolo aliiomba Veta kuanza kutoa mafunzo hayo ya ufundi kuanzia shule za
sekondari lengo likiwa ni kuwaanda kujua umuhimu wa ufundi na faida zake.
Alisema lengo la Serikali ni kujenga vyuo vya Veta katika kila wilaya hapa
nchini ambapo katika miaka mitatu mfululizo imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi
bure na akaiomba Veta kujikita zaidi katika uhamasishaji wa vijana kujiunga
katika vyuo hivyo.
Aidha Chongolo alihimiza kila mtu
kujifunza walau fani moja ya ufundi bila kujali elimu aliyonayo ambayo haimzuii
mtu kuwa na ujuzi mwingine akijitolea mfano yeye ambaye ni fundi mahiri wa
kuchomelea vyuma lakini leo hii ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Chongolo alisema hivi sasa wapo vijana wengi hawana elimu ya ufundi na
wengi wana elimu ya juu hivyo ni muhimu kutengeneza msingi kuanzia shule za
sekondari.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya
Kati,John Mwanja, alisema ujenzi wa chuo cha VETA Ikungi ulianza katika bajeti
ya 2019/2020 ambapo hadi sasa Sh.bilioni 2.3 zimeshatumika katika ujenzi huo
ambao utakamilika Aprili mwaka huu.
Mwanja alisema Serikali imetoa Sh.milioni 259 ili kukamilisha ujenzi wa
chuo hicho na kwamba kitaanza kutoa mafunzo ya kozi ndefu kwa wanafunzi 240 na
wa kozi fupi kati wanafunzi 250 hadi 900 kwa mwaka.
Alisema
faida ya chuo hicho mara kitakapokamilika kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao
343,985 wa Wilaya ya Ikungi na wakazi wapatao 1,754,370 wa Mkoa
wa Singida.
Alisema
katika kutekeleza mradi huo VETA imekumbana na changamoto mbali mbali kama kupanda
kwa bei ya vifaa vya ujenzi wakati wakiendelea
na utekelezaji
wa mradi, hali iliyopelekea pesa iliyotengwa
kutokidhi mahitaji
halisi ya mradi kutokana na bei za vifaa kupanda
zaidi ya
matarajio ya awali.
.
Alitaja
changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni uwezo mdogo wa kiuchumi wa mafundi
waliowatumia hivyo kupelekea kushindwa kuwalipa vibarua wao kwa wakati na
kupelekea baadhi yao kuacha kazi, hivyo kupelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa
mradi.
Mwanja alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya vya Veta na uboreshaji wa vyuo vya zamani.
0 Comments