Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa (wa pili kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Msikiti wa Madina Ummul -Fatma Tungansanga uliojengwa Kijiji cha Kisiliga Kata ya Gumanga Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa ufadhili wa Taasisi ya Istikaama. Kushoto kwake ni Kadhi wa Mkoa wa Arusha Sheikh Rajabu Kiungiza.
Na Dotto Mwaibale,
Singida
KADHI wa Mkoa wa
Arusha Sheikh Rajabu Kiungiza amesema msukumo wa imani uliopo ndani ya mioyo ya
waislamu ndio unaowafanya waweze kupinga ndoa za kuoana kati ya mwanaume na
mwanaume na mwanamke na mwanamke.
Sheikh Kiungiza
aliyasema hayo jana katika hafla ya ufunguzi wa Msikiti wa Madina Ummul -Fatma
Tungansanga uliojengwa Kijiji cha Kisiliga Kata ya Gumanga Wilaya ya Mkalama
mkoani Singida kwa ufadhili wa Taasisi ya Istikaama.
"Hakuna kitu
kinachotusukuma kuyapinga matendo hayo zaidi ya imani ya Mwenyezi Mungu
tuliyonayo katika mioyo yetu na tukiwa na vitu hivi viwili yaani imani na ucha
Mungu tutavishinda vita hivi" alisema Sheikh Kiungiza.
Alisema wale wote
wanaowaingilia wanaume wenzao kwa matamanio badala ya wanawake na wanawake
wanaofanya mapenzi ya jinsia moja badala ya wanaume ni watu wanaofanya ujinga kabisa mbele za
Mwenyezi Mungu.
Sheikh Kiungiza
alisema mtu mwenye akili hawezi kufanya uchafu huo ambao hata mbuzi hawaufanyi
kwani huwezi kuona mbuzi mwanaume akimkimbiza mbuzi mwenzake mwanaume kwa ajili
ya kufanya uchafu huo au mbuzi wakike akifanya hivyo dhidi ya mbuzi mwenzake wa
kike.
"Inakuweje wewe
mwanadamu ambaye Mungu amekutukuza na kuwa
mwizi wa fadhira ambaye unaacha fadhira ulizofadhiriwa na Mungu na
kufanya machafu hayo ambayo ni zaidi ya wanyama ambao hawayafanyi, ndugu zangu
waislamu ni jukumu letu kupaza sauti ya kuyakataa mambo haya." alisisitiza
Sheikh Kiungiza.
Mwenyekiti wa
Taasisi ya Istikaama Mkoa wa Singida, Khalfan Salum akizungumza kwa niaba ya
wadhamini wa msikiti huo aliomba nyumba hiyo ya Mungu itunzwe na kufanyiwa
usafi ili tija ipatikane kwa kile kilichokuwa kimekusudiwa na si vinginevyo.
Sheikh wa Mkoa wa
Singida, Issa Nassoro Issa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema
watu wanaojitoa kuhimarisha ujenzi wa nyumba za Mungu (misikiti) hawana cha
kuogopa kwa kutoa kwao kwa hofu ya kufilisika na kuwa maskini ambapo
aliwashukuru wafadhili hao na kuomba
taasisi zingine ziige mfano huo.
Aidha Sheikh Nassoro
alitoa angalizo kwa taasisi zenye kufadhili ujenzi wa misikiti kuacha tabia ya
kutoa masharti kwa waumini kuhama katika madhehebu yao na kujiunga kwao na kuwa
jambo hilo sio nzuri na hawatakuwa tayari kushirikiana na taasisi hizo.
Sheikh Nassoro
alitumia nafasi hiyo kuwaomba Waislamu, wafadhili, watu binafsi na taasisi
mbalimbali kumuenzi Mzee Sheikh Ali Majid ambaye ni kikongwe wa kwanza katika
Manispaa ya Singida kujitoa na kuguswa kulitunza jengo la Masjid Taqwa kwa
wakati huo.
Alisema mzee huyo
aliguswa na hali iliyokuwa ikifanyika kabla ya kukamilika kwa jengo la msikiti
huo ambapo baadhi ya watu walikuwa wakifanyia mambo yasiofaa na mzee huyo kwa
mikono yake alikuwa akikata miba aina ya mitunduru na kuiweka kwenye milango na
madirisha ili watu hao wasiweze kuingia.
"Ninacho waomba
ndugu waislamu ni kuwa hivi sasa msikiti huo unataka kubadilishwa na kuwa wa
kisasa zaidi wa ghorofa na ili kumuenzi Sheikh Ali Majid nawaomba mchango wa
hali na mali ili tupate vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo kwani
tayari tuna nondo 1800 ambazo zimepatikana kutoka kwa baadhi ya watu walioguswa
na jambo hilo" alisema Sheikh Nassoro.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan Mlau aliipongeza taasisi kupitia wafadhili wao kwa kujenga msikiti wenye ubora wa hali ya juu ambapo kwa Wilaya ya Iramba na Mkalama imejenga misikiti 30, madrasa zikiwa tano na kuwa msikiti huo unaufanya Mkoa wa Singida kuwa na misikiti 677.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa akizungumza kwenye uzinduzi huo.Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro Issa akipeana mkono na wageni waalikwa baada ya kuzungumza kwenye uzinduzi wa msikiti huo
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Mkoa wa Singida Sheikh Burhan Mlau, akiwashukuru wafadhili kwa ujenzi wa msikiti huo.
0 Comments