Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai (kushoto) akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika semina iliyoandaliwa na MSD ambayo inafanyika mkoani Dodoma.
Na Dotto Mwaibale,
Dodoma
MGANGA Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa madaktari wa mikoa yote ya Tanzania Bara,
Best Magoma amesema suala la dawa na vifaa tiba halipaswi kuachiwa Bohari ya
Dawa (MSD) peke yao bali washirikishwe na wadau wengine ili kuleta ufanisi katika
upatikanaji wa dawa na vifaa hivyo.
Hayo yamesemwa na
Dk. Magoma wakati akitoa mada kwa Wahariri wa vyombo vya habari katika semina
ya siku mbili iliyoandaliwa na MSD ambayo inafanyika jijini Dodoma.
" Hili suala la
dawa na vifaa tiba katika upatikanaji wake wawe wanashirikisha wadau wengine
badala ya kuiachia MSD peke yake kulifanya,” alisema Magoma.
Alisema Serikali imetoa
Sh.Bilioni 200 kwa MSD kama ruzuku kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba na
kuwa hiyo ruzuku sio chanzo pekee cha kununua vifaa hivyo bali vipo vyanzo
vingine kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) malipo ya papo kwa papo
yanayofanywa katika vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali.
“MSD ni jitu kubwa
lenye mambo mengi hivyo haiwezi kufanya kazi zote hizo bila ya kuwashirikisha
wadau wengine na hapo ndipo mafanikio yatakapo patikana,” aliongeza Dk. Magoma.
Kuhusu suala la usambazaji
wa bidhaa za afya, Dk. Magoma alisema vituo vya kutolea hupokea bidhaa za afya
moja kwa moja kutoka MSD ( Direct Delivery) na kuwa mfumo huo wa usambazaji ni
kila baada ya miezi miwili na kwamba
mara sita kwa mwaka vituo vinapokea bidhaa za afya.
Magoma aliongeza
kuwa huduma za usamabazaji hufanyika kwa dharura pale vituo vinapokua na
mahitaji ya dharura na kuwa vituo vya kutolea huduma za afya vimegawanya katika
makundi mawili yaani group A & B,
Mganga Mkuu wa Mkoa
wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa madaktari wote wa wilaya Tanzania Bara,
Dk.Samweli Marwa alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza watumishi
watakao saidia kugawa dawa katika zahanati na vituo vya afya kwani wengi
wanaofanya kazi hiyo si wafamasia.
Alisema pamoja na
kuongeza watumishi hao wale wanaofanya kazi hiyo hivi sasa ni muhimu wakapatiwa
mafunzo na kwa kufanya hivyo kutakuwa na wigo mpana wa kuwasaidia wananchi.
Akielezea baadhi ya changamoto na utatuzi wake
Dk. Marwa alisema ni usambazaji wa bidhaa za afya kutofikia asilimia 100, mikoa
kutumia Washitiri ili kusambaza bidhaa zilizokosekana pamoja na kuchelewesha
kuwasilisha shehena za bidhaa za afya.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kusimamia vituo vya afya kutuma taarifa kwa wakati, vituo kushindwa kufikia angalau
asilimia 50 ya matumizi katika ununuzi wa bidhaa za afya.
Alisema njia nyingine ambayo itasaidia kupunguza changamoto hizo ni kuendelea kuwakumbusha wadau wa MSD kusimamia miongozo ya matumizi ya mapato na kuwajengea uwezo wadau hao na kuhakikisha taarifa zinakua na ubora.
0 Comments