|
Na Dotto Mwaibale, Singida ZAIDI ya Sh. Bilioni 1.1 zimetumika kwa ajili ya kukamilisha miradi
mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Unyianga, Manispaa ya Singida. Hayo yamebainishwa na Diwani wa kata hiyo, Geofrey Mdama wakati akitoa
taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo mbele ya wajumbe wa kamati ya siasa ya
Wilaya ya Singida wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Lusia Mwiru wakati
ilipokuwa ikikagua miradi hiyo juzi. Alisema shughuli za miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya
2020/ 2025 yenye nia ya kuwaletea wananchi maendeleo. Mdama alisema matumizi ya fedha hizo ni ujenzi wa barabara, zahanati na
madarasa ya shule shikizi, sekondari na Msingi. Alisema katika ujenzi wa barabara ya Unyianga hadi Mtamaa fedha
zilizotumika ni Sh.Milioni 168 ambapo barabara ya kutoka Unyianga kwenda
Mwankoko zimetumika Sh.Milioni 378. Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya Utalii kupitia Unyianga B ambayo
imetumia Sh. Milioni 146 sambamba na barabara ya Sima kwenda Unyianga B. Akizungumzia kuhusu ujenzi wa madarasa na zahanati alisema walipokea
Sh.Milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Unyianga ambayo ujenzi wake
umekwisha kamilika. Aidha, Mdama alisema walipokea Sh. Milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa shule
Shikizi na Sh.Milioni 25 nyingine kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili katika
Shule ya Msingi Unyianga. Alitaja fedha nyingine walizopokea ni Sh.Milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa
manne ya Shule ya Sekondari ya Unyianga. Alisema wamepokea Sh.Milioni 263 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule
za sekondari, msingi na uanzishwaji wa shule shikizi ya Unyianga B. Alitaja miradi mingine ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika ni
umeme,maji na zahanati ambayo itaanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo. Mdama alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fedha hizo ambazo zimeleta maendeleo makubwa katika kata hiyo. Aidha, kwa nafasi ya pekee ana mshukuru Mbunge wa Singida Mjini Musa Sima
kwa mchango wake mkubwa pamoja na uongozi mzima wa Manispaa ya Singida na
wananchi kutokana na ushirikiano wanaoutoa kufanikisha maendeleo katika kata
hiyo. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Lucia Mwiru alipongeza uongozi wa kata hiyo kwa utekelezaji
wa miradi hiyo kwa haraka na kwa ubora wa kiwango cha juu ambapo pia alitumia
nafasi hiyo kutoa nasaa kwa wazazi na walezi kusimamia maadili na malezi kwa
watoto wao. Aidha, Mwiru alihimiza suala zima la uhai wa chama pamoja na usajili kwa wingi wanachama kwa njia ya kielektroni. |
![]() |
Wananchi wakifurahia baada ya ukaguzi wa miradi hiyo. |
Shamra shamra zikiendelea.












No comments:
Post a Comment