Na Calvin Gwabara – Tabora.
MKOA wa Morogoro umejiandaa kunufaika na uwepo wa
viwanda vya usindikaji wa Tumbaku kwa kuanzisha kilimo cha zao la Tumbaku kwa
kuanzia na wilaya ya Gairo na katika kufanikisha adhma hiyo, ushirikishwaji wa
wataalamu wa zao hilo imekuwa sehemu ya mkakati huo muhimu kwa mkoa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya
Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA), Dkt. Jacob Bulenga Lisuma wakati
akizungumza na SUAMEDIA kuhusu mipango na fursa zinazoibuliwa na Taasisi hiyo
katika kukuza uzalishaji wa zao la Tumbaku nchini. Akitanabaisha zaidi juu ya
mkakati wa kuanzisha kilimo cha Tumbaku kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa na
wilaya, Mkurugenzi huyo alisema;
“Hivi karibuni mnamo mwezi wa nane nilialikwa
kwenye kikao cha baraza la madiwani Wilayani Gairo kushiriki mjadala wenye
lengo la kutafuta jinsi bora ya kulima Tumbaku na kulifanya zao hilo kuwa la
msingi wa kiuchumi ili kunufaika na uwepo wa Viwanda vya kusindika zao hilo
mkoani Morogoro. Hili lilizingatia kwamba wananchi wa Morogoro hawajaweza
kutumia vema fursa wanastahili kutokana na uwepo wa viwanda hivyo kwa sababu
hawalimi zao husika” alieleza Dkt. Jacob.
Aliongeza “Kwahiyo tulitembelea wilayani Gairo na
kuwapa ushauri ya kwamba wao waweze kuzalisha aina ya Tumbaku ambayo inakaushwa
kwa Jua kwa sababu Wilaya ya Gairo haina miti ambayo ni uoto wa asili hivyo
itakuwa ni kinyume cha utunzaji wa mazingira iwapo watalima aina ya tumbaku ya
kukaushwa kwa moshi. Alionyesha kufurahishwa na muitikio mkubwa wa wananchi na
uongozi wa wilaya kwa ujumla na namna walivyojipanga kuhakikisha kwamba lengo
lao linatimia. Gairo wameiandikia bodi ya Tumbaku Tanzania ili wawekewe
utaratibu kama wakulima wengine na waanze mara moja uzalishaji wa tumbaku aina
ya Balley inayokaushwa kwa jua”.
Alisisitiza utayari wa Taasisi ya TORITA katika
kuwasaidia wakulima wa Gairo ili walime kitaalamu na kuleta ufanisi kama ilivyo
katika mikoa mingine ya Tabora, Katavi na Kigoma.
Aidha, amesema kwakuwa mahitaji ya watu wanataka kulima zao hilo ni
makubwa Dkt. Jacob ametumia mwanya huo
kupitia SUAMEDIA kuwakumbusha wakulima kuacha Kilimo cha mazoea na badala yake
wajisajili bodi ya tumbaku na kupata namba za utambuzi ili ziwasaidie kupata
pembejeo na kupangiwa chama cha msingi husika ambacho watauzia tumbaku yao.
Mkurugenzi huyo amesema, pamoja na Zao la Tumbaku
kuonekana kuwa ni la Mkoa wa Tabora kwa sasa TORITA imesaidia kufanya tafiti za
maeneo mbalimbali yanayofaa kulimwa zao hilo nchi nzima na mpaka sasa Tumbaku
inalimwa katika Mikoa na wilaya mbalimbali zikiwemo wilaya ya Kasulu (Kigoma),
Kahama, Biharamulo, Chunya (Mbeya), Mpanda (Katavi) na maeneo mbalimbali ya
mikoa ya Mara, Iringa na Songea.
Ametanabaisha kwamba, pamoja na mikoa hiyo
kuongea uzalishaji wa Tumbaku, Mkoa wa Mara una maeneo mengi yanayolimwa na
yanayoandaliwa kuanza kilimo cha tumbaku hivyo umeombewa kwenye Bodi ya Tumbaku
kuwa Mkoa wa Kilimo hicho.
Mkulima
akiwa kwenye moja ya mashamba ya Tumbaku Mkoani Tabora.







No comments:
Post a Comment