RC SINGIDA: WATAKAO KWAMISHA MBOLEA KUWAFIKIA WAKULIMA TUTASHUGHULIKA NAO - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, December 6, 2023

RC SINGIDA: WATAKAO KWAMISHA MBOLEA KUWAFIKIA WAKULIMA TUTASHUGHULIKA NAO

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza katika kikao kazi cha kuhimiza kilimo kwa maafisa watendaji na maafisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kilichofanyika Disemba 4, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda na Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Augustino Matomora.

..............................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mbolea ya ruzuku na mbegu za alizeti kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hivyo hata kuwa tayari kumuona mtu akikwamisha mbolea hiyo kuwafikia wakulima na watakao thubutu kufanya hivyo watashughulika nao bila ya kuwaonea huruma.

Serukamba ameyasema hayo Disemba 4, 2023 wakati akizungumza na maafisa watendaji, maafisa ugani, wenyeviti wa vijiji wa Wilaya ya Iramba katika kikao kazi kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda chenye lengo la kuhamasisha kilimo.

“Naombeni watendaji wa kata, vijiji, maafisa kilimo, wagani nisiende kijiji chochote nikaambiwa moja ya kero yao hawajapata mbolea huo ugomvi utakuwa mkubwa sana,” alisema Serukamba.

Aliwataka maafisa hao kwenda kwenye maeneo yao wanayotoka kuitisha mkutano ya wananchi na kuwasajili majina yao ili waweze kupatiwa mbolea na kuwa maeneo yatakayokuwa hayana mbolea watendaji wake watashughulikiwa.

Aidha, alimtaka Afisa Kilimo wa wilaya hiyo kutoka ofisi kwenda kwa wakulima kuona kama mbolea imewafikia badala ya kufanya kazi hiyo kwa kutumia simu akiwa amekaa ofisini.

Serukamba alisema katika msimu huu wa kilimo wilaya hiyo imeanzisha mashamba mapya  ekari 3500 kwa ajili ya kilimo cha zao la alizeti.

Alisema lengo la mkoa ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo  kutoka asilimia 50 kwa msimu uliopita hadi kufikia asilimia 70 kwa msimu huu wa 2023/ 2024.

“Mkoa wa Singida ni wa tatu kutoka mwisho kwa uzalishaji wa mazao sasa tunapaswa kuongeza jitihada tutoke hapa tulipo tupande jambo ambalo linawezekana kwani Serikali imekwisha maliza kazi yake ya kutuletea mbolea ya ruzuku na mbegu ya alizeti ambayo kwa msimu huu itatolewa kwa kulipia fedha taslimu na si kwa mkopo,” alisema Serukamba.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda alimweleza Serukamba kwamba maagizo yake yote aliyotoa yatatekelezwa na akawataka watendaji wote kujipanga vilivyo kwani mapema wiki ijayo ataanza ziara katika kata zote ya kwenda kuona utekelezaji wa usambazaji wa mbolea.

“Suala hili leo sio mara ya kwanza kwani tulilipitisha katika kongamano letu la msimu wa kilimo tulilolifanya sasa mtatushangaza iwapo mtashindwa kulitekeleza,” alisema Mwenda.Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleimani Mwenda, akizungumza kwenye kikao hicho.Afisa Kilimo Wilaya ya Iramba, Malietha Kasongo, akizungumza kwenye kikao hicho.

Afisa Mtendaji Kata ya Shelui, Dickson Temael, akizungumza.
Afisa Mtendaji Kata ya Kiomboi, Gelege Kingu, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Afisa Mtendaji Kata ya Mtoa, Regina Kitundu, akielezea mipango ya kata hiyo kuhusu uzalishaji wa zao la alizeti.
Maafisa watendaji na maafisa ugani wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad