Vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) vikishushwa Ulanga mkoani Morogoro.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
SERIKALI kupitia Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya
Dar es Salaam imesambaza vifaa tiba vya zaidi ya sh. milioni 900 kwa ajili ya
vituo vya afya 23 vya halmshauri ya Wilaya ya Ulanga.
Akizungumza jana Wilayani humo mkoani Morogoro Mbunge wa jimbo la Ulanga Salim
Hasham, alisema, wamepokea vifaa tiba hivyo na dawa za zaidi ya sh. milioni 900
kwa ajili ya vituo vya afya 23 vya halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.
Alisema kishindo cha serikali ya Rais Dk.Samia
Suluhu Hassan sekta ya afya ni kikikubwa hivyo hatua ya kupokea vifaa tiba
hivyo vya kisasa ni muendelezo wa maboresho sekta ya afya ambapo Ulanga na mkoa
wa Morogoro kwa ujumla ni wanufaika.
“Huu ni utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama Cha
Mapinduzi ibara ya 83 sura ya 3 na kwa kiasi kikubwa Mwenyekiti wetu wa Chama
ambaye ndie Rais anatutendea haki sisi wanachama kwa kufanya zaidi ya matarajio
yetu, sekta ya afya ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya taifa hili.
“Tunaona mabadilika kwa bohari yetu ya dawa ni
makubwa sana kwa miaka mitatu ya hivi karibuni, hapa kwetu hospitali ya wilaya
ilikuwa na shida ya X Ray mashine kwa zaidi ya miaka minne lakini tumepata na
watu waliokuwa wakienda kupata huduma wilaya nyingine sasa hawahangaiki tena,”alisema.
Alisema, mbali na hatua hiyo wamepokea fedha sh.
milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya ambapo mazungumzo
yanaendelea ili waweze kupatiwa eneo lingine litakalokidhi mahitaji ya wilaya
hiyo ambayo kwa sasa ni makubwa yakihusisha wawekezaji na wafanyabiashara wa
madini ambao watapatiwa huduma.
Salim alisisitiza kuwa, wilaya hiyo ndani ya
miaka mitatu imepata vituo vya afya viwili na zahanati 10 na cha kushangaza
vipo vituo vya afya ambavyo havijamaliza ujenzi kikiwemo kituo cha afya cha
Ruaha lakini MSD imeshafikisha mahitaji yote muhimu vikiwemo vifaa tiba.
“Zamani vituo vya afya vilikuwa vinaisha na
tunakaa kusubiri vifaa tiba zaidi ya mwaka, lakini kwa sasa vifaa tiba
vinasubiri mmalize wafunge na wananchi wapate huduma kwa wakati mnyonge
mnyongeni haki yake mpeni, MSD mabadiliko ni makubwa sana MSD ya mama yetu Rais
Samia sio ile tuliyokuwa tunainyooshea vidole kila wakati,”alisisitiza.
Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie
Kaema alisema, MSD kwa niaba ya serikali wanaahidi kutomuangusha Rais katika
utekelezaji wa majukumu yake, hivyo upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa
tiba nchini utaendelea kuimarima zaidi
lengo ni kuboresha huduma za afya.
Alisema, ujio wa dawa na vifaa tiba hivyo vya zaidi ya sh. milioni 900 ni
muendelezo wa maboresho hayo.
“Julai hadi Novemba tumehakikisha dawa na vifaa
tiba vya sh. milioni 600 vinaletwa hapa na sasa tumekabidhi dawa na vifaa tiba
vya zaidi ya sh. milioni 300, hivyo vituo vya afya 23 vya Ulanga watapata
bidhaa za sh. milioni 900 ambazo zote zimekamilika na sasa vinasambazwa
vituoni.
“Tunaahidi chini ya serikali yetu na wizara ya
afya tutarajie mambo makubwa zaidi kwetu MSD Mkurugenzi wetu Mkuu Mavere Tukai
ametuagiza wote tunaosimamia hii mikoa kuwa mawakala wazuri katika kuokoa
maisha ya wananchi na maisha ya wananchi yanaokolewa kwa upatikanaji wa uhakika
wa dawa na vifaa tiba zikiwemo mashine hizi za kisasa za maabara ambazo
tumezishusha hapa leo (jana),
Alitaja baadhi ya vifaa tiba ambavyo wamepatiwa
wananchi wa Ulanga kuwa ni kiti cha huduma ya meno, vitanda vya huduma ya
uchunguzi, vitanda vya wodini vya wagonjwa, vifaa vya joto kwa ajili ya watoto
njiti, vifaa vya kusaidia upumuaji, vifaa vya oxygen, vitanda vya upasuaji na
Ultrasound mashine.
Vingine ni viti vya kubebea wagonja, vifaa vya
kutundikia maji tiba, pasi ya hospitali, stendi ya pazia za kuzibia wagonja,
mikebe ya vifaa vya kujifungulia,
matoroli ya kutolea dawa, vitanda vya kujingulia na vinginevyo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ulanga
Alli Ramadhan, alisema kwa sasa hali ya huduma za afya wilayani humo imekuwa na
maboresho makubwa kuanzia watumishi, dawa na vifaa tiba.
“Hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni asilimia 95 hadi 97 tofauti na awali ilikuwa ni asilimia 70 hadi 80, hali hii imepunguza sana malalamiko ya wananchi na kuwa na imani na watumishi wetu naomba niipongeze sana MSD maboresho ni makubwa kuanzia huduma kwa sisi wateja wao na kupata zile dawa na vifaa ambavyo tulikuwa tunachukua kwa mshitiri na uletaji wa dawa na vifaa kwa wakati mkiagiza hakuna longolongo mnaletewa hii inatuma ari hata sisi katika utendaji wetu,”alisema.











No comments:
Post a Comment