TAMUFO YAWAKUMBUKA WANAMUZIKI KING KIKII, ZAHIR ZORRO WANAO SUMBULIWA NA MARADHI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, December 1, 2023

TAMUFO YAWAKUMBUKA WANAMUZIKI KING KIKII, ZAHIR ZORRO WANAO SUMBULIWA NA MARADHI

Katibu Mkuu wa Umoja wa  Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Stella Joel na viongozi wengine wa umoja huo wakimuombea Mwanamuziki Mkongwe  Zahir Ally Zorro walipomtembelea hivi karibuni nyumbani kwake Kigamboni jijini Dar es Salaam kumjulia hali kutokana na maradhi yanayomsumbua. 

Na Kulwa Mwaibale

 

UMOJA wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) umewakumbuka kwa kuwapa fedha wakongwe wa muziki wa dansi nchini,  Zahir Ally Zorro na Boniface Kikumbi Mwanza Mpango  'King Kikii' wanaopitia changamoto za maradhi ili ziwasaidie kwa chochote.

Tukio hilo lilijiri Novemba 25, 2023 ambapo viongozi wa TAMUFO, Stella Joel ambaye ni Katibu, Pastor Lucy Wilson wa Kanisa la Spring of Life Mision la Tabata ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Gospo TAMUFO na Frank Richard, Mlezi wa TAMUFO walifika kumjulia hali King Kikii nyumbani kwake Mtoni Kwa Aziz Ally Temeke.

Stella akizungumza na mgonjwa huyo ambaye afya yake bado haijaimarika baada ya kufanyiwa upasuaji hivi karibuni kabla ya kwenda Kigamboni nyumbani kwa Zahir Zorro, alisema waliamua kuwafariji wanamuziki hao kwa sababu ya mchango walioutoa katika Taifa letu kupitia tasnia ya muziki.

"King Kikii mzee wa kitambaa cheupe na Zahir Ally Zorro, kupitia muziki wamelifanyia makubwa taifa letu, kuelimisha na kuburudisha, tungo zao zinaujumbe utakaoishi milele," alisema Stella.

Aliongeza kuwa, wanamuziki hao ni wenzao tangu TAMUFO ilipoasisiwa ambapo King Kikii ni mmoja wa viongozi wake.

Alisema kuwa wakiwa Arusha walisikia kuhusu changamoto za maradhi yanayowasibu wanamuziki.hao walioshirikiananao.kwenye mikutano, matamasha sehemu mbalimbali, walipofika Dar es Salaam wameona vyema kufika kuwapa pole.

Pastor Lucy aliyeongoza maombi ili Mungu awajalie afya njema wanamuziki hao, alisema ni mpenzi wa nyimbo za wanamuziki hao tangu zamani kwa sababu zinaelimisha na kuburudisha na baadhi zinaonesha walivyo wazalendo wa nchi yao ya Tanzania..

"Wakongwe hawa wa muziki wamelifanyia mengi taifa letu kupitia muziki, nyimbo ya fungua njia kitoto chaanzatambaa, Kitambaa Cheupe, Cleopatra na Wazazi ya Zahir Zorro aliyoitunga baada ya vita vya Tanzania na Uganda vilipoisha na zingine nazipenda sana," alisema Pastor Lucy.

Aliongeza kwa maombi ambayo waliyafanya Mungu atawaponya wanamuziki hao.

Akizungumza nyumbani kwa Zorro, Dkt. Frank  Richard alisema TAMUFO itakuwa sambamba na wanamuziki hao katika kipindi chote cha udhaifu wa afya zao hadi watakapopona na kurejea kwenye shughuli zao za muziki na zingine.

"Kwa kuwathamini kama wenzetu na mchango wenu mkubwa mlioutoa katika nchi yetu kupitia muziki, sisi TAMUFO tutakuwa nanyi kwenye kipindi cha changamoto ya maradhi mnachopitia," alisema mlezi huyo wa TAMUFO.

King KikiI aliwashukuru viongozi hao kwa kufika kumjulia hali na kumpa fedha alizosema zitamsaidia katika kipindi cha maradhi anachopitia.

Aliwashukuru watanzania akiwemo Waziri Mkuu Kasim Majaliwa waliomsaidia baada ya kuguswa na changamoto ya maradhi yake, amewaomba waendelee kumsaidia kwani anahitaji fedha ili akatibiwe nje ya nchi.

Kwa upande wake Zahir Zorro, ameishukuru TAMUFO Kwa upendo wao wa kwenda kumjulia hali, pia amemshukuru Mkurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Ayub Ryoba kumkatia Bima ya afya inayomsaidia kupata matibabu.

Amesema kwa sasa anaendelea vizuri isipokuwa mwili.hauna nguvu.

Aliongeza kuwa alianza kuugua muda mfupi baada ya kifo cha binti yake Maunda na kufikia kuwa na hali mbaya.

Ameishukuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu kwa yote inayoyafanya kwa wasanii.na taifa kwa jumla.

Wanamuziki hao wanatarajia kufyatua vibao vya Gospo kumshukuru Mungu aliyesimamanao kwenye kipindi kigumu cha kuugua kwao, TAMUFO imeahidi kushirikiananao kurekodi nyimbo hizo.Viongozi hao wa TAMUFO wakimuombea mwanamuziki,  Boniface Kikumbi Mwanza Mpango  'King Kikii' walipokwenda kumjulia hali nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ally kutokana na maradhi yanayomsumbua.Mwanamuziki Mkongwe  Zahir Ally Zorro akizungumza na viongozi hao wa TAMUFO (hawapo pichani) walipo mtembelea kumjulia hali.

Maombi yakiendelea kufanyika.
Viongozi hao wa TAMUFO wakimfanyia maombi, Mwanamuziki Mkongwe  Zahir Ally Zorro .

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad