KAMPENI YA HUDUMA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA YATUA SINGIDA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 10 January 2024

KAMPENI YA HUDUMA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA YATUA SINGIDA

Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria (katikati)  ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign), akiserebuka pamoja na wadau wa sekta ya Sheria wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Januari 10, 2024 mkoani Singida. Kulia aliye nyosha mkono juu ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali.
..................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

KAMPENI ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) imezinduliwa rasmi mkoani Singida na  imelenga kuzifikia Kata 70 na vijiji 210 ambapo umetolewa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na maeneo jirani kuitumia vizuri fursa hiyo kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu  kupata elimu na huduma za masuala mbalimbali ya kisheria  zitakazotolewa bure. 

Wito huo umetolewa na Balozi Dkt. Pindi Chana,  Waziri wa Katiba na Sheria ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Januari 10, 2024 Stendi ya Mabasi ya Zamani mkoani hapa. 

Balozi Chana alisema utekelezaji wa kampeni hiyo umekuwa na mafanikio makubwa hadi kufikia Oktoba, 2023 tangu ilipoanza rasmi mwezi Aprili, 2023. 

Alisema hadi kufikia Oktoba 30, 2023, Mama Samia Legal Aid Campaign imeifikia mikoa mitano ya  Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma  na Simiyu ambapo jumla ya Halmashauri 35, Kata 397 na Vijiji/ Mitaa 1,046 imefikiwa na utekelezaji wa kampeni hiyo katika mikoa hiyo na  jumla ya wananchi 362,488 (Wanaume 179,874  wananwake 182,615 ) wamefikiwa kupitia elimu ya kisheria na huduma nyingine za kisheria. 

Balozi Chana alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia bado ni changamoto katika jamii zetu na kuwa wanawake na watoto wameendelea kuwa wahanga wa vitendo hivyo na kuwa hiyo  inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya maeneo bado yanaendelea kusimamia mila na desturi potofu zilizopitwa na wakati. 

"Tunaendelea kuchukua hatua mkononi na kutokusheshimu sheria zilizopo na katika hili niwakumbushe wajibu wa kutoa taarifa juu ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na uvunjifu wa sheria na hapa nisisitize vyombo vyetu vya utoaji haki tusimamie haki na kuhakikisha  inatendeka kwa wakati kwa washukiwa wote wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua stahiki," alisema Balozi Chana. 

Chana aliliomba Jeshi la Polisi lisaidie kuchunguza na kupeleleza kwa kina ili kukomesha mnyonyoro wote wa wahalifu katika masuala ya ukatili wa kijinsia na kuwa Serikali itaendelea kusimamia misingi ya sheria na kufanya maboresho ya sheria zetu ili kuendana na mazingira ya sasa hususani kwenye maendeleo ya teknolojia. 

Alisema kampeni hiyo inashiriki katika utatuzi wa migogoro kwenye  ngazi za kijamii ambapo jumla ya  migogoro 6,365 iliyohusu  masuala ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya watoto ilipokelewa kati ya hiyo migogoro  488 ilitatuliwa na kuhitimishwa ndani ya kipindi cha kampeni huku migogoro 5,877 ikiendelea kushughulikiwa na mamlaka  mbalimbali za kimahakama,kiutawala na wizara kupitia waratibu na wasajili wa mikoa na wilaya imeendelea kufuatilia utekelezaji wake. 

Balozi Chana alisema kampeni hiyo inawezesha pia huduma za usajili wa matukio mbalimbali ikiwemo usajli wa vyeti wa kuzaliwa na vifo kupitia Ofisi ya Kabidhi Mkuu RITA na kuwa jumla  ya wananchi 2,055 (Wanaume1,035 Wanawake 1,020) walisajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia ofisi hiyo kwenye mikoa hiyo  mitano. 

Alisema kwa upande wa maeneo ya vizuizi, kampeni hiyo iliweza kuvifikia Vituo vya Polisi 22 na Magereza 17 yametembelewa na huduma kutolewa ambapo jumla ya Wafungwa na Mahabusu 4,763 walipatiwa elimu na huduma mbalimbali za kisheria. 

Waziri Chana aliwapongeza na kutoa wito kwa viongozi wote wa dini hapa nchini kwa nyakati tofauti tofauti wamekuwa  wakikemea vitendo vya uvunjifu wa sheria, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii hususan ukatili uliokithiri dhidi ya wanawake na watoto na amewathibitishia kuwa  Wizara ya Katiba na Sheria iko tayari kushirikiana nao kwa namna yoyote ambayo itafaa katika kampeni hiyo hata kama itahusisha kutumia majukwaa yao kutoa elimu kwa umma juu ya haki na wajibu  wa Kikatiba na Kisheria. 

Aidha, Balozi Chana alivikumbusha vyombo vya habari na    wanahabari kuwa  jukumu kubwa na muhimu katika kampeni hiyo kuwaomba kujipanga vyema kama sekta ili kushirikiana katika  kutekeleza suala hilo muhimu kwa mustakabali wa heshima ya nchi na wananchi na wahakikishe wanapata elimu kwa wakati na kusaidia  kuibua changamoto zao mbalimbali na kufuatilia ufumbuzi wake hadi mwisho. 

Pia Balozi Chana alitoa wito kwa wanasiasa kujitahidi kutumia uzoefu na weledi wao katika kumuunga mkono Rais Samia na Mtetezi wa Wananchi  kuondoa kadhia ya ukatili  wa kijinsia na uvunjifu  wa haki za binadamu kwenye jamii kutokana na kutambua mchango mkubwa anautoa. 

Dkt. Chana alizishukuru asasi za kiraia kwa mchango wao  mkubwa  wanaoendelea kuutoa katika nyanja mbalimbali  kwa  watanzania na kwamba Serikali  inatambua mchango wao na itaendelea kuunga jitihada zao na kuwa wanaamini kampeni hiyo itaongeza nguvu za jitihada hizo. 

Akizungumzia Jeshi la Polisi, Dkt. Chana alilitaka kuchochea upatikanaji wa haki na kwa wakati ambapo alitoa wito kwa Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Singida,  kushughulikia kesi zote za ndoa, mimba za utotoni na ubakaji ambazo zimekaa muda mrefu katika upepelezi bila kushughulikiwa kwa kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na wanashughulikiwa ili kuondoka changamoto ya kutoroka kwa watuhumiwa pindi wanapopewa dhamana ama wanaposikia wanatafutwa na jeshi hilo. 

Aidha, Waziri Pindi Chana alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kuweka mipango endelevu ya upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi katika ngazi za kijamii uendelevu wa huduma hiyo na kuwa ndio utakamilisha adhima ya malengo ya kampeni hiyo. 

Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Pindi Chana kwa namna ya pekee alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyoiongoza nchi kwa kuzingatia katiba, sheria na taratibu tulizojiwekea kama nchi na kuwa kila mtanzania analo jukumu la kusimamia na kuzingatia  haki za binadamu, utawala wa sheria, utii wa sheria na elimu ya kikatiba na ya kisheria kwa umma. 

Balozi Chana aliwasihi viongozi kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu watakapokuwa katika maeneo yao na wahamasishe wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alisema tangu kuzinduliwa kwa kampeni hiyo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Machi 27, 2023 wana Singida walianza rasmi mkakati wa kuipokea kwani huduma za msaada wa kisheria inahitajika sana na ni muhimu kwa wananchi.

"Kupitia dawati la malalamiko tumekuwa tukipokea na kushughulikia malalamiko mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi,mirathi, ukatili wa kijinsia na wananchi waliokuwa na changamoto za kisheria tumeweza kuwaunganisha na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya kisheria," alisema Serukamba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa akizungumza kwenye uzinduzi huo aliwaomba wananchi wa Singida kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazo wabaini wahalifu jambo litakalo saidia kuufanya mkoa huo kuwa wa utulivu na amani hivyo kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza.

Naye Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima ambaye alikuwa ni Mbunge mwenyeji wa uzinduzi huo alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo itamfanya kila mtanzania kuijua haki yake na kuweza kuisimamia na kuhakikisha kwamba uwajibikaji ndani ya Serikali na kwenye jamii unaongezeka.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Utawala  Sheria na Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, Yahaya Masare alisema uzinduzi wa kampeni hiyo unatoa faraja kubwa kwa kamati hiyo kufuatia baadhi ya watuhumiwa waliofungwa kwa  makosa mbalimbali kuachiwa huru kupitia msaada huo wa kisheria baada ya kubaini hawakutenda makosa yaliyowatia hatiani.

Akitoa salamu kwa niaba ya mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria mkoani Singida, Mkurugenzi wa Shirika la Msaada wa Kisheria Singida, Paschal Tantau alisema wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa sheria wameipokea kampeni hiyo yenye kauli mbiu isemayo " Msaada wa Kisheria kwa Haki, Amani, Usawa na Maendeleo"

Alisema kampeni hiyo inawafikia walengwa wa msaada wa sheria ambao kwa namna moja au nyingine kutokana na hali zao za kiuchumi kwa muda mrefu hawakupata fursa ya kusikilizwa kwa karibu changamoto zao za kisheria zinazowakabili.

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA

(Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC ) imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hususan katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala, na masuala yahusuyo haki za binadamu kwa ujumla.

MSLAC ni mchakato wa kupata ushauri au msaada kutoka kwa wataalamu wa sheria ili kutatua masuala ya kisheria au kupata ufafanuzi kuhusu haki na wajibu wa mtu. Kampeni Hii inajumuisha mambo kama vile ushauri wa kisheria, msaada wa kisheria au uwakilishi wa kisheria katika mahakama.

"Usaidizi wa Kisheria" au "Msaada wa Kisheria" unaweza kutofautiana kidogo kulingana na muktadha wa kisheria wa nchi fulani. 

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia #MSLAC inatoa msaada wa kisheria kwa watu ambao hawawezi kumudu huduma za kisheria kikamilifu au wanaohitaji msaada wa kisheria. 

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia #MSLAC imejikita kutoa msaada wa kisheria ambao unaweza kujumuisha yafuatayo hapo chini:- 

MSLAC inatoa Ushauri wa Kisheria kwa watu wanaohitaji msaada na mwongozo katika masuala mbalimbali ya kisheria, kama vile masuala ya familia, makazi, au ajira. 

MSLAC Kuwapatia watu wasiojiweza rasilimali za kutosha ili kupata huduma za kisheria au kuwawakilisha mashauri yao mahakamani. 

MSLAC inakuwakilisha Mahakamani kwa Kutoa msaada wa kisheria kwa watu ambao wanaweza kuhitaji wakili kuwawakilisha katika masuala ya kisheria mahakamani. 

MSLAC  inatoa elimu na ufahamu kuhusu haki za kisheria na jinsi ya kuzitumia. 

MSLAC inasimamia usuluhishi wa migogoro, kwa kusaidia katika kutatua migogoro nje ya mahakama kupitia njia za usuluhishi au mazungumzo.Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, akihutubia kwenye uzinduzi huo.Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, akiwasalimia wadau wa sekta ya sheria na wananchi mara baada ya kuwasili kwenye uzinduzi huo.

Viongozi wa dini Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kati (Singida),, Dkt. Sprilian Hilinti (kushoto) na Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro (katikati) na Mbunge wa Singida mjini, Mussa Sima wakimsubiri  kumpokea Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria.

Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, akifurahi na wadau wa sekta ya sheria alipokuwa ametembelea banda la Wizara hiyo wakati wa uzinduzi huo.Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro na Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria (kulia) wakifurahi baada ya Waziri huyo alipokuwa amewasili kuzindua kampeni hiyo.Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Wakili Neema Ahmed (kushoto) akitoa maelezo kwa Balozi Dkt. Pindi Chana ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria (kulia) alipotembelea banda la chama hicho kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo.Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza kwenye uzinduzi huo.Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt.Fatma Mganga, akichangia jambo kwenye uzinduzi huo.Viongozi meza kuu wakishiriki kuimba wimbo wa TaifaSheikh Mkoa wa Singida,akiomba dua kabla ya kuanza kwa uzinduzi huo.
    Makatibu Tawala wa Wilaya wakiwa kwenye uzinduzi huo. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Rashid Rashid,   Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Warda Abdallah Obathany  na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama, Peter Masindi.  Askari wa Jeshi la Polisi wakipiga saluti kuonesha heshima wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa.Wimbo wa Taifa ukiimbwa.Wanakwaya wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mkoa wa Singida wakitoa burudani wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.

    PICHA  ZOTE  NA  SOLOMON  PHILEMON
........................
----ANGALIA  VIDEO  CHINI---

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad