Wanawake Wajasiriamali wa Wilaya ya Iramba ambao wanajishughulisha na Mama Lishe wakiwa wamebeba mitungi ya gas yenye majiko baada ya kukabidhiwa Januari 6, 2024. Mitungi hiyo imetolewa na Kampuni ya Oryx Tanzania kupitia Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi Dkt. Mwigulu Nchemba ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
.....................................................
Na Dotto Mwaibale, Iramba
JITIHADA za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutunza mazingira zimeendelea
kuungwa mkono na wadau mbalimbali ambapo Kampuni ya Gas ya Oryx Tanzania
kupitia Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni
Waziri wa Fedha kutoa mitungi ya gas yenye majiko yake kwa Mama lishe na Baba
lishe zaidi ya 700 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumza katika hafla ya
makabidhiano ya mitungi hiyo iliyofanyika Januari 6, 2024 ukumbi wa mikutano wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa
niaba ya Dkt. Nchemba alisema mitungi hiyo imetolewa na mbunge huyo kwa ajili
ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia za utunzaji wa mazingira kazi ambayo
aliianza tangu alipokuwa makamu wa Rais.
"Mhe. Mbunge alituita Dodoma mimi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya Innocent Msengi na kutueleza kuwa amefanya mazungumzo na viongozi wa
Kampuni ya Oryx gas Tanzania ambao watatusaidia kutupatia mitungi ya gas lengo
kuu likiwa ni kuziunga mkono juhudi za Rais Samia alizozianza tangu akiwa
Makamu wa Rais za kulinda na kutunza
mazingira," alisema Mwenda.
Alisema kulingana na kumbukumbu za wanamazingira hapa nchini zinaonesha
kuwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokea unatokana na ukataji wa miti
mikubwa inayohitajika kwa ajili ya nishati ya kupikia (kuni)
Alisema takwimu hizo zinatishia na kuonesha wazi kuwa tukiendelea na utaratibu huo wa ukataji miti kwa ajili ya
nishati hiyo ya kupikia ifikapo miaka 10 hadi 20 ijayo nchi yetu itabadilika na
kuwa jangwa.
Mwenda alisema kutokana na hali hiyo Dkt.Nchemba ameziiunga mkono juhudi
hizo za Rais na kuwataka kupande miti ya kutosha kwa ajili ya kulinda tabia
nchi na ndio sababu iliyomfanya azungumze na viongozi wa Kampuni ya Oryx
Tanzania ambao walikubali kumpa mitungi ya gas 700 na wao wakatoa mingine 200
na kufanya jumla ya mitungi kuwa 900 ambayo itatumiwa na wananchi wa wilaya
hiyo badala ya kutumia mkaa na kuni kwani nao wameguswa na athari za uharibifu
wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Oryx Tanzania, Benoit Araman
alisema kuanzia mwezi Julai, 2021 kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele
kutekeleza maelekezo ya Serikali waliyoyapokea kutoka kwa Rais kuwa ifikapo
mwaka 2023 wananchi wote wa Tanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Alisema kupitia mipango hiyo Oryx imepanga kutokomeza kabisa matumizi ya
nishati ya kuni na mkaa ambayo si mbaya kwa afya za watu bali pia ni hatari kwa
uharibifu wa mazingira.
Mkurugenzi huyo mkazi wa kampuni ya Oryx Tanzania alisema wanajipongeza kwa
kuwa kinara wa usambazaji wa gas ya APG kwa watanzania na kuwa wataendeea zaidi
kuwekeza, kuratibu, kueneza nishati safi
kwa kutumika gas hiyo kwa manufaa ya wote.
Baadhi ya wananchi waliopata mitungi hiyo ya gas wakiwemo viongozi wa dini
waliipongeza kampuni ya Oryx kwa kutoa mitungi hiyo ambayo itasaidia kutunza
mazingira na kuacha kabisa matumizi ya nishati ya kuni na mkaa.
Askofu Robert Lugiko wa Kanisa la
Baptisti Tanzania Jimbo la Singida, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini,
alimshukuru Rais Samia na kampuni hiyo kwa kutoa mitungi hiyo ya gas na kuwa
matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakiwaathiri sana wanawake na kueleza kuwa
kuanzia sasa anakwenda kuwa balozi wa kuhimiza matumizi ya nishati ya gas kwa
ajili ya utunzaji wa mazingira.
Katika makabidhiano ya mitungi hiyo ya gas na majiko yake maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida, Konstebo Rahma Abdarabi, Konstebo John Mduma wakiongozwa na Mkaguzi wa jeshi hilo mkoani hapa, Mwantumu Bakari walipata fursa ya kutoa elimu ya namna bora ya kukabiliana na majanga ya moto ambao unaweza kutokea wakati wa matumizi ya majiko hayo.









No comments:
Post a Comment