TANESCO SINGIDA YATOA SEMINA KWA WADAU WA NISHATI YA UMEME MANISPAA SINGIDA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 8 January 2024

TANESCO SINGIDA YATOA SEMINA KWA WADAU WA NISHATI YA UMEME MANISPAA SINGIDA

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally, akizungumza na madiwani na baadhi ya wakuu wa taasisi zilizo chini ya Serikali zilizopo Manispaa ya Singida (hawapo pichani) wakati wa semina ya wadau wa nishati ya umeme iliyoandaliwa na shirika hilo Januari 8, 2024.
.................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MADIWANI wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida wamelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida kwa huduma nzuri linazozitoa na kulitaka linapotekeleza miradi yake liwe linawashirikisha madiwani wa maeneo husika ili kutambua vijiji na vitongoji vyenye uhitaji wa huduma ya nishati ya umeme.

Mapendekezo hayo yametolewa na madiwani hao kwenye kikao cha wadau wa nishati ya umeme Mkoa wa Singida kilichoandaliwa na shirika hilo na kuwashirikisha baadhi ya wakuu wa taasisi zilizo chini ya Serikali chenye lengo la kutangaza huduma zinazotolewa pamoja na kupokea maoni na changamoto mbalimbali.

Madiwani hao walisema Tanesco ikiweka utaratibu wa kuwashirikisha wawakilishi hao kutaondoa malalamiko ya  wananchi ambao baadhi ya vijiji vyao bado havijafikishiwa  huduma ya umeme.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa madiwani kwenye miradi hiyo Diwani wa Kata ya Kisaki, Moses Ikaku alitoa mfano wa Kitongoji cha Ilahu kuwa na umeme lakini Tanesco wakakitaja kitongoji cha Ikenda kuwa ndicho chenye umeme badala ya Ilahu jambo ambalo linaweza kuwaletea wananchi usumbufu.

Kwa upande wao Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Sh.Bilioni 3.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme katika Mkoa wa Singida ambapo pia walilishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida kwa ushirikiano mkubwa wanao utoa kwa CCM na Serikali na kuliomba kuzitendea haki fedha hizo kwa kufanya kazi iliyokusudiwa na Serikali.

Hata hivyo viongozi hao waliziomba taasisi za umma mkoani hapa kushirikiana wakati wa utekelezaji wa miradi yao ili kuepusha migongano kama Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuilalamikia Tanesco kuwa wameweka nguzo zao kwenye hifadhi ya barabara au Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira singida (SUWASA) wamepitisha mabomba ya maji kwenye miundombinu ya umeme.

“Nimemsikia hapa mmoja wa kiongozi wa taasisi ya umma akilalamika dhidi ya Tanesco. Tanroads ni taasisi, Tarura ni taasisi, Suwasa na Ruwasa zote ni taasisi za umma naombeni mkae pamoja muweze kuunganisha mambo yenu kwani ninyi mkianza kulalamika, diwani analalamika, mkuu wa taasisi analalamika, watu wote tunalalamika hiyo sio sawa,” alisema Mwiru.

Mwiru alisema ni vizuri taasisi hizo zote zikakaa kwenye vikao vyao kwa pamoja kujadili wakati wa utekelezaji wa miradi kwa kuwa kazi zao sinashabihana kwa namna moja au nyingine hivyo aliwaomba kulifanyia kazi jambo hilo.

Naye Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu alizitaka taasisi zote za Serikali mkoani Singida kuwa na mahusiano na mawasiliano na kueleza kuwa haiwezekani kwenda holelaholela tu huku wakilalamika nguzo ya umeme sijui imekaa wapi, bomba langu limekatwa.

Kiaratu alisema wamekuwa wakikutana na changamoto hizo wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuwa Manispaa ya Singida katika mpango wao kabambe wa kupanga mji walizishirikisha taasisi zote na kukubaliana lakini anashangaa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo wanakwenda tofauti.

Alisema taasisi moja inapokuwa na mradi ni vizuri kabla ya kuuanza itoe taarifa kwa taasisi zingine ili kuondoa kadhia hiyo ambayo mara nyingi husababisha miundombinu iliyopo kubomolewa na kuisababishia hasara Serikali.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally alisema wamezipokea changamoto za madiwani hao na kuwa zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma sahihi, bora na kwa wakati.

Alisema kwa kutoa semina hiyo kwa madiwani hao anaamini kupitia wao wananchi wote wa Manispaa ya Singida watafikiwa na elimu hiyo.

Aidha, Ally alisema ili kukabiliana na ukatikaji umeme wa mara kwa mara shirika hilo linafanya maboresho kwa kubadilisha nguzo zilizooza na vikombe.

Mbunge wa Jimbo la Singida mjini, Musa Sima amempongeza Meneja wa shirika hilo mkoani hapa Mhandisi Mwamvita Ally kwa kuja na mbinu mpya ya kutoa semina kwa madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida na kujitambulisha baada ya kuhamia Singida akitokea Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

“Ndugu zangu madiwani wote tunakubaliana inawezekana ni mara ya kwanza kuona taasisi bila kushinikizwa kiongozi wake anakuja na kuona ili aweze kujitambulisha hana sababu ya kwenda kwenye baraza la madiwani na kusema mimi ni Meneja wa Tanesco akatengeneza programu ya kujitambusha kwa kuandaa semina. Hakika semina hii imetupa ufahamu mkubwa na kwa pamoja tunashiriki kwenye suala ili kubwa la maendeleo kwa kweli ni jambo jema sana naamini na taasisi zingine zitajifunza kupitia Tanesco,” alisema Sima.

Afisa Uhusiano na huduma kwa wateja wa shirika hilo, Mkoa wa Singida Rehema Mwaipopo, akielezea utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Singida  alisema shirika hilo kwa sasa inasimamia miradi miwili ya maendeleo ambao ni mradi wa Peri Urban III na mradi wa Kusambaza Umeme Maeneo Ya Madini, Viwanda Vidogovidogo na Kilimo cha Umwagiliaji unaofadhiliwa na serikali kupitia REA kwenye jimbo la Singida mjini ambayo ina thamani ya Sh. Bilioni 7.7 ambao upo kwenye hatua za utekelezaji.t

Alisema mradi huo wa kupeleka umeme katika maeneo, vitongoji na mitaa iliyopo pembezoni mwa miji (Vijiji-Miji) yaani peri urban ambayo yanauhitaji mkubwa wa umeme lakini pia hali ya maeneo hayo inashabihiana na maeneo ya vijijini.

Alisema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi M/S Central Electricals International Ltd katika Lot 6  vijiji 13 vyenye jumla ya vitongoji 34 ndani ya jimbo la Singida mjini na kuwa mkataba unategemewa kukamilika  Julai 19, 2024 na unathamani ya zaidi ya Sh. Bilioni 7.1 na kuwa mpaka kufikia Januari 7, 2024 wamefanikiwa kuwasha vitongoji 10 kati ya 34 ambapo ni sawa na asilimia 29.4

Wataalam wa Tanesco wakiwa na Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally (kulia) wakiandika maoni ya madiwani wakati wa kikao hicho.
Afisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Singida, Mhandisi Nyerere Ernesti, akitoa mada inayohusu usalama usalama.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo akitoa mada kwenye semina hiyo.
Washiriki wakiwa kwenye semina hiyo.
Mkurugenzi wa Usambaji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira singida (SUWASA) Mkoa wa Singida Mhandisi Lunango Muwelu, akichangia jambo kwenye semina hiyo.
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida, Malisiana Chakutema, akizungumza katika semina hiyo.
Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima, akichangia jambo kwenye semina hiyo.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye semina hiyo.
Diwani wa Kata ya Isuna, Hamisi Kisuke akisisitiza jambo kwenye semina hiyo
Washiriki wa semina hiyo wakiwa katika picha ya pamoja.

( PICHA  ZOTE NA  SOLOMON PHILEMON )
---------------------------------------------
-----ANGALIA  VIDEO  CHINI------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad