TANESCO SINGIDA YAENDELEZA MKAKATI MABORESHO MIUNDOMBINU NJIA YA UMEME MANYONI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 1 January 2024

TANESCO SINGIDA YAENDELEZA MKAKATI MABORESHO MIUNDOMBINU NJIA YA UMEME MANYONI

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)  Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally (wa pili kulia),  akiwa na Wahandisi wa shirika hilo wa  Wilaya ya Manyoni wakati wakikagua moja ya transfoma katika ukaguzi wa miundombinu ya njia ya umeme Manyoni. Kulia ni Afisa Uhusiano Huduma kwa Wateja, wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo.

...............................................................

Na Dotto Mwaibale, Manyoni

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida katika kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme ambako linatokana na uchakavu wa miundombinu  limeendelea na kazi ya kuboresha miundombinu katika wilaya zenye changamoto hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika..

Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally akizungumza na waandishi wa habari Disemba 30, 2023 wakati wa ukaguzi wa maboresho hayo alisema yanahusisha Wilaya za Ikungi, Manyoni na Itigi ambazo zinazopitiwa na njia ya umeme Manyoni.

Ally alisema hatua ya shirika hilo kuanza maboresho hayo ilitokana na maombi kutoka kwa wateja wao wanaohudumiwa na njia hiyo ambao walielezea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

“Baada ya kupokea maombi hayo timu ya wataalamu ya Tanesco mkoa kwa kushirikiana na wenzetu kutoka makao makuu tulipita kwenye njia hii ya umeme na kufanya ukaguzi na kugundua changamoto kadhaa zinazosababisha umeme kukatika,” alisema Ally.

Alisema kutokana na changamoto hizo shirika hilo lilijiwekea mkakati wa muda mfupi wa kuitatua ambao unajumuisha kubadilisha vifaa chakavu ambavyo vimeharibika kwenye njia hiyo kama vikombe ambapo tangu waanze kazi hiyo wiki mbili zilizopita tayari wamebadilisha vikombe 3000.

Alisema sambamba na ubadilishaji wa vifaa hivyo pia wanabadilisha nguzo zilizooza na kuwa wanaimani baada ya matengenezo hayo changamoto hiyo itamalizika.

Meneja huyo aliongeza kuwa wanafanya kazi hiyo ikiwa ni kutekeleza lengo la shirika hilo pia ni agizo la Serikali la kuhakikisha wanawapatia wananchi huduma iliyo bora.

Aidha, Ally alisema pamoja na kuifanyia kazi changamoto hiyo ipo nyingine kubwa ya uharibifu wa miundombinu ambayo inafanywa na wananchi katika shughuli zao za kibinadamu wakati wakisafisha mashamba yao ambayo yapo kwenye njia ya umeme na kusababisha kuchoma nguzo na kusababisha hasara kwa shirika hilo.

Meneja huyo alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kuilinda miundombinu ya shirika hilo kwani jukumu hilo ni la kila mtu na si shirika hilo peke yake.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni, Jumanne Mkhandi aliishukuru Serikali kupitia shirika hilo kwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakikika kutokana na maboresho hayo yanayoendelea kufanyika kwenye njia hiyo ya umeme.

Ismail alisema mahitaji ya umeme katika wilaya hiyo na nyingine zote ambazo zipo kwenye njia hiyo ni makubwa mno kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi na viwanda kutegemea nishati ya umeme hivyo unapokosekana inakuwa ni changamoto kwao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Dkt. Pius Chaya naye alianza kwa kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anazozifanya katika jimbo hilo kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya umeme.

Alisema changamoto kubwa iliyopo kwenye jimbo hilo ni ya kukatika umeme na kuwa kituo cha kupozea umeme wanacho kitegemea ni cha Singida mjini ambapo umeme ukipozwa huko ndio urudi tena Manyoni na kuwa unatembea takribani kilometa 150.

Dkt.Chaya alisema kutokana na hali hiyo iwapo kutatokea  changamoto yoyote kwenye njia hiyo basi wilaya ya Manyoni inakosa umeme.

Mbunge Chaya alisema changamoto hiyo inakwenda kumalizika baada ya kumueleza Rais na kumuomba ambapo ametoa Sh.Bilioni 30 kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme katika wilaya hiyo kazi itakayoanza  mwaka huu wa 2024.

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Manyoni, Manoni Nilla ambaye ni kinyozi katika saluni  na Caleb Stanley ambaye anaendesha kiwanda kidogo cha kusindika nafaka wameipongeza Serikali kupitia Tanesco kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu cha kukatika kwa umeme mara kwa mara na kusababisha kuzorotesha shughuli zao.

“ Tume yaona maboresho ya miundombinu ya njia ya umeme Manyoni yanayoendelea kufanywa na ndugu zetu wa Tanesco kwa wiki mbili sasa hakika ni kazi nzuri tunaamini yanakwenda kumaliza changamoto iliyokuwepo ya kukatika kwa umeme,” alisema Stanley.


Fundi wa shirika hilo akiwajibika ipasavyo ikiwa ni maboresho ya miundombinu hiyo.
Kazi ya maboresho ya njia hiyo ya umeme Manyoni ikiendelea.
Kazi ikiendelea.
Mafundi wa shirika hilo wakiendelea na maboresho ya miundombinu hiyo eneo la Ulyampiti wilayani Ikungi.
Muonekano wa nguzo za umeme baada ya kufanyiwa maboresho kwenye njia hiyo.
Gari la shirika hilo likisambaza nguzo kwenye maeneo ya maboresho.
Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Dkt. Pius Chaya, akizungumzia maboresho yanayofanywa na shirika hilo kupitia Serikali.
Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Mhandisi Mwamvita Ally akizungumzia maboresho hayo. 
.............................
ANGALIA  VIDEO  CHINI
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad