Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdarahman, akishiriki kufanya usafi katika soko la Makorora wakati wa ziara yake ya kuyakagua masoko hayo na kusikiliza kero za wafanyabiashara. Ziara hiyo ameifanya Februari 25, 2024.
................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa
Tanga, Rajabu Abdarahman, ameonesha kukerwa na mazingira machafu aliyoyakuta
katika Soko la Makorora, ambapo ameitaka Halmashauri ya Jiji la Tanga
kuhakikisha inaimarisha hali ya usafi wa maeneo hayo.
Mwenyekiti Abdarahman alionesha masikitiko yake
hayo jana (leo) wakati alipofanya ziara hiyo lengo likiwa kushirikiana na
wafanyabiashara na wananchi kufanya usafi wa mazingira kwenye soko hilo.
Abdarahman ambaye katika ziara yake hiyo alianzia
Soko Uzunguni lililopo Kata ya Centre, alisema kuwa nyakati za maazimisho ya
miaka 47 ya CCM Chama tawala kilitoa maagizo kuhakikisha usafi kwenye masoko yaliyopo
Jijini Tanga unaimarishwa.
Hata hivyo alionesha kushangazwa kwake kukuta
maagizo hayo yakiwa hayajatekelezwa huku akimtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga
kumpatia maelezo suala ambalo lilionekana kukosa majibu ya kutosha.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoani Tanga alisema,
maeneo ya masoko yanapaswa kuwa safi wakati wote kwa vile wananchi ndipo
wanapofika kwa ajili ya kupata mahitaji kwa lengo la kuboresha afya zao.
Mkuu wa wilaya ya Tanga James Kaji alisema,
uchafu huo ni matokeo ya watendaji kutowajika huku akimsihi Kiongozi huyo wa
Chama Mkoa kumpatia muda ili kulishughulikia suala hilo.
"Mheshimiwa Mwenyekiti hapa ni kwamba
hatuwajibiki, na tulishaanza kuchukua hatua ingawa tunapochukua hatua huko
Halmashauri tunaonekana wabaya"alisema Mkuu wa Wilaya ya Tanga James Kaji.
Katika ziara hiyo ya Mwenyekiti huyo wa Mkoa
ilipatikana fursa ya wafanyabiashara kuwasilisha kero zao ambapo Mwasimba Kombo
alilalamikia suala la ukosefu wa Uongozi kwenye soko hilo la Makorora.
Mwasimba alisema, uongozi uliopo umewekwa na
Ushirika jambo ambalo ni kinyume na taratibu za Katiba yao ambapo Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Tanga alimtaka Mkurugenzi kumpatia ufafanuzi jinsi ya Viongozi
wanavyopatikana.
Mwananchi mwingine alilalakikia hali ya kutuama
kwa maji ya mvua kwenye maeneo ya soko hilo la Makorora ambapo wananchi
walitakiwa kufanya subira katika kipindi hiki ambacho upembuzi yakinifu ikiwa
ni sehemu ya kuelekea kwenye ujenzi wa soko jipya.
Pamoja na hayo kikao hicho kilibaini kuwa
kupatikana kwa Uongozi ni matokeo ya chaguzi zinazofanywa na wafanyabiashara
wenyewe na katika hilo Mkuu wa wilaya James Kaji aliahidi kusimamia kwa haraka
suala la kupatikana Viongozi kwenye soko la Makorora.
"Mheshimiwa Mwenyekiti mpaka kufikia Ijumaa
hapa Uongozi utakuwa umeshapatikana.Ndugu zangu wafanyabiashara bila kubaguana
uvyama na mambo mengine mkae nami nitakuja tupate Viongozi "alisema Mkuu
wa wilaya.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdarahman, amemuagiza Mkuu wa wilaya ya
Tanga James Kaji kufuatilia uhalali uuzwaji kiwanja kinachodaiwa kuwa milking
halali ya Serikali.
Kiwanja hicho kipo huko eneo la Kwanjeka ambapo
Wananchi walimweleza Mwenyekiti wa CCM Mkoa kuwa awali eneo hilo lilipangwa
kujengwa Zahanati ila kiwanja hicho kimeuzwa kwa mtu binafsi mwenye nia ya
kuendesha mradi wa aina hiyo kwenye sekta ya afya.
Kutokana na hali hiyo ,Mwenyekiti wa CCM Mkoa alisema iko haja aliyenunua Kiwanja hicho kutafutwa hatua ambayonitasaidia kuwapata waliyokiuza na hivyo kutoa sababu za kuuza huku akisisitiza kusema ikiwezekana kiwanja hicho kinapaswa kurudi Serikalini.
0 Comments