Mchungaji Oscar Faranga Msimamizi wa Kanisa la Moravian Mkoa wa Singida Jimbo la Magharibi Tabora.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na Dotto Mwaibale, (Singidani Blog).
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano la Tanzania, Tulia Ackson anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi katika ibada maalumu itakayo wahusisha Wachungaji 60 kutoka Chuo
Kikuu cha Teofilo Kisanji cha Kanisa la Moravian Tanzania kilichopo Mkoa wa Mbeya watakao
wasili Mjini Singida Mei 13, 2024.
Mchungaji Oscar Faranga wa Kanisa hilo Jimbo la
Magharibi Tabora ambaye ni Msimamizi wa kanisa hilo Mkoa wa Singida alisema
ibada hiyo ya kihistoria ndani ya kanisa hilo itafanyika Kanisa Kuu la Moravian
Mjini Singida na itaongozwa na Baba Askofu Ezekiel Yona wa Jimbo hilo ambapo
pia litafanyika changizo la kupata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Ofisi ya
Jimbo la Mission Singida litakalo ongozwa na Spika wa Bunge Tulia Ackson.
Faranga alisema ujio wa wageni hao mkoani Singida
ni neema kubwa kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya jirani.
Alisema mara baada ya kuwasili wachungaji hao Mei
13, 2024 kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumanne ya Mei 14, 2024 hadi Ijumaa ya
Mei 17, 2024 watafanya kazi ya uinjilisti kwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali,
uchumi, makuzi ya watoto haki zao mafunzo ambayo pia yatawanufaisha wanawake.
Alisema ziara hiyo ya mafunzo itafanyika nyumba
kwa nyumba ambayo itaanza saa 3 asubuhi na kuambatana na matendo ya huruma kwa
kusaidia makundi yasiyojiweza na watoto yatima kwa kutoa zawadi mbalimbali.
Mchungaji Faranga alisema pamoja na mafunzo hayo
wachungaji hao katika siku hizo kuanzia saa 7 mchana watafanya mikutano ya neno
la Mungu hadi jioni katika viwanja vya Kanisa la Moraviani la Mandewa ambalo
lipo nyuma ya Hospitali ya Rufaa ya Mandewa.
"Jumapili ya Mei 19, 2024 wachungaji hao chini
ya mgeni rasmi Spika wa Bunge Tulia Ackson watashiriki semina na ibada itakayo
ongozwa na Baba Askofu Ezekel Yona itakayofanyika katika Kanisa Kuu la Moravian Mjini
Singida," alisema Mchungaji Faranga.
Faranga alisema wachungaji hao watafanya uinjilisti
kwa kupita nyumba kwa nyumba katika mitaa ya Unyamikumi, Magwe, Kimpungua na
Karakana na wataongozwa na wenyeji wao Mchungaji Yona Ezekiel wa Kanisa la
Moravian Parishi ya Mandewa na Mchungaji Yona Mbogo wa kanisa hilo Singida
mjini kwa kusaidiwa na wazee wa kanisa wa Parishi zao.
Mchungaji Faranga alitumia nafasi hiyo kuwaalika
wana Singida na madhehebu mengine kwenda kushirikiana na wachungaji hao kwa
mambo mbalimbali kwani huduma itakayotolewa ni ya bure na kueleza kuwa
maandalizi yote ya ibada hiyo tayari yamekwisha kamilika.








No comments:
Post a Comment