MDAU WA MAENDELEO MANYONI ATOA MASHINE ZA KUDURUFU MITIHANI KWA SHULE 10 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 19 June 2024

MDAU WA MAENDELEO MANYONI ATOA MASHINE ZA KUDURUFU MITIHANI KWA SHULE 10

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea msaada wa mashine za kudurufu mitihani zilizotolewa na mdau wa maendeleo, Joseph Nyalandu.

.................................... 

Na Jumbe Ismailly, Manyoni.             

SHULE za msingi na sekondari kumi zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Manyoni, mkoani Singida zimepokea msaada wa mashine za kudurufu mitihani na hivyo kuondokana na utaratibu waliokuwanao wa kuwachangisha fedha wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hizo kwa ajili ya kudurufu mitihani. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakuu wa shule hizo, Afisa elimu kata ya Muhalala,Mashaka Martini Ringi alisema kwamba msaada huo utakwenda kuleta mapinduzi makubwa sana katika taaluma katika shule hizo. 

Kwa mujibu wa Ringi shule hizo zilikuwa na uhaba mkubwa sana wa mashine za kudurufu na kwamba shulenyingi zilikuwa zikitumia gharama kubwa kwa ajili ya kuzalisha mitihani yao au mitihani ya mazoezi yale ya mara kwa mara yanayotakiwa ili yaweze kukidhi viwango vya elimu. 

“Hivyo basi tunaamini kwa kupitia msaada huu ama msaada huo ambao umetolewa na ndugu yetu Nyalandu tunaenda kufanya mabadiliko makubwa sana katika sekta ya elimu,hususani katika taaluma zetU” alisisitiza Ringi ambaye pia ni Mkuu wa shule ya sekondari Muhalala. 

Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kintinku,Mateso Masinde Bwire alibainisha kuwa shule hiyo ilikuwa na changamoto nyingi kwa sababu shule hiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi,hivyo wakati wa kipindi cha mitihani walikuwa wakitumia gharama kubwa kudurufu mitihani. 

Aidha Masinde licha ya kumshukuru mdau aliyetoa msaada huo lakini aliweka bayana kwamba kupatikana kwa mashine hizo za kudurufu kutaendelea kutatua changamoto iliyokuwa ikizikabili shule zilizopo katika Halmashauri ya wilaya hiyo. 

“Kwa hiyo ninamshukuru kwa asilimia kubwa na pia tupende kusema kwamba kama wapo wengi wa moyo kama wa huyu bwana huyu mfadhili,basi waje wajitokeze kwa wingi kwa sababu ukiangalia shule zilizopewa ni shule chache lakini wilaya ya Manyoni ina shule nyingi”alifafanua mwalimu mkuu huyo. 

Akikabidhi msaada huo wa mashine kumi za kudufu zenye thamani ya shilingi milioni 15,mdau wa maendeleo wa wilaya ya Manyoni, Joseph Nyalandu alisema msaada huo unalenga kuwapunguzia wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule za Manyoni gharama walizokuwa wakitumia wakati wa kudufu mitihani. 

Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Jumanne Mlagaza alisema kupatikana kwa chombo hicho kutaisaidia pia ofisi ya utawala kutoendelea kutoa nyaraka za serikali nje ya ofisi na hivyo kusababisha siri za serikali kuanikwa hadharani,lakini kwa sasa siri za ofisi zitabakia ofisini. 

Shule zilizopokea msaada huo ni pamoja na shule za sekondari za Makanda,Chikuyu,Makuru,Mkwese,Mhalala,Masemapya,Sanza,na Heka wakati kwa shule za msingi ni Kintinku na Lusilile.

Mashine hizo zikiwa ndani ya maboksi baada ya kukabidhiwa.
Picha ya pamoja baada ya makabidhiano ya mashine hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad