Sheikh Mkoa wa Singida, Issa Nasoro akikagua mradi wa mashine ya kusaga na kukoboa unaoendeshwa na Waislamu wa Kata ya Makuro iliyopo Wilaya ya Singida wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya jana.
.............................
Na Dotto Mwaibale, Singidani
Blog
SHEIKH wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro amewataka Waislamu mkoani
humo kutotumika na baadhi ya watu wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi na kuwa hiyo sio kazi yao.
Kiongozi huyo wa dini mkoani hapa Sheikh Nasoro ambaye alikuwa
mgeni rasmi aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Waislamu wa Kata ya
Makuro baada ya kutembelea na kukagua miradi iliyotekelezwa na waislamu wa kata hiyo.
Baadhi ya miradi aliyoitembelea ni mradi wa mashine za kusaga na
kukoboa mahindi ambazo zipo katika vitongoji vya Mkenge, Matumbo, Magugu na
maeneo mengine huku idadi yake zikiwa sita ambapo kila mashine imegharimu zaidi
ya Sh.Milioni 6.
Miradi mingine iliyotembelewa na Sheikh Nasoro wakati wa ziara
hiyo ni madarasa yaliyojengwa kwa ajili ya kufundishia watoto elimu ya dini
ambayo yapo katika kila kitongoji na shamba la mahindi la ekari 50 pamoja na gari aina ya Noah.
"Sasa msitumike kwa ajili ya manufaa ya watu wanaogombea
hatukatai kila mwananchi anayo haki ya kugombea nafasi yoyote anayoitaka
tunachoomba ni Mwenyezi Mungu atuletee viongozi waadilifu na hiyo ndiyo kazi
yetu lakini sio ya kutengeneza mazingira ya kupiga debe kwa wagombea wa ubunge
na udiwani," alisema Sheikh Nasoro.
Alisema wajibu wao ni kumsemea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
mambo mengi ya maendeleo aliyoyafanya kwenye sekta za afya, barabara,
elimu, maji na nyingine zote na kwa upande wake hakuna mtu atakayemshika mdomo asiweze kusema na kueleza kuwa malipo ya mtenda wema ni kumlipa wema.
Alisema miradi yote hiyo Rais Samia ameisimamia na kuikamilisha katika kipindi
kigumu kwani hakuandaliwa baada ya Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Pombe
Magufuli kufariki akiwa madarakani na kufanikiwa kuvivaa viatu vyake kwa
kutekeleza miradi hiyo kwa zaidi ya asilimia 80.
Sheikh Nasoro alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Waislamu wa kata
hiyo kwa kuwa vinara wa kutekeleza maagizo ya ofisi yake ya kila waislamu
kwenye kata zao kuanzisha miradi ya maendeleo ambapo aliwatia moyo kuwa hata
maono yao ya kupata trekta kwa ajili ya kilimo yatafanikiwa kwa kuwa tayari
wameonesha njia ya mafanikio.
"Mama Samia anatoa fedha za mikopo na ninyi kupitia umoja
wenu huo hamjazuiliwa tuwasiliane tuone namna mtakavyo zipate fedha hizo ili
mkopeshwe," alisema Sheikh Nasoro.
Aidha, Sheikh Nasoro aliwataka waislamu wa kata hiyo baada ya
kupata mafanikio hayo sasa waanzishe kilimo cha zao la biashara la alizeti na wafungue
kiwanda cha uchakataji na kuongeza thamani ya zao hilo kwa kuuza mafuta
yatakayo andikwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kiwanda cha Mafuta
Makuro.
Kwa upande wake Diwani wa Vitu Maalumu wa kata hiyo Hadija Msuri
alisema kazi kubwa wanayoifanya ni kupokea maelekezo kutoka kwa Rais Samia na
Mufti wa Tanzania kupitia viongozi wao na kuyapeleka kwa wananchi na
kushirikiana nao na ndio chanzo cha mafanikio yao mbalimbali kwenye kata hiyo.
Mlezi wa Waislamu wa kata hiyo, Iddi Isango alimuomba
Sheikh Nasoro kuwasaidia kupata umeme kwa ajili ya kuendesha mashine hizo
ambazo zipo katika vitongoji mbalimbali huku zikiwa na miundombinu
yote lakini hazifanyi kazi kutokana na TANESCO Mkoa wa Singida
kushindwa kuwaunganishia umeme.
Mtaalamu na Mwanasheria wa Ofisi ya Sheikh Nasoro Abdul Ramadhani
alisema Waislamu wa kata hiyo wanajitambua na wanafanya kazi zao kwa kufuata
sheria na taratibu za nchi ndio maana wanapata mafanikio makubwa.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro akipokelewa alipokuwa akianza ziara yake ya kikazi katika Kata ya Makuro.
Sheikh Issa Nasoro akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waislamu wa Kata ya Makuro wakati akihitimisha ziara yake.







No comments:
Post a Comment