Na; Mwandishi Wetu – Arusha
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu,
Mheshimiwa Jenista Mhagama, amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuzingatia
vipaombele ambavyo ni muhimu kupewa msukumo katika utekelezaji wa shughuli kwa
mwaka wa fedha 2024/25.
Ameyasema
hayo mapema leo tarehe 31 Julai, 2024 Jijini Arusha alipokuwa akifungua kikao
kazi cha Mazingativu (Retreat) kilichohusisha watendaji na watumishi kutoka
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) pamoja na Taasisi zake.
Akiongelea
kipaombele cha kwanza ambacho ni Kuratibu Ujenzi wa Majengo ya Serikali katika
Mji wa Serikali Mtumba, Waziri Mhagama alisema, Ofisi ya Waziri Mkuu katika
mwaka wa fedha 2024/25 itaendelea na uratibu wa ujenzi wa majengo ya Ofisi za
Wizara, Taasisi pamoja na miundombinu mbalimbali katika Mji wa Serikali wa
Mtumba, pamoja na kutoa vibali vya ujenzi kwa Taasisi za Serikali zinazoendelea
kuhamia Makao Makuu ya Chama na Serikali Dodoma, ikiwa na nia kuhakikisha kuwa
Awamu ya Tatu ya ujenzi wa Mji wa Serikali inakamilika kwa wakati na watumishi
wanahamia katika majengo hayo ndani ya mwaka wa fedha 2024/25 na kuelekeza kuwa Uratibu huo uimarishwe sambamba na kuweka
ufuatiliaji wa karibu wa ujenzi pamoja na ununuzi wa samani za majengo yote.
Akiongelea
suala la Kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli za
Serikali, Waziri Mhagama Alibainisha kuwa, Kulingana na muundo mpya wa Ofisi ya
Waziri Mkuu ipo Idara mpya iliyoundwa ambayo jukumu lake kubwa ni kusimamia
masuala yote ya Tathmini na Ufuatiliaji wa Utendaji wa Serikali kwa ujumla
kuanzia ngazi za Wizara na taasisi zake, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
Aidha Waziri
Mhagama Aliipongeza Idara hiyo kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya na kusema
kuwa hadi saa imeandaa Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini na
imekamilisha Mwongozo wa Menejimenti ya Tathmini nchini na Mwongozo wa kufanya
tathmini ya utayari wa masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Taasisi za
Serikali.
“Baada ya
kazi hiyo nzuri sasa tunahitaji kuona matokeo ya utendaji unaotokana na
kuimarishwa kwa ufuatiliaji na tathmini, Masuala mbalimbali ambayo ni muhimu
kutiliwa mkazo ni ufuatiliaji wa maoni na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo hutoa mwelekeo wa utendaji wa Serikali.”
Alisisitiza Waziri Mhagama.
Aliendelea
kusema kuwa, Hatua hii itajenga imani zaidi kwa wadau kuhusu hatua zinazochukuliwa
na Serikali kudhibiti matumizi mabaya ya mali za umma na kuelekeza kazi ya
kukamilisha Mfumo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Shughuli
za Serikali (Government Wide Integrated Monitoring and Evaluation System)
ikamilike mapema kabla ya mwezi Disemba, 2024 na ili mfumo huo uanze kufanya
kazi na kuwezesha upimaji wa utendaji wa Serikali kufanyika kwa urahisi, haraka
na ufanisi mkubwa.
Akiongelea
kuhusu Kuimarisha Uwezo wa Uchapishaji wa Nyaraka za Serikali, Waziri Mhagama
alipongeza jithada za maboresho yanayoendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
kiwanda kipya, ununuzi wa mashine mpya saba na matengenezo ya mashine zaidi ya
13.
“Nawapongeza
wataalam waliobuni na kuandaa maandiko yaliyowezesha kupata mafanikio haya kwa
muda mfupi, Naendelea kutoa wito kuwa shughuli za uchapaji wa nyaraka zote za
Serikali ufanywe na Idara ya Mpiga Chapa wa Serikali na ufuatiliaji ufanyike
kwa Taasisi ambazo zinakiuka masharti ya Waraka uliotolewa kwa Watendaji wote.”
Alisisitiza Waziri Mhagama.
Akizungumza
kuhusiana na Vita dhidi ya biashara haramu na Matumizi ya Dawa ya kulevya,
Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo kupongeza hatua mbalimbali za udhibiti wa
dawa za kulevya nchini akitolea mfano wa mafanikio yaliyopatikana na kusema
kuwa ni kiashiria kikubwa cha utendaji mzuri wa Mamlaka ya kuthibiti na
kupambana na dawa za kulevya nchini.
“Dhahiri
kwamba nchi yetu imejipatia heshima ndani na nje ya nchi kwa kuwa na mifumo
imara ya udhibiti wa dawa za kulevya na tumeweza kuwalinda watu wetu dhidi ya
matumizi ya dawa za kulevya.” Alisema
Aidha,
Waziri Mhagama alibainisha kuwa, ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita (6) chini
ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa biashara ya
dawa ya kulevya inakomeshwa, kwani ina madhara makubwa sana kwa jamii ya
Watanzania na inaathiri nguvu kazi ya Taifa na kutoa wito wa kuendeleza
jitihada za kuendeleza mapambano,
sambamba na kuweka msukumo wa utekelezaji wa Sera mpya ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2024.
Akiongelea
suala la Usimamizi na uratibu wa masuala ya Uchaguzi, Waziri Mhagama alisema,
Mwaka huu wa 2024 na mwaka 2025 kutafanyika chaguzi mbalimbali, Mwaka 2024
kutafanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Mwaka 2025 utafanyika Uchaguzi
Mkuu.
“Chaguzi hizi zinahitaji maandalizi ya kutosha
na uratibu mzuri, hivyo nitoe wito kwa Taasisi inayohusika na maandalizi ya
Uchaguzi pamoja na Idara ya Bunge na Siasa kufanya maandalizi na uratibu kwa
ukamilifu ili kufanikisha chaguzi hizi.”
Akihitimisha
hotuba yake alitumianfursa hiyo kutoa pole kwa wananchi waliopatwa na maafa ya
Mafuriko mwishoni mwa mwaka 2023 hadi mwezi Aprili, 2024, na Mvua za El Nino,
na kusema kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na maafa
hayo.
“Nitumie fursa hii kupongeza jitihada zilizochukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) katika kukabiliana na maafa hayo, Tuendelee kufanya kazi kama Timu ili kupata matokeo makubwa zaidi katika kukabiliana na majanga huku jitihada kubwa zikielekezwa katika utoaji wa elimu kwa umma.”










No comments:
Post a Comment