Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu akipokea nyaraka mbalimbali zinazoelezea majukumu majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi hiyo, Bi. Sarah mara baada ya kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma .
NA MPIGA PICHA WETU.
------------------------------
MWENYEKITI wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu aipongeza Ofisi ya
Makamu wa Rais kwa utoaji wa elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka
ambao ni fursa ya ajira.
Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi
hizo leo Jumatano Julai 7, 2024) wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu
wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane)
yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa
taka zinazozalishwa nchini kwa sasa
zimekuwa ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za
uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na
kuchochea maendeleo ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.
“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu kuhusu
fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha jamii na
kuhamasisha utunzaji wa mazingira”
amesema Mhe. Jaji Mwaimu.
Aidha Jaji Mwaimu amewataka
wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa
Rais na kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya
uhifadhi wa mazingira kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika
ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa taka ni fursa
iliyojificha na hivyo elimu kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani
sio
kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo,
bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.
“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa
kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza kuchangamkia
fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na namna zinavyotakiwa kutenganishwa” amesema Jaji Mwaimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde amesema
Ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala
ya Muungano na Mazingira ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya
habari.
Ameongeza kuwa katika kupanua
wigo wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho
hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya
kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.
Ametaja maeneo hayo kuwa ni
pamoja na masuala ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa
buluu, fursa zitokanazo na taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
“Kupitia maonesho tuna nyaraka
mbalimbali ambazo ni vitabu ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa
Rais, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira
(2022-2032), vipeperushi, majarida ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu
kwa wananchi na wadau nk” amesema Kibonde.
Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana
na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki
maonesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika
kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8
Agosti, 2024.
Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.
0 Comments