Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Damas Ndumbaro akifungua Tamasha la Kitaifa la Utamaduni mjini Songea mkoani Ruvuma.Septemba 20, 2024..........................
Na Elizabeth Zaya, Songea
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk.Damas Ndumbaro, ameiagiza Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania(TCRA), kuwashughulikia wale wote wanaohamasisha
mmonyoko wa maadili kupitia mitandao ya kijamii na kusigina mila na tamaduni za
Kitanzania.
Dk.Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua Tamasha la Kitaifa la
Utamaduni mjini Songea mkoani Ruvuma.
Amesema hakuna taifa lolote duniani lisiloheshimu na kuthamini mila,
desturi na tamaduni zao na kwamba ni jukumu la TCRA kuwashughulikia ipasavyo
wale wote wanaotumia vibaya mitandao hiyo.
"TCRA mna jukumu kubwa la kuhahikisha wale wanaokiuka mila na desturi
za Kitanzania, kuzisigina na kuhamasisha mambo yanayochangia kuleta mmonyoko wa
maadili katika nchi yetu wanashughulikiwa ipasavyo,”amesema Dk.Ndumbaro.
“Tusipokuwa na utamaduni wetu, hatuna utu na tusipouenzi hatutauendeleza na
ili taifa liwe hai lazima kuenzi na kuendeleza utamaduni wake, lazima
turithishe utamaduni kwa vijana pamoja na watoto,tuwafundishe mila na desturi
za Kitanzania, kiswahili, miiko yetu na ndipo taifa litaendelea kuwa hai.”
Amesema licha ya umuhimu mkubwa uliopo katika kuheshimu haki za binadamu,
lakini wapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya tafsri ya haki hizo za
binadamu kuingiza tamaduni za kigeni ambazo ni kinyume na zile za Kitanzania na
kwamba suala hilo halikubaliki.
"Haki za binadamu ni suala muhimu sana ambalo tunahitaji kuliheshimu
na kulizingatia, lakini baadhi tunatumia haki za binadamu vibaya kwa kuingiza
tamaduni za kigeni zisizofaa katika jamii yetu, tusitumie kisingizio hicho
kukiuka miiko, maadili na desturi zetu kwa kuwa tukifanya hivyo tutakuwa
tunaiua nchi yetu na kufanya hivyo nchi yetu itakuwa mfuu,”amesema Dk.Ndumbaro.
"Waswahili wanasema mkataa kwao ni mtumwa na sisi tusikatae kwetu,
katika kuenzi mila na desturi lazima tutambue taasisi muhimu ambazo zinaweza
kufanikisha jambo hilo tukianza na familia, taasisi za dini, vyombo vya habari,
shule na nyinginezo.”
Amesema maadili mazuri ndio yatalisaidia taifa kuondoa mmonyoko wa maadili.
“Tunaamini kwamba taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kulinda
maadili ya nchi yetu, watengeneza maudhui katika mitamdao ya kijamii na vyombo
vya habari vina umuhimu mkubwa, kwa hiyo ninavisihi vitusaidie katika
hilo,”amesema Dk.Ndumbaro.
Dk.Ndumbaro amesema kaulimbiu katika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni mwaka
huu inasema ‘utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza."









No comments:
Post a Comment