Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a ,akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka wakati akizungumza na waandishi wa habari.jijini Dar es Salaam, Januari 23, 2025.
................................................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo na ushauri kwa taasisi mbalimbali kuchukua tahadhari ili kukabiliana na mKaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka kwa waandishi wa habari. atukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa yatakayoweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Angalizo hilo limetolewa Januari 23, 2025 jijini, Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka kwa waandishi wa habari.
“Mwelekeo wa mvua tunaoutoa kwenu wana habari umezingatia zaidi kipindi cha mvua za Masika kwa miezi mitatu na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi vitazingatiwa katika utabiri wa kila siku na utabiri wa kila mwezi,” alisema Chang’a.
Alisema watumiaji wa taarifa hiyo wanashauriwa kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Akizungumzia mifumo ya hali ya hewa alisema Joto la bahari la juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Hindi ikilinganishwa na upande wa magharibi mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Afrika Mashariki).
Alisema hali hiyo inatarajiwa kupunguza kasi ya msukumo wa unyevunyevu kutoka Bahari ya Hindi kuelekea maeneo ya ukanda wa pwani ya nchi. Eneo la Tropiki ya Kati ya Bahari ya Pasifiki, linatarajiwa joto la Bahari la chini kidogo ya wastani. Vilevile, joto la bahari la wastani linatarajiwa katika eneo la pwani ya kusini mashariki mwa Bahari ya Atlantiki (Pwani ya Angola). Hali hii kwa pamoja inatarajiwa kudhoofisha mifumo inayosababisha mvua katika msimu huu.
Aliongeza kuwa kwa upande mwingine, upepo katika Ziwa Victoria unatarajiwa kuvuma kutoka magharibi na kueleza kuwa hali hiyo inatarajiwa kuimarisha kidogo mifumo inayosababisha mvua katika maeneo yaliyopo upande wa mashariki mwa Ziwa Victoria na nyanda za juu kaskazini mashariki.
Dkt. Chang’a akizungumzia athari zinazoweza kutokea na ushauri wa kisekta ulioandaliwa na TMA Tanzania kwa kushirikiana na wataalam wa sekta husika katika mkutano wa wadau wa hali ya hewa uliofanyika Januari 20, 2025, na mkutano na Wanahabari uliofanyika Januari 22, 2025. Wadau wa sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii wanashauriwa kupanga na kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia taarifa mahususi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.
Akizungumzia kuhusu angalizo na ushauri wakati wa kipindi hicho kwenye eneo la Kilimo na Usalama wa Chakula alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani. Vilevile, wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea yanayoendana na hali ya ongezeko la unyevu kama vile ukungu yanatarajiwa kuongezeka na kuathiri mazao kama ndizi, mahindi,mpunga, mihogo na maharage. Hata hivyo hali ya upungufu wa unyevu inaweza kujitokeza hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Alisema Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, kuhifadhi maji shambani, kuzuia mmomonyoko na upotevu wa rutuba kutokana na kutuwamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko. Aidha, inashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo na kudhibiti kwa wakati magonjwa ya mimea na wadudu waharibifu ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“ Wakulima wanashauriwa kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi. Aidha, wakulima na maafisa ugani wanashauriwa kuendelea kutumia utabiri wa siku na siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu, “ alisema Chang’a.
Akizungumzia kuhusu Mifugo na Uvuvi alisema hali hiyo inaweza kupelekea athari katika ukuaji wa mazao ya kilimo hivyo kama hali hiyo itajitokeza inapaswa kutolewa taarifa haraka kwa vyombo vinavyohusika
Alisema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani, wafugaji nawavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki. Hata hivyo, milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo, na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza.
Aliongeza kuwa upungufu wa maji unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani na hivyo unaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Alisema Wafugaji wanashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo. Aidha, wafugaji na wavuvi wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa na maofisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na kuendelea kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa wakati wa msimu.
Dkt. Chang’a akizungumzia Utalii na Wanyamapori katika kipindi cha Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa zinaweza kusababisha uhaba wa malisho na maji kwa wanyamapori katika mbuga na mapori ya akiba na hivyo kusababisha migogoro kati ya wanyamapori na jamii inayowazunguka. Hata hivyo, mvua nyingi zinaweza kusababisha kutuama na kusambaa kwa maji na kusababisha kuhama kwa wanyamapori, hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa wanyama wanaofugwa kutokana na wanyamapori kuingia katika maeneo ya jamii yanayozunguka hifadhi na mapori ya akiba. Pia, hali hii inaweza kusababisha hatari kwa binadamu na wanyama wanaofugwa kutokana na kushambuliwa na wanyama pori.
Alisema Mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu mbalimbali katika mbuga na mapori ya akiba na kujenga uelewa kwa jamii ili kuchukua hatua stahiki kutokana na athari zinazoweza kujitokeza. Hivyo, jamii inashauriwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanyamapori wanapoingia katika maeneo yao ya makazi.
Akizungumzia Usafiri na Usafirishaji alisema kwa ujumla, Sekta ya Usafiri na Usafirishaji inatarajiwa kunufaika kutokana na mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani katika msimu huu wa Masika. Kwa upande mwingine, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani.
Alisema katika kipindi hicho matukio ya uharibifu wa miundombinu ya Barabara na reli sambamba na kuongezeka kwa ajali za usafiri wa nchi kavu yanaweza kujitokeza yakiwemo matukio ya kuchelewa, kuahirishwa kwa safari za ndege na kwenye maji pamoja na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji katika Sekta ya Usafiri wa Anga na kwenye maji zianaweza kujitokeza.
“Wadau wa sekta hii wanashauriwa kuchukua hatua stahiki katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya usafirina usafirishaji ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Chang’a.
Chang’a akizungumzia Nishati, Maji na Madini kupungua kwa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kunatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Alisema ongezeko la vina vya maji katika mabwawa na mito linatarajiwa kujitokeza hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani na hivyo kupelekea kuongezeka kwa matukio ya mafuriko hususan katika maeneo yanayoathiriwa zaidi na mafuriko.
Alisema upungufu wa maji unaweza kupelekea ongezeko la gharama za kutibu maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kueleza kuwa matumizi endelevu ya rasilimali maji yanasisitizwa hususan katika shughuli za umwagiliaji, uzalishaji wa umeme wa maji, shughuli za madini, matumizi ya viwandani na majumbani.
Chang’a alisema jamii na Mamlaka za Nishati na Maji zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kuepuka athari zinazoweza kuathiri miundombinu ya maji na nishati.
Dkt. Chang’a akizungumzia Mamlaka za Miji na Wilaya alisema wakati wa Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo zinaweza kupelekea upungufu wa upatikanaji wa maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.
Alisema Mamlaka za miji na wilaya zinashauriwa kuchukua hatua madhubuti ikiwemo kuimarisha na kuboresha mifumo ya usambazaji maji safi ili kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa maji katika kaya na sekta nyingine. Vilevile, Mamlaka zinashauriwa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maji taka ili kuepuka athari za kiafya zinazohusiana na upungufu wa maji.
Alisema pia, Mamlaka husika zinashauriwa kutoa elimu ya uelewa kwa timu mbalimbali za usimamizi
katika halmashauri kuhusu hali ya hewa inayotarajiwa katika msimu huo hiyo ni pamoja na kuhamasisha uundwaji wa mipango na bajeti mahususi za kisekta ili kujiandaa na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Alisema katika msimu huo Mamlaka husika zinashauriwa kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote kwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji sambamba na kufanya matengenezo ya mara kwa mara.
Dkt. Chang’a akizungumzia Sekta ya Afya juu ya uharibifu wa miundombinu ya maji unaoweza kusababishwa na maji ya mvua kutuama na kutiririka katika makazi ya watu unaweza kusababisha uchafuzi wa maji na hivyo kusababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko yanayohusiana na maji machafu na wadudu wadhurifu.
Alisema Mamlaka za Afya na jamii zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ili kupunguza athari hasi za kiafya zinazotarajiwa kwa kuharibu mazalia ya mbu, kutibu maji kabla ya kuyatumia, kunywa maji safi na salama pamoja na kuhakikisha uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kutosha katika vituo vya Afya. Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani, jamii inaweza kulazimika kutumia maji yasiyo safi na salama hivyo hatua stahiki za kiafya zinashauriwa kuzingatiwa ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Akizungumzia Sekta Binafsi alisema shughuli za kilimo biashara na uzalishaji viwandani zinaweza kuathirika kutokana na upungufu wa malighafi za kilimo unaotokana na upungufu wa mvua hususan kwenye maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha ongezeko la gharama za upatikanaji wa malighafi na uendeshajina kuwa upungufu wa mvua unaweza kuathiri ubora wa bidhaa mfano miti ya nguzo, mbao, nyama na asali.
Alisema Wadau wa Sekta Binafsi wanashauriwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali ikiwemo wataalam wa hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza. Taasisi za Benki na Bima zinashauriwa kuandaa na kutoa huduma mahususi kwa wadau ili kujenga ustahimilivu katika biashara.
Akizungumzia Menejimenti ya Maafa alisema wakati wa Vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kupelekea uharibifu wa miundombinu, mazingira, mlipuko wa magonjwa pamoja na upotevu wa mali na maisha. Hivyo, mamlaka husika katika Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini inashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Alisema Wasimamizi wa shughuli za mazingira wanashauriwa kuzingatia taarifa hii ipasavyo na kuwa, sekta, mamlaka husika na Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji/Mitaa zinashauriwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa elimu ya maafa na miongozo itakayohamasisha katika kujiandaa, kuzuia au kupunguza na kukabiliana na maafa pamoja na kuhamasisha uhifadhi wa chakula.
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa Vyombo vya Habari alisema wanashauriwa kufuatilia na kupata taarifa sahihi za utabiri wa Hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kutoa taarifa kwa wakati kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu athari zinazoweza kujitokeza.
“Wanahabari wanashauriwa kutafuta na kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa wataalam wa sekta husika ili kuandaa na kusambaza makala na ripoti za kisekta kwa lugha rahisi kwa lengo la kuhabarisha na kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya utabiri wa hali ya hewa katika kukabiliana na athari zinazotarajiwa, “ alisema Chang’a.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika.
Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Kwa Mawasiliano ya kutoa taarifa zozote zitakazohusu athari kutokana na mvua hizo kwa taasisi zote zielekezwe kwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Chuo Kikuu cha Dodoma,Jengo la Utawala, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, 1 Mtaa wa CIVE, S.L.P 27, 41218 Dodoma; Simu: +255 26 2962610: Nukushi: +255 26 2962610 Barua pepe; met@meteo.go.tz; Tovuti: www.meteo.go.tz.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a, akisisitiza jambo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mchambuzi wa Hali ya Hewa , Dkt. Alfred Kondoe, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari.








No comments:
Post a Comment