MAMA MWENYE MTOTO MLEMAVU APIGA MAGOTI MBELE YA WATANZANIA KUOMBA MSAADA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 28 March 2025

MAMA MWENYE MTOTO MLEMAVU APIGA MAGOTI MBELE YA WATANZANIA KUOMBA MSAADA

Mtoto Aden Ernest Mlay (17) Mwenye Ulemavu akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Muheza Kibaha mkoani Pwani.

................................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

NGUGU zangu watanzania mwenzenu nimekwama sina mbele wala nyuma, sina mahala pa kuishi, sina uhakika wa chakula na  mtoto wangu ni mlemavu na pia ni mgonjwa, gharama za matibabu yake ni kubwa sasa ni zaidi ya miezi sita hajaenda shule.

Hivyo ndivyo anavyoanza kujieleza Bi. Naemi Mandimbula (50) Mkazi wa Mtaa wa Muheza Kibaha mkoani Pwani, mama wa mtoto huyo mwenye ulemavu kuhusu madhira anayopata kutokana na changamoto mbalimbali za maisha zinazo mkabili ikiwemo hiyo ya kuumwa kwa mtoto wake Aden Ernest Mlay (17)

“Nimeangaika sana ili nipate msamaha wa matibabu ya mtoto wangu bado sijafanikiwa siwezi kufanya chochote wala kwenda mbali na nyumbani kutafuta riziki kwa sababu ya mwanangu jambo ambalo limeongeza ugumu wa maisha yangu.,” alisema Mandimbula.

Alisema mume wake alimkataa mtoto huyo (Dotto) kwa madai kuwa katika familia yao huwa hawazai wenye ulemavu na kuwa Kulwa wake yupo kidato cha tatu wakati ndugu yake huyo akiwa darasa la tano  kutokana na changamoto aliyonayo.

Mama huyo anasema mtoto wake huyo ni mlemavu ambaye hawezi kufanya chochote bila ya kusaidiwa na pia anachangamoto ya maradhi ya ubongo na kukakamaa mwili na alipokwenda Hospitali aliandikiwa dawa ambazo dozi yake ni kuanzia Sh. 50,000 hadi 60,000 ambazo anazitumia kwa mwezi fedha ambayo ameshindwa kuimudu.

Amesema changamoto kubwa aliyonayo ni sehemu ya kuishi baada ya nyumba aliyokuwa amesitiriwa kuishi kubomolewa kutokana na kujengwa eneo la Serikali na kuwa hivi sasa anaishi kwenye kibanda alicho jenga kwa muda kilichopo eneo hilo.

Mjumbe wa shina namba 10 wa Mtaa wa Muheza, Abuu Raphael amethibitisha kumfahama mama huyo na madhira yote anayoyapitia na kueleza kuwa amekuwa akimsaidia katika hatua mbalimbali za matibabu ya mtoto huyo huku kubwa akiomba asaidiwe kupata msamaha wa matibabu na eneo la kuishi kwa kuzingatia kuwa ni mmoja wa watu waliopo kwenye kundi la kaya maskini.

“Nimekuwa nikimuandikia barua mbalimbali kwenda maeneo tofauti kwa ajili ya kupata msaada hadi kwa  mkuu wa wilaya amekwisha fika,” alisema Raphael.

Ngugu watanzania mmemsikia huyo mama akielezea changamoto aliyonayo hivyo anapiga magoti mbele yenu akihitaji msaada wenu iwe fedha na ushauri kama alivyosema ana mtoto ambaye ni mgonjwa, hana sehemu ya kuishi na hata kula yake ni ya kubahatisha hivyo shime tujitokeze kumsaidia hata kama utakuwa na Sh. 1000 kwake ni kubwa kwani kutoa ni moyo wala sio utajiri,

Mtoto Aden Ernest Mlay (17) Mwenye Ulemavu akiwa amepakatwa na mtoto mwezake.
Bi. Naemi Mandimbula (50) Mkazi wa Mtaa wa Muheza Kibaha mkoani Pwani, mama wa mtoto huyo akiwa amempakata mtoto wake, Aden Mlay (17)
Hiki ni kibanda anachoishi BiNaemi Mandimbula (50) na familia yake.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad