ANDENGENYE AJITOSA RASMI KWENYE SIASA AUTAKA UBUNGE JIMBO LA BUSOKELO - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, July 1, 2025

ANDENGENYE AJITOSA RASMI KWENYE SIASA AUTAKA UBUNGE JIMBO LA BUSOKELO


 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tukuyu Wilaya ya Rungwe, Abdallah Mpokwa (kulia), akimkabidhi fomu Thobias Andengenye ya kuomba ridhaa ya kugombea ubunge Jimbo la Busokelo lililopo Rungwe Mkoa wa Mbeya Juni 28, 2025.
............................................ 

Na Dotto Mwaibale 

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma CGF (Rtd) Mhe. Thobias Andengenye ameingia rasmi kwenye siasa na tayari amechukua fomu kuomba ridhaa ya chama chake kuwania kuteuliwa kugombea Ubunge Jimbo la Busokelo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Andengenye anakuwa miongoni mwa makada wa chama hicho watakaochuana na mbunge wa jimbo hilo, Atupele Mwakibete anayetetea nafasi yake.

Wengine wanaowania nafasi hiyo katika jimbo hilo ni mtaalamu wa masuala ya  ugavi, ununuzi na masoko, Ezekiel Mwakyambo Gwatengile, Atupele Mwakibete anayetetea nafasi hiyo, Wakili Gerald Mwayonde, Lutengano Mwalwiba na wengine. 

Mwana CCM atakayepata ridhaa ya kugombea nafasi hiyo na kushinda kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu atakwenda kuwahudumia wananchi kwenye kata 13 zilizopo katika jimbo hilo la Busokelo lililopo Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

Andengenye anatajwa kuwa ni mtia nia mwenye ushawishi na uwezo mkubwa kutokana na kushika nafasi mbalimbali za uongozi na ni mtu wa msimamo asiyeyumba, mweledi na msomi. 

Mwana siasa huyo amewahi kufanya kazi ndani ya jeshi la polisi na kushika nyadhifa mbalimbali za juu kama  Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kupata mafunzo katika chuo maarufu cha Bramshill nchini Uingereza alikosomea uongozi.  

  Mtia nia huyo alijiunga na jeshi la polisi akitokea masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata shahada yake ya kwanza ya Utawala na Uhusiano wa Kimataifa. 

Mbali na kushika nafasi hizo pia amefanya kazi ya ukamanda wa polisi kwenye baadhi ya mikoa na baadae kuteliwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania enzi za Uhai wake, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. 

Baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo, kwa mara nyingine Hayati  Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma nafasi aliyoitumikia kabla hajaingia rasmi kwenye kinyang’anyiro hicho cha ubunge.

Katika jimbo hilo Serikali imefanya kazi kubwa chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia mbunge aliyemaliza muda wake, Atupele Mwakibete lakini kutokana na kuwepo kwa demokrasia watia nia hao wa nafasi hiyo wamejitokeza ili atayefanikiwa kuwa mbunge aweze kuendeleza  maendeleo kwenye maeneo  ambayo bado yana changamoto kwenye sekta ya elimu, afya, barabara, umeme, kilimo, uhifadhi wa mazingira na mengineyo.

Jimbo la Busokelo linahitaji kupata viongozi na si bora viongozi wenye uwezo, weledi, maono na ubunifu ili liweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kutekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi ya 2025/ 2030.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad