Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba, Mhe. Proscovia Jaka Mwambi.
......................................
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), ambao ni miongoni ya jumuiya za chama hicho imekuwa ni nguzo muhimu ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora nchini.
Vijana ndani ya chama hicho wamekuwa wakishika nafasi za uongozi baada ya kuandaliwa vizuri wakianzia Idara ya Chipukizi iliyoanzishwa na waasisi wa Taifa chini ya Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Jumuiya hiyo ya vijana ambayo ndani yake ipo Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu imekuwa ikitoa mafunzo ya uongozi bora, maadili, uaminifu, kufanya kazi kwa kujitolea, itikadi, Itifaki pamoja na uzalendo wa dhati.
Mafunzo hayo yamekuwa ni kichocheo kikubwa katika nchi
kupata viongozi mahiri waliopitia
kwenye jumuiya hiyo ambao wapo katika nafasi mbalimbali za utumishi.
Miongoni mwao walipata morali wa kuingia kwenye masuala ya siasa kupitia chama hicho baada ya kuwaona wazazi, ndugu na jamaa na watu wengine waliokuwa viongozi ndani ya chama hicho na serikali walivyofanya kazi nzuri.
Leo hii tunaona baadhi ya vijana waliopitia jumuiya hiyo
ambao wazazi wao wamekitumikia chama wakishika nafasi mbalimbali na kufanya vizuri baada ya kuwa viongozi kutokana na kuandaliwa.
Hatua hiyo ni nzuri
na wala siyo dhambi tukizingatia usemi wa wahenga unaosema ibada njema huanzia
nyumbani, maji hufata mkondo, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, mtoto wa nyoka ni
nyoka na mingine mingi.
Watoto hao wa viongozi na wale ambao wamepitia katika jumuiya hiyo
wanaonesha njia, uwezo na uzalendo wa kulitumikia taifa hatua ambayo tunajivunia na
kukipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kazi kubwa ya kuwaandaa.
Katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025 tumeona jinsi
kundi kubwa la vijana wa chama hicho walivyojitokeza kwa wingi kuchukua fomu za
kutia nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuwapitisha kugombea nafasi za
udiwani na ubunge.
Wamefikia hatua hiyo baada ya kujiona wameiva vilivyo hivyo
wataweza kulitumikia taifa.
Proscovia Jaka Mwambi ni Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba ambaye ni mtoto wa Mwanadiplomasia Hayati Jaka Mgwabi Mwambi kiongozi ambaye alihudumu vizuri ndani ya chama na Serikali.
Katibu Tawala huyo ni zao la UVCCM aliyeshika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na jumuiya zake ambazo zipo mstari wa mbele katika kuwajenga vijana kimaadili.
Moja ya nafasi aliyowahi kushika ni ya Katibu Myeka wa Naibu
Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara nafasi aliyoitumikia kwa uadilifu na baadae kuaminiwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumteua kuwa Katibu
Tawala wa wilaya hiyo.
Nafasi nyingine alizowahi kushika ndani ya chama hicho na Jumuiya
zake ni Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa, Mjumbe
wa Baraza Kuu UVCCM Taifa, Mjumbe wa Baraza UWT Mkoa wa Morogoro, Katibu
Msaidizi Idara Siasa uhusiano wa Kimataifa na Katibu Msaidizi Idara ya Itikadi,
Mafunzo na Uenezi.
Aidha nafasi nyingine ni Katibu wa Mwenyekiti UWT Taifa, Katibu wa muda wa Katibu Mkuu UWT Taifa,
Katibu Msaidizi Idara ya Organizesheni UWT Taifa, Katibu wa UWT Wilaya ya
Kibaha, Mjumbe wa Baraza UWT Mkoa wa Pwani, Mjumbe wa Baraza UWT Wilaya Kibaha,
Mjumbe wa Halmashauri Kuu Wilaya ya Kibaha, Katibu wa UWT Tawi la Urusi,
Mwekahazina Tawi la CCM Urusi na Hamasa UVCCM Chuo cha Mipango Dodoma.
Tumeona jinsi anavyofanya kazi katika wilaya hiyo
akisaidiana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Erasto Sima hakika Mhe. Rais hakubahatisha
kumpa nafasi hiyo.
Mwambi ambaye ni mshauri na mtekelezaji mkuu wa shughuli
zote za Serikali wilayani humo liwe jua iwe mvua amekuwa kazini wakati wote huku
akishirikiana kwa karibu na Maafisa Tarafa wote ndani ya wilaya hiyo na
wananchi kwa ujumla.
Kazi yake nyingine ni kumshauri mkuu wa wilaya masuala
yanayohusu ulinzi na usalama, utekelezaji wa majukumu ya sherehe na dhifa,
malalamiko ya wananchi, kuandaa makadirio ya matumizi, msajili wa ndoa na
kusaidia Halmashauri kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Kutokana
na jitihada anayoifanya ya kuwatumikia wananchi huenda Rais ajaye baada ya
uchaguzi mkuu akampa nafasi nyingine ya juu na kumfanya aendelee kuwa kiongozi
bora na pengine kufikia nafasi ya juu zaidi kupita aliyofikia baba yake kwani
nyota njema uonekana mapema asubuhi.
Hayati Jaka Mgwabi Mwambi alizaliwa mwaka 1950 na alifariki
dunia mwaka 2019, alikuwa mwanasiasa na mwana diplomasia mbobezi aliyepata kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Tanga na Iringa na Makamu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Taifa.
Makala haya yameandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754362990)
Katibu Tawala Wilaya ya Bukoba, Mhe. Proscovia Jaka Mwambi (aliyeshika karatasi), akijumuika katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu 2025.









No comments:
Post a Comment