Katika hatua ya kihistoria ya siasa nchini, baadhi ya vyama vya upinzani vimeonyesha ushirikiano wa wazi na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa jinsi inavyoendesha maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Wameeleza imani yao katika uwazi, ushirikishwaji na weledi vinavyoonekana kuleta matumaini mapya kwa uchaguzi wa haki, huru na wa kuaminika.
Katika Mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Vyama vya Siasa uliofanyika jijini Dodoma, viongozi wa vyama vya siasa waliothibitishwa walionyesha msimamo chanya kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi.
“Uwazi huu unatujengea imani” – Prof. Ibrahim Lipumba (CUF)
Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ameonyesha kuridhika kwao na maandalizi ya mwaka huu akieleza kuwa:
“Kupata daftari la kudumu la wapiga kura kwa wakati kumeongeza ufanisi katika maandalizi yetu ya kampeni. Tunaamini mazingira ya uchaguzi wa haki yanawezekana.”
Prof. Lipumba aliongeza kuwa kwa uchaguzi huu, CUF imeweza kufanya maandalizi ya kina ikiwemo mapitio ya Ilani, mafunzo ya maadili, mikakati ya kampeni, na kuanzisha vikosi kazi vya kitaifa hadi mikoa kusimamia maandalizi hayo.
“Tumejifunza kutokana na tofauti za chaguzi zilizopita, na mwaka huu tunaona uwazi wa hali ya juu unaotupa uhuru wa kujiandaa na kushiriki kikamilifu,” alisema.
Pia, alisisitiza umuhimu wa uwazi zaidi, ushirikishwaji mpana wa wadau na uhakiki wa daftari la wapiga kura kuhakikisha kila raia mwenye sifa anapata nafasi ya kushiriki.
ADA-TADEA: Wanawake na Vijana Wajitokeza Viongozi
Juma Ally Khatib, Mwenyekiti wa ADA-TADEA, amepongeza juhudi za Tume ya Uchaguzi na vyama vya siasa katika kuhakikisha ushiriki wa wanawake na vijana kwa njia za vitendo.
“Tunaendelea kuweka vipaumbele vya wazi vya ushiriki wa wanawake na vijana, si kama mapambo, bali kama nguvu ya mabadiliko na maendeleo,” alisema.
ADA-TADEA imeanzisha mikakati ya kuwawezesha wanawake na vijana kugombea majimbo ya wazi, kutoa mafunzo ya uongozi na kuandaa makongamano ya hamasa.
INEC Yajipanga Kukamilisha Uchaguzi kwa Uwazi
Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, amethibitisha kuwa mabadiliko ya majimbo yamezingatia takwimu rasmi za idadi ya watu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na maoni ya wadau wa uchaguzi.
“Tumepokea maoni mbalimbali na kuongeza kata tano mpya, kufanya jumla ya kata 3,960 kwa Tanzania Bara. Hii inalenga kuboresha uwakilishi wa wananchi,” alisema.
Ameeleza kuwa kalenda ya uchaguzi imeanza rasmi, ambapo utoaji wa fomu kwa wagombea utaanza Agosti 9 hadi 27, na kampeni kuanza Agosti 28 hadi Oktoba 27.
Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa kila hatua ya maandalizi imekuwa ikifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha vyama vya siasa, kuhakikisha uchaguzi wa haki na kuaminika.
Saluti ya Upinzani, Ishara ya Ukomavu wa Demokrasia
Hatua ya vyama vya upinzani kuipigia saluti Tume Huru ni ishara ya mabadiliko chanya katika siasa za Tanzania, ikionyesha ukomavu wa kisiasa na kuongezeka kwa uaminifu katika mfumo wa uchaguzi.
Wataalam wa siasa wanasisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika elimu ya wapiga kura, amani ya kitaifa, na ushirikiano wa kisiasa ili kufanikisha uchaguzi unaoleta maendeleo.
Makala haya yameandaliwa na Victor Bariety -0757-856284








No comments:
Post a Comment