Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliofanyika kwa njia ya Mtandao katika ukumbi wa mkutano wa NEC (White House) Makao Makuu ya CCM, Jijini Dodoma jana Julai 26 , 2025. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mkutano huo Mkuu kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao na kuwakutanisha Wajumbe wote wa mkutano huo kutoka nchini.
.........................................
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikifanya mabadiliko
madogo katika katiba yake yameibuka mawazo tofauti yakielezea kuwa ni mazuri
huku wengine wakisema bado yanatakiwa kuboreshwa
zaidi.
Chama hicho jana kilifanya mkutano maalumu chini ya
Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Samia Suluhu Hassan na kufanya marekebisho madogo katika eneo la uchaguaji
idadi ya wagombea nafasi ya udiwani, ubunge na Baraza la Uwakilishi.
Katika katiba ya awali idadi ya wagombea ilikuwa ni watatu
lakini baada ya mabadiliko hayo madogo idadi hiyo imeongezwa baada ya wajumbe
wa mkutano huo kuridhia ongezeko hilo kwa kupiga kura.
Awali Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Samia alisema “ Mkutano
wetu leo utakuwa na ajenda moja tu yakufanya marekebisho madogo sana kwenye
katiba yetu ya Chama Cha Mapinduzi, hatukuweza kamati kuu kujipa mamlaka ya
kufanya kazi ambayo tunaomba mturuhusu bila ya kurudi kwenu kwa sababu hiki
chama ni cha wana CCM si cha kamati kuu peke yake,”. alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa wameamua kurudi kwao kupitia mkutano huo wa
dharura ili kupata ruhusa yao ya kufanya marekebisho madogo katiba yao.
Dkt. Samia alisema wamefikia hatua hiyo baada ya chama hicho
kutanua demokrasia katika kuchagua viongozi ngazi ya taifa, jimbo na kata na
ngazi za madiwani jambo ambalo limewavutia wana CCM wengi sana kuomba kugombea
ambapo kuna maeneo yana wagombea wengi hadi 39 na 40.
Alisema hivyo kwenda na watu watatu kati ya watu wengi hao lisingekuwa
jambo la busara lakini wakati huo huo kamati kuu imebanwa na katiba kutoongeza
majina ndio maana wakaamua kurudi kwa wajumbe kuomba ridhaa ya kubadilisha
katiba ili kuongeza idadi ya wagombea kama kamati kuu itakavyoona inafaa.
“Tumeamua kurudi kwenu jambo letu ni kuomba kuongeza idadi
ya wagombea wafike wanne, watano kadri tutakavyoona inafaa kutokana na idadi ya
wingi wa watu walioomba kwenye jimbo husika,” alisema.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo Dkt. Samia aliomba wajumbe wa
mkutano mkuu huo wapige kura kutoka maeneo waliyopo kote nchini kura ambazo zilitakiwa
zifike theluthi mbili kama katiba inavyoelekeza ili kujua wangapi wamekubali na
kukataa.
Mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Kibaha, Subira Mgalu
alipongeza hatua ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa na wajumbe wake wa kamati
kuu kwa hatua ya kufanya mkutano huo kwa njia ya mtandao na kueleza kuwa CCM ya
leo ipo kwenye mapinduzi makubwa ya maendeleo na Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kama dunia inavyokwenda.
“Kufanya mkutano huu kwa njia ya mtandao imesaidia kuokoa
fedha nyingi ambazo zitakwenda kufanya shughuli nyingine za chama, binafsi
nimeshiriki mkutano huu nikiwa na wenzangu hapa Kibaha hakika chama chetu chini
ya Rais Samia kimekuwa cha kisasa zaidi,” alisema Mgalu.
Alisema Rais Samia ni mama wa demokrasia kufanya mkutano huo
kwa lengo la kubadilisha katiba na kuongeza idadi ya wagombea
wanaotakiwa kuteuliwa kutoka watatu hadi zaidi ni ukukomavu wa kiongozi ambaye
hana ubaguzi hivyo kila mwana CCM anapaswa kumpongeza.
Mhandisi Felix Dagaki mgombea ubunge Jimbo la Itigi mkoani
Singida alipongeza wajumbe wa mkutano mkuu kuridhia ombi la kamati kuu la
kuongeza wagombea wa nafasi za ubunge, ujumbe wa baraza la wawakilishi na
udiwani ili kwenda kupigiwa kura za maoni.
“ Ni jambo kubwa mno lililofanywa na Mwenyekiti wa chama
chetu Taifa kutokana za uzalendo alionao kwa Watanzania kwani sasa kumekuwa na
uchangamfu kwa wagombea wa nafasi hizo ambao wengi wao walikata tamaa hata ya
kuingia nafasi ya tatu bora kutokana na wingi wa waliomba kugombea,” alisema
Dagaki.
Dagaki aliomba chama hicho kifanye maboresho zaidi kwenye
katiba yake badala ya kuwachagua baadhi ya wagombea ili kufanyiwa uteuzi wa
kugombea, kipengele hicho kibadilishwe na iwe kwa kila mwana CCM aliyegombea
hata wakiwa zaidi ya 30 waingizwe kwenye zoezi la kupigiwa kura za maoni katika
maeneo yao.
Alisema kura za maoni za wananchi ambao wanawajua wagombea
hao ndizo zitakazowachuja na hivyo kupunguza malalamiko ambayo yangeweza
kutokea ukizingatia kuwa watia nia hao wanakuwa wamelenga kuwatumikia wananchi huku
wakichukua fomu kwa gharama kubwa hivyo kuwaondoa mapema ni kama kuwanyima haki
yao.
Naye Shahibu Selemani Mgombea Udiwani Kata ya
Ligoma Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma anasema Rais Samia ni mama wa ukweli na
mama wa demokrasia ambaye anawapenda wananchi wake.
“ Hatua hii
ya kuongeza idadi ya wagombea ili wateuliwe na kupigiwa kura za maoni ni
dhamira nzuri ya Dkt. Samia ya kutaka kuwapata viongozi makini watakaowatumikia wananchi kwa uzalendo
mkubwa,” alisema Selemani.
Mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Nungwi
Zanzibar, Hussein Ramadhan Layya, maarufu kwa jina la Msokolo, anasema hatua
hiyo ya kuongeza idadi ya wanaoteuliwa ili kupigiwa kura za maoni ni nzuri
lakini itakuwa ni vizuri zaidi kamati kuu ikiweka bayana idadi rasmi ya
wagombea itakayowapitisha badala ya kueleza tu kuwa itaona yenyewe kulingana na
idadi ya wagombea katika eneo husika.
“Kamati kuu iweke kikomo cha wagombea watakao
wachagua kama ni 10 au 15 ili kwenda kupigiwa kura ya maoni na isiishie kusema
itaangalia yenyewe jambo ambalo litasaidia kuondoa mashaka ya kuwapendekeza
watu ambao pengine watakuwa na maslahi na baadhi yao.
Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana, Mhandisi Kwilasa
Ntare amesema hatua hiyo ya kuongeza wagombea imeleta matumaini makubwa kwa
wagombea tofauti na ile idadi ya watu watatu.
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya Suma
Fyandomo alisema Mungu ameipendelea Tanzania kwa kuipa Rais mwenye hofu na
mapenzi kwa wananchi wake kwani kitendo cha kuongeza idadi ya wagombea
watakaoteuliwa ili kupigiwa kura za maoni kwenye uchaguzi mkuu anaonesha ni
jinsi gani alivyo kiongozi bora.
“Mwenyekiti wetu nimuite tu kuwa ni jembe la
watanzania kwani kila eneo ameimarika iwe kwenye serikali mambo yana kwenda
vizuri na kwenye chama ndiyo sisemi kabisa Mungu ampe afya na maisha marefu
aweze kutufikisha kwenye nchi yenye asali, maziwa na neema kubwa,” alisema Fyandomo.
Katika mkutano mkuu huo ulioendeshwa kwa njia ya mtandao
ambao ulikuwa na ajenda kuu moja ya kufanya marekebisho madogo katika katiba ya
chama hicho yalipitishwa kwa asilimia 99.8.
Kura za wazi zilipigwa katika mkutano huo kwa Wajumbe
waliopo katika wilaya na mikoa na Rais Dkt. Samia akiwa katika Ukumbi wa NEC -
Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma ambapo kati ya wajumbe wa mkutano huo 1,931
waliohudhuria ni 1,915 na 16 walikuwa na hudhuru huku kura za ndio zikiwa 1,912
na zilizoharibika zikiwa 3 hivyo kufanya jumla ya kura za ndio kuwa ni sawa
na asilimia 99.8 na kupitisha mabadiliko
hayo.
Akihitimisha mkutano huo Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dkt.
Samia Suluhu Hassan alisema vijana wengi wanatarajiwa kupewa nafasi kubwa
katika nafasi za ubunge, udiwani na baraza la uwakilishi.
Makala haya yameandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754362990)
Wajumbe wakibadilishana mawazo kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo.
Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
Taswira ya mkutano huo.
Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo aliyetoa maoni yake kuhusu mabadiliko madogo ya katiba yaliyofanywa.Mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Nungwi Zanzibar, Hussein Ramadhan Layya, maarufu kwa jina la Msokolo, aliytoa maoni yake kuhusu marekebisho ya katiba.
Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana, Mhandisi Kwilasa NtareMhandisi Felix Dagaki mgombea ubunge wa Jimbo la Itigi mkoani Singida , ambaye ametoa maoni yake.
Mgombea Ubunge Jimbo la Kibaha, Subira Mgalu ambaye ametoa maoni yake.
Shahibu Selemani Mgombea Udiwani Kata ya Ligoma Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambaye ametoa maoni yake.





















No comments:
Post a Comment