MAADHIMISHO WIKI YA TIBA ASILI KITAIFA – MAMIA YA WATAALAMU WATUA DODOMA

Subscribe Us

MAADHIMISHO WIKI YA TIBA ASILI KITAIFA – MAMIA YA WATAALAMU WATUA DODOMA

Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili, yanayofanyika kuanzia Agosti 25 hadi 31 kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma yakiendelea.

.........................................

Na Godwin Myovela – Dodoma

Mamia ya wataalamu, wabunifu, wazalishaji na wanasayansi wa tiba asili wamewasili jijini Dodoma tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi katika maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili, yanayofanyika kuanzia Agosti 25 hadi 31 kwenye viwanja vya Chinangali.

Maadhimisho hayo yanabebwa na kauli mbiu: “Tuimarishe Huduma za Tiba Asili zenye Ushahidi wa Kisayansi.”

Tukio hilo limeandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Idara ya Tiba, kwa kushirikisha wataalamu wa tiba asili kutoka pembe zote za nchi, lengo ni kutoa elimu, kushiriki tafiti, kuonyesha ubunifu mpya na kutoa huduma mbadala za kiafya.

Mgeni Rasmi wa maadhimisho haya anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

Akizungumza jana jijini hapa, Mratibu wa maonesho hayo, Bw. Musa Lipukuta kutoka Idara ya Tiba Wizara ya Afya, alisema serikali imejipanga kuhakikisha huduma zote na bidhaa zinazotolewa zinatekelezwa kwa kuzingatia sera, miongozo na sheria ya Baraza la Tiba Asili namba 23 ya mwaka 2002.

“Tunataka wananchi waamini tiba asili kwa sababu tunazisimamia kitaalamu na kisheria, huku tukishirikiana na taasisi za utafiti kuhakikisha zina ubora na usalama wa kutosha,” alisema Lipukuta.

Kwa sasa, huduma jumuishi za dawa aina 26 za tiba asili kwa magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza zinapatikana katika hospitali za kisasa katika jumla ya mikoa 14, ikiwemo Tanga, Morogoro, Dodoma na Temeke.

Mgonjwa anapofika hospitalini ana uhuru wa kuchagua tiba ya kisasa au tiba asili, huku Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ikihusika moja kwa moja kukusanya na kusambaza dawa hizo katika vituo husika.

Lipukuta alisema hatua hiyo ni mwelekeo muhimu wa Tanzania kuelekea kuwa na tiba yake ya kipekee ya asili kama ilivyo kwa mataifa mengine duniani. 

Alibainisha kwamba chanzo kikuu cha dawa hizo ni mimea, madini, mabaki ya wanyama na mazao ya baharini, hivyo ipo haja ya watoa huduma wa tiba asili kuanzisha mashamba ya miti dawa ili kurahisisha upatikanaji wa malighafi.

“Kwa kuzingatia umuhimu huu, serikali ipo mbioni kuanzisha Hospitali ya Tiba Asili, itakayokuwa kituo cha matibabu, utafiti, mafunzo na tiba utalii,” alifafanua Lipukuta.

Maonesho ya mwaka huu yamevutia takribani mabanda 50, ambayo yanatoa huduma za kitaalamu kutoka mikoa mbalimbali, huku wananchi wakipata fursa ya kutembelea na kupata vionjo mbalimbali kama chai za mitishamba, ushauri wa kiafya na kushuhudia teknolojia mpya za uchakataji wa dawa.

Aidha, Baraza la Tiba Asili la Taifa linaendesha zoezi maalum la kusajili waganga wa tiba asili na vituo vya tiba ambavyo bado havijakamilisha taratibu, ili kuhakikisha huduma zote zinatolewa kwa mujibu wa miongozo ya kitaalamu na kwa usalama wa wananchi.

Akizungumzia ubunifu wa mwaka huu, Lipukuta alisema kuna ongezeko kubwa la washiriki walioboresha bidhaa na mbinu za utoaji huduma ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Safari hii tumesisitiza ubora, usajili wa bidhaa, na namna bora ya kuwasilisha bidhaa kwa wananchi. Hii imeongeza mvuto na imani ya jamii,” alisema.

Hata hivyo, kuelekea kilele cha maadhimisho kutakuwa na Mkutano wa Kisayansi wa Tiba Asili (Scientific AGM) unaotarajiwa kufanyika Agosti 29, ambapo tafiti mpya, changamoto na mwelekeo wa tiba asili kitaifa vitajadiliwa na wataalamu.

“Scientific AGM itakuwa chachu ya kuunganisha utafiti na vitendo. Ni hatua kubwa ya kuhakikisha tiba asili inapata heshima na nafasi inayostahili katika sekta ya afya," alihitimisha Bw. Lipukuta.









 

Post a Comment

0 Comments