MUHAS YAZINDUA PROGRAMU YA DIPLOMA YA TIBA ASILI

Subscribe Us

MUHAS YAZINDUA PROGRAMU YA DIPLOMA YA TIBA ASILI

Mhadhiri na mtafiti kutoka Taasisi ya Dawa Asili ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt.Mourice Mbunde, akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo,

............................

Na Godwin Myovela-Dodoma 

Taasisi ya Dawa Asili ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) imeandika ukurasa mpya katika historia ya tiba nchini kwa kuzindua rasmi programu ya kwanza ya kitaaluma ya stashahada ya tiba asili. 

Hatua hii imejidhihirisha katika Maadhimisho ya Wiki ya Tiba Asili Kitaifa yanayoratibiwa na Wizara ya Afya kupitia Idara ya Tiba, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia Agosti 25–31, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.

Ujio huu umeweka matumaini mapya ya kuinua kiwango cha elimu, tafiti na ubunifu wa tiba asili yenye ushahidi wa kisayansi, huku MUHAS ikijivunia pia bidhaa kadhaa zilizosajiliwa kama zao la maboresho ya afya kwa wananchi. 

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo, Dk. Mourice Mbunde, mhadhiri na mtafiti kutoka Taasisi ya Dawa Asili ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), alisema taasisi hiyo imekuja kipekee kuonesha mafanikio ya tafiti zao ambazo tayari zimezalisha bidhaa kadhaa zinazosaidia kudhibiti magonjwa mbalimbali.

“Tumekuja kama taasisi kuonesha kazi za tafiti zetu ambazo zimesaidia kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya kudhibiti maradhi mbalimbali. Lakini mwaka huu tunajivunia zaidi kwani tumekuja pia na mwelekeo mpya wa mafunzo rasmi kwa wadau wa tiba asili nchini,” alisema Dk. Mbunde.

Kwa mara ya kwanza nchini, MUHAS imeanzisha programu ya mafunzo rasmi ya stashahada (diploma) ya tiba asili, hatua ambayo imeelezwa kuwa ya kihistoria katika kuinua viwango vya taaluma hiyo.

“Kupitia programu hii, tunawaalika wale wote waliomaliza kidato cha nne au cha sita na kusoma masomo ya sayansi, kujiunga ili wajifunze namna bora ya kutengeneza dawa za asili, kuziboresha, na kuhakikisha zinafikia viwango vya kitaifa na kimataifa,” alifafanua.

Mbali na diploma, MUHAS pia imezindua mafunzo ya muda mfupi ya wiki moja kwa wadau wa tiba asili ambao hawana nafasi ya kusoma kwa muda mrefu. Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ubora na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. 

Taasisi hiyo imeeleza kujivunia mafanikio makubwa ya tafiti zake, ambapo baadhi ya bidhaa zimesajiliwa na sasa zinapatikana sokoni na madukani, zikisaidia watu katika kulinda na kuboresha afya zao.

“Tunapofika kwenye maonesho kama haya tunafurahi sana kuona baadhi ya wanafunzi tuliowapa mafunzo ya muda mfupi, sasa wakifanya kazi kwa ubora na ufanisi mkubwa, wakitoa huduma bora kwa Watanzania kupitia tiba asili,” alisisitiza Dk. Mbunde.

Alisema ni nafasi ya kipekee kwa wananchi wote, wataalamu wa afya, wanafunzi na wadau wa tiba asili, kufika kwenye viwanja vya Chinangali Park kushuhudia, kujifunza na kupata elimu ya moja kwa moja kutoka kwa watafiti na taasisi zinazohusika na tiba asili nchini.

“Tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi, si tu kuona bidhaa, bali pia kujifunza namna tiba asili inavyoboreshwa kitaalamu na kisayansi ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya kwa afya ya kila Mtanzania,” alisema

Wiki ya Tiba Asili Kitaifa imeendelea kuwa jukwaa la kipekee la kutangaza matokeo ya tafiti, kutoa elimu, kushirikisha jamii na kuongeza uelewa kuhusu tiba asili inayotegemea ushahidi wa kisayansi.

Wananchi wote wanakaribishwa kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho haya makubwa ya kitaifa, ambayo yanahimiza afya, ujuzi, na ubunifu wa Kitanzania kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mmoja wa wananchi ikisoma kipeperushi alipotembelea banda la MUHAS.
Dkt.Mourice Mbunde, akizungumza na mmoja wa wananchi aliyetembelea banda lao kwenye maonesho hayo.
 

Post a Comment

0 Comments