Na Godwin Myovela, Dodoma
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, Profesa Joseph Otieno, amewasha moto wa hamasa akiwataka Watanzania kurejea katika misingi ya tiba na vyakula vya asili ili kuimarisha kinga za miili yao dhidi ya mlipuko wa magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambako maonesho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanaendelea hadi Agosti 31 chini ya kauli mbiu “Tuimarishe Huduma za Tiba Asili zenye Ushahidi wa Kisayansi”, Prof. Otieno alisema magonjwa yasiyoambukiza siyo hatima, bali ni matokeo ya mabadiliko mabaya ya kimaisha na ulaji hovyo wa vyakula visivyo vya asili.
“Magonjwa haya tumeyaleta sisi wenyewe, si kwamba yametufuata. Tulipotupa mbogamboga na vyakula vyetu vya asili tukakimbilia vile vilivyotoka nje, tulipoteza viambata vya asili vinavyopambana na maradhi. Hivyo sasa imetufikisha kwenye hatari kubwa kiafya,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Prof. Otieno, tiba asili na vyakula vya kienyeji siyo tu dawa, bali pia ni kinga ya mwili wa mwanadamu. Alisema mimea na mboga za asili zimekuwa zikihakikisha uimara wa miili tangu enzi za mababu, na sasa ni wakati wa kizazi kipya kuvirejesha kwenye mlo wa kila siku.
Alitoa mifano ya mimea tiba na mboga zinazotumika pia kama chakula, ikiwemo mgagani, ambazo huchangia kutibu na kudhibiti magonjwa sugu.
“Tiba asili kwa kiasi kikubwa ni chakula. Wataalamu wanachukua majani, wanayaponda, kuyafungasha, na tunauza—lakini kiuhalisia ni chakula ambacho ndani yake kimebeba dawa. Ukiweka kwenye uji, ugali, maziwa au mboga, unajikuta unatibika bila hata kujua,” alisema kwa msisitizo.
Prof. Otieno aliwaalika wakazi wa Dodoma na mikoa jirani kufika Chinangali Park kushuhudia na kujipatia dawa na vyakula vya asili vinavyotibu na kulinda afya, akisisitiza kuwa hatua hii ni zaidi ya tiba—ni mapinduzi ya kiafya na kurudi kwenye mizizi ya mwafrika.
Profesa Joseph Otieno akizungumza na viongozi mbalimbali katika maonesho hayo.Ukaguzi wa bidhaa hizo ukiendelea.
Mahojiano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yakifanyika
Ukaguzi wa bidhaa hizo ukiendelea
0 Comments