Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza jana Septemba 3, 2025 katika Kongamano la Nne la Madereva wa Serikali lililofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini , Dodoma.
..................................
Na Godwin Myovela Dodoma
Katika hotuba yake yenye msisitizo na uzito wa kitaifa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka madereva wa serikali kote nchini kuenzi wajibu wao wa kipekee wa kutunza siri za viongozi na serikali, huku akisisitiza kwamba nafasi yao ni zaidi ya kuendesha magari.
Akizungumza Septemba 3 mwaka huu, katika Kongamano la Nne la Madereva wa Serikali lililofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma, Majaliwa alisema madereva ni kiungo cha karibu sana na viongozi, hivyo hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kulinda heshima na taswira ya serikali.
“Nyie ni watu muhimu sana. Kwa umuhimu huu, mtambue kuwa nyie ndiyo mnapaswa kuwa nambari moja katika kutunza siri za serikali na viongozi mnaowaendesha,” alisema.
Alifafanua kuwa siri wanazoshuhudia kazini – ikiwemo maongezi ya simu au mijadala ya faragha – ni jambo linalopaswa kuzikwa mioyoni mwao kwa uadilifu, kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
Mbali na suala la siri, Waziri Mkuu aliwataka madereva wa serikali kuongeza weledi wao katika nyanja nyingine muhimu ikiwemo usafi wa mavazi na kielelezo cha nidhamu ya muonekano kazini.
Aliwakumbusha umuhimu wa ukaguzi wa magari huku akisisitiza kabla ya safari yoyote, gari lazima likaguliwe kwa kina ili kuepuka hatari.
Sambamba na hilo alihimiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu sahihi kwa maana ya kila safari iwe na rejista iliyojazwa ipasavyo kwa uwazi na uwajibikaji.
Huku akionyesha msisitizo wa aina yake aliwataka madereva wote kuwa waaminifu kwenye masuala ya kitaalamu kwa kuepuka kuendesha magari yenye viashiria vya hitilafu.
“Mwambie mwajiri huwezi kuendesha gari kwa sababu linahitaji ukarabati wa lazima,” alisisitiza Majaliwa.
Aidha, aliwakumbusha kuacha matumizi ya namba feki, ving’ora visivyo halali, na vilevi, huku akihimiza utii wa sheria za barabarani.
“Mara nyingi mmekuwa mkilalamikiwa na wadau kwa kuendesha kwa kasi hata katika maeneo yenye kiwango cha mwendo kilichodhibitiwa. Acheni tabia hiyo,” alisema.
Kongamano hilo liliambatana na kaulimbiu:“Dereva wa Serikali, Epuka Ajali, Linda Gari Lako na Watumiaji Wengine wa Barabara. Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.”
Kwa msisitizo huo, Waziri Mkuu Majaliwa alihitimisha kwa kuwataka madereva wajitambue kama nguzo ya taifa, akisema;
“Dereva wa serikali si dereva pekee. Ni mhimili wa heshima na usiri wa taifa.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati akiwasili kufungua kongamano hilo.Madereva wa Serikali wakiwa kwenye kongamano hilo.
0 Comments