TAKUKURU MKOA WA TANGA KUWABANA WAGOMBEA UONGOZI UCHAGUZI MKUU 2025

Subscribe Us

TAKUKURU MKOA WA TANGA KUWABANA WAGOMBEA UONGOZI UCHAGUZI MKUU 2025

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah, akizungumza ofisini kwake jana mkoani humo.

...............................................

Na Mashaka Kibaya, Tanga

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa imewataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona mienendo isiyofaa kwa wagombea wa uongozi ili hatua madhubuti kuchukuliwa lengo likiwa kudhibiti mapema athari za vitendo hivyo katika uchaguzi.

Katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika jana ofisini kwake akiwasilisha taarifa kwa umma, Kamanda wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoani Tanga, Ramadhani Ndwatah, aliwasihi wananchi kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa lengo la kudhibiti mapema vitendo vya rushwa.

"Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga kutoa taarifa TAKUKURU pale unapoona mienendo isiyofaa kwa wagombea ili zichukuliwe hatua madhubuti na kudhibiti mapema athari za vitendo hivyo katika uchaguzi" alisema Ndwatah.

Kuhusu mafanikio katika utendaji kazi wa TAKUKURU mkoani Tanga kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Ndwatah alisema, Shilingi 10,500,000 zimeokolewa kutokana na ufuatiliaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TAKUKURU katika kuzuia vitendo vya rushwa ambapo wamekuwa wakifuatilia miradi ya maendeleo ili kuweza kutekelezwa kwa ufanisi na kufikia malengo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupeleka miradi hiyo kwa wananchi.

Ndwatah alisema, katika utekelezaji jukumu hilo TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 29 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 7,997,662,950.00 katika sekta za barabara na elimu.

Aidha taasisi hiyo ilibaini Tsh 475,000,000 zilitolewa na halmashauri ya wilaya ya Muheza kupitia fedha za mfuko wa barabara (Road Fund) kujenga barabara kiwango cha lami yenye urefu wa mita 830 ambapo ilibainika kuwa barabara hiyo ilitakiwa kuwa na nguzo za taa za umeme wa jua 29 badala yake ziliwekwa nguzo na taa 26.

Kutokana na hali hiyo taasisi hiyo ilichukua hatua kwa kuwasiliana na ofisi ya TARURA wilaya kuwaeleza mapungufu yaliyobainika ambapo maboresho na marekebisho yametekelezwa kwa kuwekwa nguzo na taa zake tatu zenye thamani ya Shilingi 10,500,000.00.

Kwa mujibu wa Ndwata,miradi mingine 10 yenye thamani ya Tsh 2,869,191,631.00 ilibainika kuwa na mapungufu kama vile kutekelezwa bila malipo ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), miradi kutozingatia michoro na ramani na miradi kutekelezwa kwa muda mrefu zaidi ya muda wa mikataba.

Pia kulikuwa na changamoto ya kitabu cha kutoa na kupokea Vifaa (issue voucher) kutojazwa kwa wakati ambapo kutokana na mapungufu hayo hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuyarekebisha ikiwemo kuzijulisha mamlaka husika.

Ndwatah alieleza kuwa elimu kwa umma imeendelea kutolewa ili kufikia idadi kubwa ya watakaowania na kuongeza ushiriki wao katika mapambano dhidi ya rushwa.

Amesema kwamba, makundi mbalimbali yamepewa elimu zikiendeshwa semina 60, uimarishaji klabu 73 za wapinga rushwa, kufanyika kwa mikutano ya hadhara 57, maonesho 15, makala 14 na vipindi vya redio 15.

Ameongoza kuwa,elimu kwa umma imeongeza ushiriki mkubwa wa wadau katika kampeni za uzuiaji rushwa,wananchi walio wengi wameonyesha uzalendo wa kweli katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na Wananchi kuonyesha utayari kushiriki kampeni za uzuiaji rushwa kwa kushiriki kwenye vikao na mikutano inayoandaliwa na TAKUKURU. 

Vile vile utekelezaji wa programu ya TAKUKURU Rafiki umeendelea ambapo wananchi wamenufaika na utatuzi wa kero katika maeneo ya kutolea huduma iwenye sekta za afya, elimu, maendeleo ya jamii, kilimo, utawala na miundombu.

Katika mikakati ya kuzuia rushwa kipindi cha julai - septemba 2025, TAKUKURU itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo, kuendelea kutoka elimu kwa Wananchi na kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya programu ya TAKUKURU - Rafiki.

Taarifa ikitolewa kwa waandishi wa habari.
 

Post a Comment

0 Comments