WATUMISHI WALIOGOMBEA UBUNGE, UDIWANI WAMWANGUKIA KATIBU MKUU KIONGOZI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, 27 September 2025

WATUMISHI WALIOGOMBEA UBUNGE, UDIWANI WAMWANGUKIA KATIBU MKUU KIONGOZI

Mikutano ya kampeni ikiendelea

...........................

Na Mwandishi Wetu

Katika historia ya utumishi wa umma nchini Tanzania, daima kumewekwa mizani ya kisheria inayolenga kulinda hadhi na haki za mtumishi. 

Moja ya mizani hiyo ni Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namba 1 wa mwaka 2015, unaoweka bayana taratibu kwa watumishi wa umma wanaotaka kugombea nyadhifa za kisiasa. 

Waraka huu unatoa fursa kwa mtumishi kushiriki siasa bila kupoteza haki yake ya msingi ya ajira.

Kwa mujibu wa waraka huo, endapo mtumishi hatapitishwa na Tume ya Uchaguzi au chama chake, anatakiwa kurejea mara moja kazini. 

Hii si fadhila ya mwajiri, bali ni haki ya msingi ya mtumishi. Hata hivyo, hali ya sasa imegeuka kuwa kinyume chake. 

Mamia ya watumishi waliogombea nafasi za udiwani na ubunge, baada ya kushindwa kupitishwa, wamesalia mitaani—wamezuiwa mishahara yao, bima zao za afya zimesitishwa, na vibali vya kurejea kazini havijatolewa.

Kwa mtazamo wa uadilifu wa kisheria na utu, hali hii inatia doa kubwa. Kwanza, ni uvunjaji wa waraka ulio wazi na unaotakiwa kutekelezwa bila masharti ya muda. 

Pili, ni kupuuza dhana ya haki za kijamii kwa mtumishi na familia yake, ambao sasa wameingia kwenye mateso ya kifedha, kiafya na kisaikolojia.

Ni muhimu tukiri ukweli; siyo kosa kwa mtumishi wa umma kutumia haki yake ya kikatiba kugombea nafasi ya uongozi. Ni dhihirisho la ukomavu wa demokrasia na ushiriki wa wananchi katika kujenga taifa.

Lakini ni kosa kubwa, kimaadili na kisheria, kumwacha mtumishi huyo akiteseka kwa sababu tu hakupitishwa na chama au tume.

Kuchelewesha vibali hadi baada ya uchaguzi ni hoja isiyo na msingi wowote wa kisheria. Haki haiwezi kusubiri matokeo ya kisiasa. Haki inapaswa kutolewa pale inapostahili. Na katika mazingira haya, haki ya mtumishi kurudi kazini ni ya haraka.

Athari za hali hii hazipo tu katika ngazi ya kifamilia. Zinaweza pia kuathiri morali ya kikazi na taswira ya utumishi wa umma nchini. 

Watumishi wanaweza kuona mfumo ni wa kibaguzi na usio na usawa, hali inayoweza kupunguza hamasa na ari ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Tunapozungumzia ajira za umma kama mhimili wa maendeleo, hatuwezi kuacha kundi hili likiendelea kuumizwa kimya kimya. 

Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kwa mageuzi makubwa katika sekta ya ajira na huduma za kijamii. Hii ndiyo nafasi sahihi ya kuthibitisha msimamo wake kwa kuhakikisha watumishi hawa wanarejeshwa kazini haraka.

Ni wakati wa Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Utumishi wa Umma kusimama imara na kusimamia utekelezaji wa waraka huu. 

Maamuzi ya haraka yatakuwa si tu kurejesha haki, bali pia kujenga imani kwa umma kwamba mifumo ya kisheria na kiutumishi inafanya kazi bila upendeleo.

Ni wakati sasa wa mamlaka inayohusika kuwarudisha kazini wote waliokosa uteuzi wa kisiasa kwa mujibu wa Waraka wa 2015.

Pia kuhakikisha wanarejesha mishahara na bima zao kuanzia mwezi walipositishwa ili kuondoa athari walizoingia bila sababu ya msingi.

Sambamba na kutoa tamko rasmi la serikali ili kuondoa mkanganyiko na tetesi mitaani kwamba vibali vitatolewa baada ya uchaguzi, jambo lisilo na msingi wa kisheria.

Kwa kufanya hivyo, serikali haitakuwa tu imewarejeshea matumaini watumishi hawa, bali pia itakuwa imedhihirisha uongozi wa haki, usawa na utu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad