MISUGHAA SPORT CENTRE CHAONESHA TIJA SINGIDA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 5 October 2025

MISUGHAA SPORT CENTRE CHAONESHA TIJA SINGIDA

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Jackson Maruma akizungumza katika mahafali ya 16 ya kidato cha nne yaliyofanyika Oktoba 2, 2025.

.................................

Dotto Mwaibale na Philemon Solomoni, Singida

KITUO cha kuibua vipaji vya mpira wa miguu kinachojulikana kwa jina la Misughaa Sport Centre kilichoanzishwa Shule ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kimeanza kuonesha tija.

Mkuu wa shule hiyo Jackson Maruma akizungumza wakati akitoa taarifa ya shule hiyo kwenye mahafali ya 16 ya kidato cha nne yaliyofanyika Oktoba 2, 2025 alisema kituo hicho kimeanza kuonesha tija.

Alisema kituo hicho kimepata usajili namba  S13011 Misughaa Sports Centre chenye malengo ya kuinua na kutengeneza vipaji vitakavyo tumika mashuleni na Taifa kwa ujumla.

“Ajenda yetu kubwa ni kuhakikisha wanafunzi wetu hapa shuleni hawajihusishi tu kwa masuala ya taaluma madarasani bali ni pamoja na  mambo ya vipaji mbalimbali ambavyo Mungu amewapatia,” alisema Maruma.

Alisema dunia ya sasa mtu anaweza kufanikiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya vipaji vya aina tofautitofauti kama muziki, kuigiza, michezo na vingine vyote vyenye maslahi mapana kwa Taifa letu.

 Mwalimu wa michezo wa shule hiyo Protasi Hema alisema shule hiyo ilionesha kuwa na watoto wenye vipaji ambapo alipeleka wazo hilo kwa mkuu wa shule hiyo Maruma ambaye alitoa baraka zote za kuanzishwa kwa kituo hicho.

Hema alisema kituo hicho kilianza mwaka 2018 ambapo usajili wake waliupata mwaka 2022.

“Kituo hiki kinachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali lakini wengi wanatoka hapa Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein,” alisema Hema.

Alisema wamekuwa wakiwapa majaribio ya aina mbalimbali ya kuibua vipaji vya wanafunzi hao ambapo baadhi yao waliwapeleka timu ya Azam ijini Dar es Salaam na Mbeya ambao wameonesha kufanya vizuri.

Mwalimu Hema alisema kituo hicho kinaendeshwa na shule lakini msaada mkubwa unatoka  kwa wazazi ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kusaidia kituo hicho ambacho ni muhimu katika kukuza vipaji vya watoto.

Aidha, Hema alisema wanapo safiri kwenda mikoa mingine wamekuwa wakisaidiwa na wadau mbalimbali na kueleza kuwa tangu kianzishwe kituo hicho wamesafiri mara nne.

“Kwetu ni mafanikio makubwa na yenye tija na ni hatua nzuri tunaomba wadau mbalimbali watushike mkono kwani mahitaji ya kituo chetu ni makubwa mno changamoto tuliyonayo ni fedha za kukiendesha,” alisema.

Kiongozi wa wanafunzi hao, Haruna Said akizungumza kwa niaba ya wenzake aliushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kuanzisha kituo hicho ambacho kinawaandaa vizuri kimechezo.

“Tuna mshukuru sana mkuu wa shule yetu Mwalimu Maruma kwa kuanzisha kituo hiki tumeweza kusafiri kwenda Mbeya na Dar es Salaam kujipima na timu kubwa kwetu ni fursa kubwa,” alisema.

Said aliwaomba wazazi na wadau mbalimbali kuendelea kuwaunga mkono kwa hali na mali ili waweze kufika mbali kimichezo na kuwa wachezaji wa kitaifa na kimataifa.

Mwalimu wa Michezo wa shule hiyo, Protas Hema akizungumzia maendeleo ya kituo cha michezo kilichopo katika shule hiyo.
Wazazi wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wanafunzi wanaofunzwa vipaji vya michezo wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mazoezi.
Wanafunzi wanaolelewa kimichezo na kituo hicho wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mazoezi.
Wanafunzi wakimenyana uwanjani.
Wanafunzi wakiwa kwenye mazoezi katika kituo hicho.
Mazoezi yakiendelea.
Mchezaji wa kike akionesha kipaji cha kucheza mpira
Vipaji vikioneshwa na wanafunzi hao.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad