Bendera ya Taifa
........................
Na Godwin Myovela
Tanzania ipo katika kipindi kigumu cha kutafakari na kuponya nafsi ya taifa. Tumepitia siku ngumu — siku zilizojaza hewa ya huzuni, mashaka, maumivu na maswali yasiyo na majibu.
Baadhi ya Watanzania wamepoteza ndugu zao, wengine wamejeruhiwa, na wengi wanabeba majeraha yasiyoonekana — yale ya moyoni.
Uchaguzi mkuu na matukio ya maandamano yaliyofuata kwa takribani siku 5 kuanzia Oktoba 29 yameacha alama nzito katika historia yetu. Ni kweli, tumepoteza, lakini tusipoteze taifa lenyewe.
Ni wakati wa kutulia. Wakati wa kuangalia mbele kwa busara, si kwa hasira. Wakati wa kujifunza, si kulaumiana. Wakati wa kujenga, si kubomoa.
Kama mama wa taifa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anakabiliwa na jukumu zito — si la kisiasa tu, bali la kihistoria. Taifa linamtazama. Dunia inasikiliza. Na Watanzania, hasa vijana, wanahitaji kuona matumaini.
Hotuba yake ya kuapishwa ilikuwa na sauti ya faraja na matumaini, lakini hotuba anayotarajia kutoa wakati wa kufungua Bunge inatarajiwa kuwa dawa ya moyo wa taifa.
Ni wakati wa kuzungumza kwa upendo, kwa ujasiri, na kwa hekima. Ni wakati wa kusema: “Tanzania inasamehe, Tanzania inajenga upya, Tanzania inaendelea.”
Vijana ndio moyo wa taifa letu. Lakini nguvu bila mwelekeo ni dhoruba. Hasira bila dira ni moto unaotuteketeza wenyewe. Vijana wa Tanzania wasimame leo si kama wapiganaji wa hasira, bali kama walinzi wa amani.
Wajifunze kwamba mabadiliko ya kweli hayaji kwa ghasia, bali kwa hoja, maadili na umoja.Tujifunze kutoka kwenye historia za mataifa mbalimbali kwamba damu haijengi taifa — hekima ndiyo msingi wa ujenzi.
Kuna wakati mamlaka hufikiri nguvu ni sauti. Lakini nguvu ya kweli ni kusikiliza. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ni nguzo ya amani yetu, lakini sasa zaidi ya yote vinapaswa kuwa ngao ya haki.
Tusitafute adui miongoni mwa watanzania wenzetu; adui wetu wa kweli ni chuki, hofu na ubaguzi. Ni wakati wa kurudisha imani kati ya dola na raia.
Waandishi wa habari nao wasinyamazishwe — bali waongoze kwa hekima. Hii si saa ya kurusha lawama, bali ya kutafuta suluhu. Kalamu isiwe silaha ya hasira, bali taarifa ya uponyaji. Vyombo vya habari viwe daraja la kuelewana, si ukuta wa kugawanya.
Tanzania ni kama moyo unaopiga kwa mapigo mawili — Bara na Zanzibar. Tukipoteza usawa kati ya haya mapigo, taifa letu litaishi kwa mshtuko wa moyo wa kisiasa na kijamii.
Ni wakati wa kujenga tena imani ya kidugu, kuheshimiana, na kushirikiana bila mashaka. Zanzibar si upande wa pili wa bahari — ni upande wa pili wa moyo wetu.
Uwekezaji hauji kwenye kelele, bali kwenye utulivu. Dunia inaitazama Tanzania — je, tuna amani ya kweli au ni utulivu wa bandia? Serikali yetu inapaswa kutoa ishara wazi kwamba Tanzania ni bandari salama ya uwekezaji, biashara, na matumaini.
Hii ni saa ya kurejesha imani ya ndani na nje.
Tusinyanyue mikono kumlaumu mwingine. Kwa sasa, tusitafute nani alikosea, bali tuone wapi tunaanzia kuponya. Tusisahau kwamba damu ya Mtanzania ni takatifu — iwe ya mfuasi wa chama chochote au dini yoyote.
Ni wakati wa kutamka kwa dhati: “Hatutaki visasi, tunataka Tanzania.” Taifa letu ni kama mti uliotingishwa na upepo mkali — matawi mengine yamevunjika, lakini mzizi uko hai.
Mzizi huo ni umoja wetu, utu wetu, na imani yetu kwa Mungu.Tuungane kama watoto wa nyumba moja. Tuwape pole walioumia, tuwape heshima waliopoteza maisha, na tuendelee kama taifa lenye maono mapya.
Tanzania itabaki imara ikiwa tutaamua kuiponya — si kwa maneno, bali kwa matendo ya upendo, msamaha na haki.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu awaponye Watanzania wote.
Ishara ya Umoja na Mshikamano wa Taifa.






No comments:
Post a Comment