Uchumi wa wilaya kuimarishwa kupitia Kilimo
Asisitiza rasilimali ardhi kulindwa, aonya tabia za uuzaji usiofuata taratibu pamoja na suala la makazi holela.
Mbunge wa Jimbo la Kilindi, Salehe Mbwana Mhando akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi Desemba 6, 2025.
....................................
Na Mashaka Kibaya, Kilindi.
MBUNGE wa Jimbo la Kilindi Salehe Mbwana Mhando amewata madiwani kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali ardhi huku akiasa uuzaji usiofuata taratibu na ujenzi holela hatua ambayo itawezesha kuharakisha maendeleo.
Mhando ametoa nasaha hizo Desemba 6, 2025 wakati akizungumza katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani tangu kumalizika Kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ambapo amehimiza ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wadau wilayani humo.
Katika Salaam zake baada ya kupatiwa fursa ya kuzungumza, Mhando almaarufu 'Kitochi' alisema, wilaya hiyo imebahatika kuwa na ardhi nzuri iliyokosa kufanyiwa uwekezaji wa kutosha huku akitanabaisha kuwa sasa wakati umefika kufanya mabadiliko.
Alisema, wataalam wakipewa ushirikiano utakaowawezesha kuonesha umahiri na ubunifu wao kazini kwa kuja na kilimo cha mazao yenye tija kupitia ardhi iliyopo itakuwa muhimu ya kuitangaza Kilindi kitaifa na hata kimataifa na kuifanya wilaya hiyo kuwa ya kupigiwa mfano.
Kutokana na hali hiyo ameasa uuzaji na ujenzi holela huku akiwasihi wajumbe wa baraza la madiwani kwenda kusimamia suala hilo kwenye maeneo yao huku akiwahimiza kuimarisha ushirikiano hatua aliyoieleza kusaidia kufikia lengo.
"Lazima tukasimamie sawa sawa ardhi, isiuzwe bila taratibu kufuatwa, kusiwepo makazi holela.Tukishirikiana tunakwenda kujenga Kilindi mpya"alisema Mhando na kuongeza kuwa wananchi wameonesha imani kubwa na viongozi wao na ndio maana wamewachagua Kwa kura nyingi.
"Wananchi wa Kilindi wanahitaji mabadiliko ya kweli sio mzaha... ndio sababu imani yao kwetu imekuwa kubwa, tumepata imani kubwa kabla ya kutenda, wananchi wamenieleza hawaridhishwi na miundombinu ya barabara tukishirikiana lami itafika Kilindi ndani ya miaka mitano"alisema Mhando.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa CCM, kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara wilayani Kilindi itakuwa fursa muhimu kwa wananchi kuweza kusafirisha mazao yao na kurahisisha upatikanaji wa huduma nyingine ambazo imekuwa kikwazo katika kuzifikia.
Pia Mhando alisema, Kilindi kuna shida ya maji, akisema viongozi wana kila sababu kushirikiana katika kupata suluhisho ya changamoto hiyo ambapo ashauri kujengwa kwa utamaduni wa kuwaenzi watumishi wachapakazi na kwamba kwa wale watakaokuwa vikwazo hawatokufumbiwa macho.
Katika mkutano huo madiwani ulitumika kwa wajumbe kula kiapo na kumchagua Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu wake, mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo,Tamko Ally, ambaye alimtangaza Dkt Michael Samwel Chabai kuwa Mwenyekiti na Mariam Mjela kuwa Makamu wake wakipata kura zote za ndio.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Hashim Mgandilwa aliwataka madiwani kufahamu wajibu mkubwa walionao katika majukumu wanayopaswa kwenda kuyatekeleza kwenye maeneo yao huku akiwasihi kuirejea kwa makini ilani iliyopo sanjari na kujenga utamaduni wa kufuatilia hotuba za viongozi wakubwa.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.















No comments:
Post a Comment