MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA KILINDI ATAKA UKUSANYAJI WA MAPATO - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 8 December 2025

MWENYEKITI HALMASHAURI YA WILAYA KILINDI ATAKA UKUSANYAJI WA MAPATO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga,Dkt Michael Samwel Chabai, akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi Desemba 6, 2025 ambapo aliwahimiza madiwani kusimamia ukusanyaji wa mapato.

..................................

Na Mashaka Kibaya, Kikindi

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga,Dkt Michael Samwel Chabai amewataka madiwani kuwa wasimamizi wazuri wa ukusanyaji mapato sanjari na kuwa wabunifu wa vyanzo husika hatua ambayo itasaidia kufanikisha miradi mingi ya maendeleo.

Dkt Chabai ametoa wito huo juzi wakati akiwasilisha shukrani zake baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa wa uenyekiti wa halmashauri nafasi ambayo atahudumu kwa muda wa miaka mitano.

Katika mkutano huo wa kwanza wa baraza la madiwani ambalo wajumbe waliutumia 'Kuapa' na kuchagua  viongozi wao, Mgeni rasmi ambaye ni Katibu tawala wa wilaya,Tamko Ally, pia alimtangaza Mariam Majele kuwa makamu Mwenyekiti ambapo wote wawili walishinda kwa kura zote za ndio.

Kuhusu umuhimu wa ukusanyaji mapato, Dkt Chabai alisema,madiwani wanapaswa kuwa wabunifu wa vyanzo vipya huku wakiwa wasimamizi wazuri hatua ambayo itasaidia kupata fedha za kuiendesha Halmashauri hiyo ya Kilindi.

"Nianze kuwashukuru wajumbe kwa kutuamini, nitahakikisha umoja na mshikamano vinaimarika...twendeni tukashirikiane kusimamia ukusanyaji mapato pia tuwe wabunifu wa vyanzo vipya "alisema Dkt Chabai wakati akiwasilisha shukrani kwa wajumbe.

Aidha alizungumzia changamoto ya migogoro ya ardhi akisema,madiwani wanapaswa kuhakikisha kero hiyo namalizika kwa amani bila kuanzishwa mingine na iwapo watakumbana na vikwazo waviwasilishe ngazi nyingine.

Pamoja na hayo amesisitiza umuhimu wa madiwani kwenda kutekekeza ahadi zao walizowaahidi wananchi wakati wakiwaomba kura ambapo pia alitumia fursa hiyo kuwasihi kufuata miongozo.

Ili kuweza kutekekeza majukumu yao kwa ufanisi, Dkt Chabai aliwakumbusha madiwani kuona umuhimu wa kujifunza na hata kujiendekeza zaidi kielimu, akitejea ahadi za mwanaCCM inayosema "nitajielimisha kadri ya uwezo wangu".

Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi, Rajabu Kumbi alisisitiza mshikamano miongoni mwa wadau wilayani humo huku akitanabaisha kwamba uchaguzi umemalizika na sasa ni kufanya kazi.

Alisema kuwa,inawezekana nyakati za uchaguzi kwa namna moja ama nyingine watu walikinzana, na kama hilo lilitokea jambo la msingi ni kusameheana hatua ambayo itasaidia kuijenga Kilind mpya.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad