BOT YAONYA WANAOBADILISHA FEDHA BILA YA KUWA NA LESENI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, January 22, 2026

BOT YAONYA WANAOBADILISHA FEDHA BILA YA KUWA NA LESENI

 Afisa Mchambuzi Masuala ya fedha wa benki hiyo, Charles Kanuda, akizungumza kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Fedha Kitaifa yanayoendelea viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara Jijini Tanga.

....................................... 

Na Mashaka Kibaya,Tanga.

BENKI Kuu ya Tanzania (BOT) imewataka watu wanaojihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kuacha mara moja vitendo hivyo.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mkuu Mwandamizi wa benki hiyo, Mwile Kauzeni, wakati akizungumzia na Waandishi wa habari kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Fedha Kitaifa yanayoendelea viwanja vya Shule ya Sekondari ya Usagara Jijini Tanga.

“ Tunawataka watu hao wanaojihusisha biashara hiyo kufuata sheria ambayo itawawezesha kupata leseni inayoruhusu uendeshaji wa shughuli zao,” alisema Kauzeni.

Mwile aliyasema hayo alipokuwa akijibu baadhi ya maswali ya wanahabari waliotaka kujua hatua zinachukuliwa na benki hiyo katika kudhibiti watu hao.

Alisema ili mtu afanye biashara hiyo anapaswa kufuata taratibu za kisheria vinginevyo atakuwa ametenda kosa la jinai hivyo wenye nia kuendesha shughuli hiyo watembelee matawi ya benki hiyo kwa maelezo zaidi.

Charles Kanuda ambaye ni Afisa Mchambuzi Masuala ya fedha wa benki hiyo alisema Serikali imekuja na mfuko wa udhamini wa mikopo ambapo kwa mtanzania anayehitaji huku akiwa hana dhamana toshelevu atapata dhamana mpaka asilimia 75.

Kanuda alisema watu wengi wamekuwa wakijaribu kwenda kukopa huku wakiombwa dhamana yenye thamani kubwa zaidi ya mikopo wanayohitaji hivyo kushindwa kupata mikopo.

Amesema hali hiyo imewasababisha watanzania wengi kushindwa kuchukua mikopo au kuchukua kiasi kidogo jambo ambalo limeathiri ufanisi wa biashara zao wanazoziendesha.

Kauli Mbiu ya maadhimisho hayo ni “Elimu ya fedha , msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi"

Kwa upande wake Mwalimu Mwajuma Kileo wa Shule ya Msingi Mkwakwani jijini hapa alisema ameridhishwa na elimu aliyoipata baada ya kutembelea banda la benki hiyo.

“ Kwa kutembelea banda hilo pamoja na wanafunzi wetu wamejifunza namna ya kutambua fedha bandia mambo ambayo tulikuwa hawayajui ingawa tulikuwa tukiwafundisha kupitia somo la uraia,” alisema Kileo.

Adrus Mahmoud (12) mwanafunzi wa darasa la sita wa Shule hiyo alisema amefarijika kupatiwa elimu ya ziada juu ya kutambua alama za kificho zilizomo kwenye noti hivyo kumsaidia kuzibaini.

Afisa Mkuu Mwandamizi wa benki hiyo, Mwile Kauzeni, wakati akizungumzia na Waandishi wa habari
 Mwanafunzi  Adrus Mahmoud (12), akizungumza.

Mwalimu Mwajuma Kileo wa Shule ya Msingi Mkwakwani  akizungumza.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad