Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Joseph Mkude, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi na kwa wakati huku akibainisha kuwa bima ya afya ni nguzo muhimu katika kufanikisha lengo la afya kwa wote.
Mhe. Mkude alitoa kauli hiyo jana baada ya kupima afya yake katika kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali inayotekelezwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na JKCI.
Alisisitiza kuwa bima ya afya ina mchango mkubwa katika kuwezesha wananchi kupata matibabu ya kibingwa ikiwemo huduma za magonjwa ya moyo ambazo mara nyingi hugharimu fedha nyingi endapo mgonjwa atalazimika kujilipia binafsi. Alieleza kuwa kupitia bima ya afya, wananchi hupata fursa ya kufanyiwa vipimo vya kina, kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa na kuanza matibabu kwa wakati bila kikwazo cha gharama.
“Kujiunga na bima ya afya kunalinda familia dhidi ya mshtuko wa kifedha unaoweza kujitokeza pindi mmoja wao anapokumbwa na ugonjwa unaohitaji matibabu ya muda mrefu au ya kibingwa, ninatoa wito kwa jamii kuchukua hatua mapema kwa kujiunga na mifumo ya bima ya afya. Katika wilaya ya Arusha tumezindua mpango wa mafunzo katika ngazi ya wilaya, kata na mitaa”, alisema Mhe. Mkude.
Akizungumzia kambi hiyo ya matibabu, alisema ni fursa adhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi, hali ambayo awali ilikuwa ikiigharimu familia nyingi fedha na muda mwingi.
Aidha, alisema amefika ALMC kupima afya ya moyo wake akiwa pamoja na wanafamilia wake, akiwahimiza wananchi kuutumia mwanzo wa mwaka 2026 kama chachu ya kuzingatia na kuboresha afya zao.
Naye Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iraghe, aliipongeza kambi hiyo huku akisema itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri kwenda kutafuta huduma za kibingwa nje ya mkoa.
Alisema amehudhuria kambi hiyo akiwa ameambatana na madiwani wa kata za Jiji la Arusha baada ya kuwahamasisha viongozi hao kujitathmini kiafya ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Alifananisha vifaa vinavyotumika katika kambi hiyo na vile alivyoviona alipowahi kupata matibabu nchini India, akisema havina tofauti kwa ubora.
Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Arusha, Minata Salastule, alisema ameridhishwa na huduma alizopata katika kambi hiyo, huku akiwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kupima afya zao. Alieleza kuwa vipimo vinatolewa kwa haraka, havichukui muda mrefu na vinamwezesha mgonjwa kupata ushauri wa kitaalamu na kurejea nyumbani mapema.
Aliongeza kuwa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi ili wengi zaidi wajiunge, kwani bima huwasaidia kupata huduma hata pale wanapokosa fedha taslimu. Alishukuru juhudi za JKCI na ALMC kwa kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi wa Arusha.
Kwa upande wao waandishi wa habari waliopata nafasi ya kupima afya zao katika kambi hiyo walisema mara nyingi huwa mstari wa mbele kuripoti masuala ya afya lakini hujisahau wao wenyewe. Walitoa wito kwa waandishi wenzao na wananchi kwa ujumla kujitokeza kupima afya, hususan ya moyo ili kulinda uhai wao na kuendelea kuitumikia jamii.
Mwandishi wa Habari wa ITV, Arnord Rweyemamu aliomba Serikali na wadau wa sekta ya afya kuendelea kusogeza huduma za kibingwa hadi maeneo ya vijijini, ambako wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo huku akisisitiza kuwa afya njema ni msingi wa maendeleo ya jamii.







No comments:
Post a Comment