DC KILINDI AHIMIZA UKUSANYAJI MAPATO KWENYE MINADA, MAZAO - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, 29 January 2026

DC KILINDI AHIMIZA UKUSANYAJI MAPATO KWENYE MINADA, MAZAO

p>

 Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa akizungumza kwenye kikaao cha baraza la madiwani kilichoketi Januari 28, 2026 mkoani Tanga

........................

Na Mashaka Kibaya, Kilindi 

MKUU wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Hashim Mgandilwa, amewataka  Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, kuhakikisha minada ya mifugo na ya mazao inatumika vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

Mgandilwa ametoa wito huo  kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Januari 28,  2026 na kueleza kwamba kuna umuhimu mkubwa kwa halmashauri kudhibiti vyanzo vya mapato akitaja Minada na Mazao, akishauri ukusanyaji wa mapato yake kufanyika kwa asilimia 100% wakati wakiendelea kufikiria vyanzo vingine.

Alisema ili halmashauri iweze kupata nafasi ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ni lazima kuangazia kwenye suala la ukusanyaji mapato, akitoa msisitizo kwa baraza la madiwani kusimamia vyanzo hivyo.

"Msisitizo wangu mkubwa kwenye baraza ni lazina kwenye vyanzo shikika ambavyo kimsingi ndivyo tunavitegemea ikiwemo minada na mazao ni kuhakikisha tunakusanya kwa asilimia 100,"alisema Mgandilwa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema, bado kuna mianya ya ukusanyaji wa mapato kwa baadhi ya watu kuhusika na utoroshaji wa mazao na vyanzo vingine huku akibainisha uwepo wa mashine 'POS' chache za ukusanyaji mapato kwenye minada.

Kutokana na hali hiyo,wako baadhi ya watu wanauziana bidhaa na kuondoka bila ya kulipa ushuru huku wakiwepo wengine wanaonunua na kuuza mifugo nje au pembezoni mwa minada husika.

Pamoja na hayo, Mgandilwa alisema, iko haja ya kufanyika kwa uwekezaji wenye lengo la kupata faida kuliko kusubiri vyanzo visivyo na uhakika vikiwemo vile ambavyo vimekuwa vikitegemea mvua.

"Tunatakiwa kuondoka na kuanza kufikiri kufanya uwekezaji wa miradi mingine, ambapo kwa namna moja ama nyingine inaweza kutuzalishia fedha ambazo zitatumika kutekeleza miradi"alisema Mgandilwa.

Aidha alisema, iwapo kutafanyika uwekezaji utakaowezesha upatikanaji wa mapato mengine kuna uwezekano wa halmashauri ya wilaya ya Kilindi kuwa miongoni mwa zile zinazofanya vizuri kwenye suala la ukusanyaji wa mapato.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Dkt Michael Chabai alisema,wanakabiliwa na uwepo wa miradi mingi viporo kama vyumba vya madarasa na mingine hali ambayo imechangiwa na mazingira inayotekelezwa akitaja suala la kuongezeka gharama za ziada.

Dkt Chabai alisema ongezeko la gharama za ziada limesababisha fedha zinazotengwa kutokutosheleza ,ambapo hata hivyo halmashauri imejipanga kutumia mapato yake ya ndani katika kukamilisha miradi hiyo.

Dkt Chabai amesema, katika bajeti zinazofuata, halmashauri itatenga fedha kwa kadri zitakavyopatikana utaratibu ambao utaweza kusaidia ukamilishwaji wa miradi viporo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad