DIWANI AWAONDOA HOFU WAKAZI KIVULE, UJENZI BARABARA YA BANANA, MSONGOLA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, January 9, 2026

DIWANI AWAONDOA HOFU WAKAZI KIVULE, UJENZI BARABARA YA BANANA, MSONGOLA

 

Diwani wa  Kata ya Kivule CCM, Rajabu Manyinya akizungumza Januari 7, 2025   kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Kikundi cha Uwezo Community Micro Finance (UWEZO), uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

...................................  

 Na Mwandishi Wetu.             

DIWANI wa Kata ya Kivule, Ilala jijini Dar es Salaam, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Manyinya, amewaondoa hofu wananchi, baada ya kusema miundo mbinu ya barabara kutoka Banana hadi Msongola ujenzi wake utakamilika kwa kiwango cha lami.

Hayo aliyasema jana, Januari 7, 2025 kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Kikundi cha Uwezo Community Micro Finance (UWEZO), uliofanyika jijini Dar es Salaam. 

Manyinya ambaye alikuwa mwalikwa katika mkutano huo, alisema wakazi wa Kivule wasiwe na wasiwasi juu ya ujenzi wa barabara hiyo, kwani mkandarasi anaendelea na kazi.

Alisema kuwa tayari kipande cha Msongola, mkandarasi ameanza kutandaza kokoto kwa ajili ya kuweka lami.

Diwani huyo aliwataka wananchi wa kata hiyo kuachana na maneno ya baadhi ya watu wanaobeza  ujenzi wa barabara hiyo.

"Baadhi ya watu wanasema barabara kutoka Banana hadi Msongola ujenzi wake hautaendelea kwa sababu ilikuwa ni siasa za kampeni ya uchaguzi, niwahakikishie, mimi na mbunge wa Jimbo la Kivule,  Ojambi tutasimamia ujenzi wa barabara hii" alisema Manyinya.

Manyinya alisema pamoja na kero kubwa ya Kivule ni barabara za ndani ya mitaa, lakini ameanza kuishughulikia ambapo wanatarajia kuweka vifusi ili ziweze kupitika muda wote. 

Wakati huo huo, Diwani huyo aliwapongeza viongozi wa UWEZO kwa kushirikiana na wenzao SSI_Group & SS Foundation kuchangia damu ukiwa ni mpango wa Taifa wa damu salama.

Diwani huyo ambaye alikuwa ni mmoja waliochangia damu, alisema kwake tukio hilo ni kubwa, kwani linalenga kuokoa maisha ya watu wengi.               Alisema akiwa diwani wa kata hiyo ataunga mkono vikundi vyote.

Manyinya alisema UWEZO ni kikundi ambacho kina viongozi makini na wana malengo ya kweli ya kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja. 

Awaomba wakazi wa Kivule na maeneo mengine kujiunga na kikundi cha UWEZO ili waweze kununua hisa na kukopa mikopo ya kibiashara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad