...........................
Na Dotto Mwaibale, Tanga
MAKAMU wa pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga Mhe. Hemed Suleiman Abdullah anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 49 tangu kuzaliwa kwa chama hicho Februari 5, 1977.
Maadhimisho hayo yatafanyika kimkoa wilayani Muheza na yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa chama, Serikali, wananchi na wadau mbalimbali.
Februari 01, 2026 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abraham atayazindua rasmi maadhimisho hayo wilayani Lushoto.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu Januari 30, 2026 Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Samwel Kiondo Mngazija alisema maandalizi ya uzinduzi wa maadhimisho hayo kimkoa yanaendelea vizuri.
“Maandalizi ya uzinduzi wa maadhimisho hayo yanaendelea vizuri na hivi sasa tupo wilayani Lushoto kwa ajili ya maandalizi hayo yatakayofanyika kimkoa Februari 01, 2026,” alisema Kiondo.
Kiondo alisema katika ngazi zote za kata na wilaya maadhimisho hayo yanaendelea ambapo wataungana nao kwenye kilele chake wilayani Muheza Februari 5, 2026.
Alisema Jumuiya zote za chama hicho kuanzia ya Wazazi, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM) zinafanya maadhimisho hayo kwa kufanya shughuli mbalimbali kwa kufuata ratiba ilivyopangwa.
Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Samwel Kiondo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi na wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi wa maadhimisho hayo wilayani Lushoto na siku ya kilele chake wilayani Muheza.
Alitaja baadhi ya shughuli ambazo zitafanyika siku hiyo ya uzinduzi wa maadhimisho hayo kuwa ni kupanda miti, kutembelea na kuwajulia hali wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto na baada ya hapo Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abraham atahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara.
Taarifa hii imeaandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990.








No comments:
Post a Comment