...........................
Na Dotto Mwaibale, Tanga
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abraham anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 49 tangu kuzaliwa kwa chama hicho Februari 5, 1977.
Uzinduzi huo utafanyika kimkoa wilayani Lushoto na yanatarajiwa kuhudhuriwa na mamia ya watu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu Januari 30, 2026 Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Samwel Kiondo Mngazija alisema maandalizi ya uzinduzi huo kimkoa yanaendelea vizuri na yatafanyika Februari 01, 2026 wilayani Lushoto.
“Maandalizi ya uzinduzi wa maadhimisho hayo yanaendelea vizuri na hapa ninapozungumza nanyi tupo wilayani Lushoto kwa ajili ya maandalizi hayo,” alisema Kiondo.
Kiondo alisema katika ngazi ya kata na wilaya maadhimisho hayo yanaendelea ambapo wataungana nao kwenye kilele chake wilayani Muheza Februari 5, 2026 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamo wa Pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga.
Alisema Jumuiya zote za chama hicho kuanzia ya Wazazi, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) zinafanya maadhimisho hayo kwa shughuli mbalimbali za chama na kijamii.
Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Samwel Kiondo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi na wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi huo.
Kiondo aalisema katika uzinduzi huo kutakuwa na matukio mbalimbali kama kupanda miti, kutembelea na kuwajulia hali wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto na baada ya hapo Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, Rajabu Abraham atahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara.








No comments:
Post a Comment