..........................
Na Dotto Mwaibale
WAZIRI wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ameonesha dhamira ya dhati ya kubadilisha Tasnia ya Habari Mtandaoni nchini kwa kutoa ahadi ya kuiomba Serikali kutenga Sh. bilioni
moja hadi bilioni mbili kwa ajili ya kuwakopesha ili waweze kununua vifaa vya
kufanyia kazi.
Makonda ameonesha dhamira
hiyo Januari 13, 2026, wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo Mtumba
jijini Dodoma katika hafla ya makabidhiano ya ofisi kati yake na aliyekuwa Waziri
wa Wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi.
“Mhe. Katibu Mkuu vijana wengi wa taifa letu wamejiajiri kwenye habari hasa online TV na wanaotumia mitandao ya kijamii tutaiomba mamlaka na Mhe. Rais anapenda sana vijana wa Social Media.
Nitaenda kumlilia atupatie fedha kiasi cha sh. bilioni moja hadi bilioni mbili tuwakopeshe waandishi wa habari za mitandaoni waweze kununua vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi,” alisema Makonda.
Alisema wakipata fedha
hizo watawapatia waandishi hao ili wawe na vifaa vyao wenyewe na wanaporekodi
wasitumie simu badala yake watumie kamera za kisasa, na kompyuta nzuri na kuweza kutengeneza
maudhui ambayo dunia itaiona Tanzania katika ubora wake.
Ahadi hiyo ya Makonda inakwenda sanjari na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Desemba 18, 2025 Katibu Mkuu wa
wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari wa mitandaoni na bloga katika kikao kazi kilicho andaliwa
na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alitoa salamu za Rais kuwa ameomba
waandishi hao walelewe.
Msigwa alisema Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulea na kuwawezesha
waandishi wa habari wa mitandaoni na mabloga,
Alisema Tanzania Bloggers
Network (TBN) na Jukwaa la Mitandao Tanzania (JUMIKITA) kuwa ni wadau wakubwa
wa serikali katika tasnia ya habari, akisisitiza kuwa mchango wao ni muhimu
katika kusambaza taarifa na kujenga mawasiliano kati ya serikali na wananchi.
“Serikali imewaamini waandishi wa mitandaoni, sasa nanyi
muendelee kuonesha imani kwa serikali. Ushirikiano wetu umeendelea kuimarika na
changamoto zinazojitokeza tunazitatua kwa pamoja,” alisema Msigwa.
Aidha, Msigwa alieleza kuwa wizara hiyo ipo katika mchakato wa
kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha waandishi wa habari, hususan wa
mitandaoni.








No comments:
Post a Comment