DIWANI MANYONI ATOA VIFAA VYA SHULE KWA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, January 14, 2026

DIWANI MANYONI ATOA VIFAA VYA SHULE KWA WANAFUNZI KIDATO CHA KWANZA

 Diwani wa Kata ya Mkwese iliyopo Halmashauri ya Wilaya Manyoni Mkoa wa Singida Mhe. Ng'wigulu Shigella (katikati kushoto) akiwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari ya Mpambaa wakati wa hafla ya kuwakabidhi vifaa vya shule iliyofanyika Januari 14, 2026.

........................... 

Na Dotto Mwaibale

KUJITOA kusaidia watu wengine ni jambo jema na pia ni kitendo cha baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya watu wanafikiri kutoa msaada wowote ni lazima uwe mkubwa kumbe msaada hata ukiwa mdogo kutokana na uwezo wa mtoaji kwa mpokeaji utakuwa mkubwa.

Kutoa ni moyo wa mtu na siyo utajiri hivyo tupaswa kujenga tabia ya kutoa msaada kwa wenzetu kama vitabu vitakatifu vya  dini zote vinavyotuelekeza.

Tabia ya kutoa inalinda na kuheshimu utu wa mtu kwa kumpatia chakula,  malazi, mavazi, huduma za afya, vifaa vya shule na mahitaji mengine ya kibinadamu ambayo yanadumisha upendo, amani na mshikamano miongoni mwa jamii. 

Hapa napenda nimzungumzie Diwani wa Kata ya Mkwese iliyopo Halmashauri ya Wilaya Manyoni Mkoa wa Singida Mhe. Ng'wigulu Shigella.

Diwani huyu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo kwanza ameanza kazi rasmi ya kuwatumikia wananchi wa kata hiyo kwa vitendo huku akishirikiana nao kwa kila jambo.

Kutokana na kuwiwa kuwatumikia wananchi wake jicho la utumishi wake hasa katika majira haya ya msimu wa watoto kwenda shule aliona aungane na baadhi ya wazazi na walezi ambao watoto wao wanaenda kuanza kidato cha kwanza kwa kuwanunulia vifaa vya shule.

vifaa vilivyotolewa na kukabidhiwa kwa watoto hao 109 ni daftari aina ya “Counter Book” sita kwa kila mwanafunzi,

Watoto walionufaika na msaada huo ni ambao wameanza kidato cha kwanza  Shule ya Sekondari ya Mpambaa iliyopo katika kata hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Shigella alisema ameona aungane na wazazi na walezi wa watoto hao kwa ajili ya kusaidia vifaa hivyo vichache kwa  kuwapa watoto hao ikiwa kama motisha kwao ya kuanza kidato cha kwanza.

“Watoto wetu ndiyo mnaanza masomo ya kidato cha kwanza wito wangu zingatieni masomo yenu hasa ya mchepuo wa sayansi ambayo ndiyo msingi mzuri wa maendeleo yenu na kufuata mnachoelekezwa na walimu wenu msijiingize kwenye vitendo visivyofaa,” alisema Shigella.

 Aidha, Shigella alisema msaada huo ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwaunga mkono wazazi na walezi  ambao wameonesha jitihada za kuwasimamia watoto wao vizuri hadi kufikia hatua ya kuanza kidato cha kwanza.

Diwani Shigella alisema pia amefanya hivyo ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anahimiza elimu bure kwa watoto kuanzia shule ya awali hadi sekondari hivyo kuwapunguzia wazazi mzigo wa kuwasomesha na kueleza kuwa utaratibu huo utakuwa endelevu kila mwaka.

    m    he. Shigella akikabidhi vifaa hivyo.
Wanafunzi wa shule hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Shigella wakati wa kukabidhiwa vifaa hivyo. 

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad