MFUKO WA BIMA YA AMANA UMEONGEZEKA HADI KUFIKIA SHILINGI TRILIONI 1.46 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, January 24, 2026

MFUKO WA BIMA YA AMANA UMEONGEZEKA HADI KUFIKIA SHILINGI TRILIONI 1.46

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, akizungumza na Waandishi wa Habari Januari 22, 2026 Jijini Tanga

Na Waandishi Wetu, Tanga

MFUKO wa  Bima ya Amana umeongezeka kutoka Sh. Bil 1.5 zilizotolewa na Serikali wakati wa kuanzishwa kwake  mwaka 1994 hadi kufikia Sh. Trilioni 1.46 mwaka 2025 ambazo zimetokana na michango ya kila mwaka kutoka kwa wanachama na faida inayotokana na uwekezaji katika dhamana za Serikali.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa bodi hiyo Lwaga Mwambande, Januari 22, 2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa yanayoendelea kufanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari  Usagara Jijini Tanga.

 Mwambande alisema

lengo la kuanzishwa kwa Bodi ya Bima ya Amana ni kuwalinda wenye amana ndogo kutokana na athari ya kupoteza amana zao pindi benki au taasisi ya fedha inapofilisika utaratibu ambao unauwezesha umma kuendelea kuwa na imani na mfumo wa fedha nchini Tanzania.

"Bodi ya Bima ya Amana 'Deposit Insurance Board' ni taasisi iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha mwaka 1991.Kufuatia kufutwa kwa sheria hiyo bodi imeendelea kuwepo na kufanya kazi kwa mujibu wa kifungu cha 36 hadi 42 cha sheria ya mwaka 2006," alisema Mwambande.

Kuhusu suala la uanachama, Mwambande alisema ni kila benki au taasisi ya fedha iliyopewa leseni na benki Kuu ya Tanzania ( BoT), kufanya shughuli au biashara ya benki nchini inapaswa kuchangia  kwenye mfuko wa Bima ya Amana.

Mwambande alitumia fursa hiyo kuzungumzia kazi za bodi ya bima ya amana akisema ni kukusanya michango ya kila mwaka kutoka kwa wanachama ambapo kwa sasa benki na taasisi za fedha zinachangia kwa kutoa kiasi cha asilimia 0.15 cha amana zote kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mwambande aliongeza kuwa benki na taasisi za fedha zina jukumu la kulipa michango kwenye mfuko wa bima ya amana huku wenye amana wakiwa hawawajibiki kuchangia kwenye mfuko huo.

Alitaja kazi nyingine ya Bodi hiyo kuwa ni kuwekeza fedha za mfuko kwa mujibu wa sera ya uwekezaji ya Bodi ya Bima ya Amana na kuwalipa wenye amana kwa mujibu wa sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 pale benki au taasisi ya fedha inapowekwa katika ufilisi.

Alitaja kazi nyingine ni kusimamia ufilisi wa benki au taasisi pale ambapo bodi ya bima ya amana imeteuliwa na benki kuu ya Tanzania kufanya kazi hiyo.  

Aidha, Mwambande amesema kuanzia mwezi Julai 2025, Bodi imeanza kutekeleza jukumu la kupunguza hasara katika inyopitia changamoto ili irejee katika utendaji wa kawaida badala ya kuiacha hadi ife na baadae kulipa fidia na kufilisi kwa gharama kubwa zaidi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad